Habari za Punde

ZFA yajiandaa kuzipeleka Zanzibar Heroes, Kenya Zanzibar Queens Rwanda na U 17 Burundi





 Na Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) kimepokea barua kutoka kwa Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuhusu Mashindano mbali mbali wanayoandaa Baraza hilo yakiwemo ya Chalenj kwa Wanaume na Wanawake pamoja na Mashindano ya Vijana.

Akithibitisha kupokea Barua kutoka CECAFA Katibu wa ZFA Mohd Ali Hilali “Tedy” amesema Zanzibar itashiriki Mashindano yote hayo ambapo kwasasa wapo katika mchakato wa kuitafuta timu ya Taifa ya Zanzibar kwa Wanawake (Zanzibar Queens) pamoja na Timu ya Taifa ya Wanaume Zanzibar Heroes.
“Tumepokea barua kutoka CECAFA kuhusu mashindano ya Chalenj pamoja na ya vijana, sisi kama Zanzibar tutakwenda hata kama kwa basi lakini tutashiriki”. Alisema Tedy.

Mashindano ya CECAFA Chalenj CUP kwa Wanawake yataanza rasmi Novemba 3 hadi 12, 2017 huko nchini Rwanda ambapo timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Queens) itashiriki.

Kwa upande wa Wanaume Mashindano ya CECAFA Chalenj CUP yanatarajiwa kufanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 9, 2017 ambapo timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) itashiriki.

Wakati huo huo kutafanyika Mashindano ya Vijana ya CECAFA chini ya miaka 17 nchini Burundi kuanzia Disemba 12 hadi 22, 2017.

Aidha CECAFA pia wameandaa Mashindano mengine ya Vijana ambayo yatafanyika Agost 11 hadi 25,2018 Jijini Dar es salam ambapo timu ya Vijana ya Zanzibar U-17 pia ikitarajiwa kushiriki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.