Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dk.Abdallah Mabodi Aongoza Mazishi ya Kada wa CCM Yaliofanyika Katika Kijiji cha Bwejuu.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akiwa na viongozi mbali mbali wakati wa kuswalia maiti katika msikiti wa Bwejuu.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akiwa na wachama wa CCM na wananchi kwa ujumla katika harakati za mazishi ya  marehemu Hassan Vuai Hassan.

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi leo ameongoza mamia ya wanachama na wananchi katika mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa Kusini Unguja Hassan Vuai Hassan ‘’Nyomboa’’ yaliyofanyika kijijini kwao Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja.

Kada huyo ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa CCM ameumwa ghafla na kufariki dunia jana akiwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja  alikopelekwa kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza Dk. Mabodi katika mazishi hayo amesema CCM imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na imepoteza kada jasiri aliyejitolea kwa muda mrefu kulinda na kutetea maslahi ya chama hicho.

Dk. Mabodi amesema CCM imepata pigo kubwa baada ya kumpoteza mwanachama huyo aliyefanya kazi za chama kwa ufanisi mkubwa bila ya kuchoka na atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa makada wengine wanaotakiwa kumuenzi kwa kufuata nyayo zake.

Pia Dk. Mabodi alitoa salamu za pole kutoka kwa Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein aliyeelezea kusikitishwa kwake na kifo hicho na kuiomba familia ya marehemu kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.

“Marehemu Nyoboa ni mpiganiji mwenzangu tumekuwa wote toka tukiwa wadogo toka enzi za Paunia hadi tukawa wakubwa na tukaendelea kukitumikia chama, alikuwa ni mchapakazi na mtu wa watu.

Nasaha zangu sisi tuliobaki tuendelee kumuombea dua na kumuenzi kwa kufuata nyayo zake.”, alieleza kwa uzuni Dk.Mabodi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja  Ramadhan Ali Abdallah alisema Mkoa huo umepoteza kiongozi na kada muhimu aliyekuwa ni mtu makini na asiyeyumba kwa kile anachoamini kuwa ni sahihi katika kuimarisha chama hicho kiitikadi na kisiasa.

Akisoma wasifu wa Marehemu huyo, Kaimu Katibu wa CCM  Wilaya ya Kusini Unguja, Hafidh Hassan Mkadam amesema marehemu amefariki dunia akiwa na umri wa miaka  66 na ametumikia chama, serikali  na Jumuiya zake kwa nafasi mbali mbali za kiuongozi na kiutendaji.

Marehemu Nyomboa enzi za uhai wake aliwahi kuwashika nyadhifa mbali mbali zikiwemo afisa Utumishi afisi ndogo ya wazazi Zanzibar, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Wete Pemba, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Chunya, Mjumbe wa Kamati ya siasa wa CCM Wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja, Diwani wa Wadi ya Paje na hadi kufa kwake pia alikuwa ni Afisa Usalama na Maadili wa CCM Wilaya ya kusini Unguja.

Katika wasifu wake marehemu ameacha vizuka wawili na watoto 13 na wajukuu 17.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu pahali pema pepo Amini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.