Habari za Punde

Msiwasafishe watoto wakishabakwa, kulawitiwa


NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAZAZI na walezi nchini, wametakiwa kutowasafisha watoto wao waliobakwa au kulawitiwa, na ikitokezea wamewasafisha, wasisite kuwapeleke hospitali kuwafanyia uchunguuzi, kwani kukosekana kwa maji maji kwenye sehemu za siri, sio kigezo cha kupoteza ushahidi, makamani.

 Kauli hiyo imetolewa na Mwendesha mashitaka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kisiwani Pemba, Mohamed Ali Juma wakati alipokuwa akijibu hoja za wajumbe wa kamati kuu ya mradi wa GEWE, kwenye mkutano uliofanyika uwanja wa Gombani mjini Chakechake.

Alisema kukosekana kwa maji maji maalum au mbegu za kiume kwenye sehemu iliofanyiwa tendo la ulawiti au ubakaji, hakuuwi kesi, kama wengine wanavyofikiria, na wala ushahidi na ubakaji haondolewi kwa kumuosha mtoto.

Mwendesha mashiataka huyo, alieleza kuwa hata kama wazazi au walezi watawaosha watoto wao, waliobakwa au kulawitiwa chamsingi wawafikishe hospitalini, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguuzi wa kitaalamu, na iwapo wamebakwa njia zake za siri zitaonyesha.

Alifafanua, tena ni vyema kwa wazazi na walezi hao watawasafisha watoto waliobakwa au kulawitiwa, ili kuwaepushia na uwezekano wa kukumbwa na magonjwa  mbali mbali kama vile ya zinaa.

“Sisi kesi inapokuja mahakamani za ubakaji, basi daktari anakuja na jawabu kwamba, ameingiliwa na ipo michubuko au michaniko, lakini marenda, mbegu za kiume, maji maji yaliotokana na tendo hilo, wala si ushahidi kamili, basi mpenyo ndio sahihi”,alisema.

Hata hivyo Mwendesha mashitaka huyo, amesema wananchi kuendelea kutofika mahakamani kutoa ushahidi kwa sababu ya rushwa muhali, waelewe kuwa ni kuyanaiwirisha matendo ya udhalilishaji yaliopo nchini.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa jamii wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed, alisema bado wasaidizi wa sheria waliopo majimboni, hawajaibuka vya kutosha kushirikiana na wadau wengine katika mapambano dhidi ya udhalilishaji.

Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Kangagani Awena Salum Kombo, alisema lazima iwepo sheria madhubuti ya kuwaadhibu, wasiotaka kufika mahakamani na kutoa ushahidi.

“Zipo kesi za udhalilishaji zimesababishwa kufutwa, kwa sababu mtu alieshuhudia au alieniletea taarifa za awali, hakuwa tayari tena kwenda mahakamni kutoa ushahidi, lazima kama hawa waadhibiwe”,alifafanua.

Nae sheha wa shehia ya Mchanga mdogo Asaa Makame Said, alisema kuna ahuweni kubwa kwenye shehia yake, ikilinganishwa na miaka minne nyuma, kabla ya kufikiwa na mradi wa kupinga udhalilishaji GEWE.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa GEWE (III)  kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar, Asha Abdi Makame, alisema mradi huo zaidi unakuja kuwajengea uwezo waandishi wa habari, ili waibue habari zilizofanyiwa utatfiti wa kutosha.

“Tayari waandishi wameshapewa elimu, na watapita kwenye maeneo yenu, ili kuwauliza na kutaka takwimu juu ya kesi za udhalilishaji, hivyo wapeni ushirikiano ili wakamilishe kwa wakati”,alifafanua.

Aidha Mwenyekiti wa kamati hiyo ya GEWE Khamis Shaban, alisema lazima jamii waelimishwe, kwamba wasiowaoshe watoto wao waliobakwa au kulawitiwa na ikitokezea wamewasafisha, wasisite kuwafikisha hospitali kwa kufanyiwa uchunguzi.


Mradi wa GEWE III, unatekeleza kwenye wilaya ya Wete kwa Pemba, kwa shehia sita za Kiungoni, Shengejuu, Mchanga mdogo, Kangagani, Mjini ole na Kinyikani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.