Habari za Punde

Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar Riziki Pembe Awataka Wananchi Zanzibar Wabadili Mfumo wa Maisha Kujiepusha na Maradhi ya Kisukari Zanzibar.

 Kaimu Waziri wa Afya ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma akizungumza na waandishi wa habari  katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja kuhusu hali ya maradhi ya kisukari Zanzibar na njia za kujiepusha nayo
Mwakilishi wa Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) Zanzibar Dkt. Ghirmay Andermichael akizungumzia hali ya ugonjwa wa kisukari duniani katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja  (kushoto) Kaimu Waziri wa Afya Riziki Pembe Juma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Halima Mohd Salum akimkaribisha Kaimu Waziri wa Afya Riziki Pembe Juma kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya kisukari duniani katika mkutano uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Kaimu Waziri wa Afya ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma akizungumza na waandishi wa habari  katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja kuhusu hali ya maradhi ya kisukari Zanzibar na njia za kujiepusha nayo

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 14/11/2017.
Kaimu Waziri wa Afya Mhe. Riziki Pembe Juma  amesema ugonjwa wa kisukari unaepukika iwapo mtu atazingatia mfumo bora wa maisha ikiwemo lishe bora na kufanya mazoezi  angalau dakika 30 kwa siku .

Hayo aliyasema wakati alipokuwa akizungumza na waandishi  wa habari  kuhusu maadhimisho ya siku ya kisukari duniani katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja.

Alisema watu bado hawajakuwa tayari kubadilisha mfumo wa maisha na wanaendelea kula chakula ambacho ni kichocheo cha kupata maradhi ya sukari na baadhi ya wanaougua maradhi hayo hupoteza viungo na kupata  ulemavu wa maisha na hatimae hufariki .

Alifahamisha kuwa ongezeko la ugonjwa wa kisukari limekuwa likiathiri jamii ya Wazanzibari wengi na hauchagui rika wala jinsia na hata baadhi ya watoto wameathirika na tatizo hilo jambo ambalo litachangia kupoteza nguvu kazi ya taifa hapo baadae .

Mhe. Riziki ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali alisema katika kuhakikisha kunafatiliwa ustawi wa watoto Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wamefanya uchunguzi wa afya za wanafunzi wa skuli 33 za Unguja na Pemba  kuanzia mwishoni mwezi wa Oktoba mwaka huu kuwachunguza afya zao.

Alifahamisha kuwa utafiti umeonyesha matatizo ya afya yaliyogunduliwa yanahitaji zaidi usimamizi wa jamii kwani suala la lishe na usafi ni mambo yanayoweza kusimamiwa kikamilifu na wazee na walezi majumbani.

“Ongezeko kubwa la watoto wenye kisukari linatutia taharuki ya hali ya juu na linatusukuma kufanya utafiti makhsusi ili tuweze kubaini sababu za ongezeko hili “alisema  Kaimu Waziri wa Afya.

Alieleza kuwa mwaka 2016 kitengo cha kudhibiti maradhi yasioambukiza kiliwapima wafanyakazi 1,948 wa taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kugundua asilimia sita ya wafanyakazi hao wanaviwango vya  juu vya sukari

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya  Afya Halima Moh’d Salum alisema  sababu kubwa ya watoto kupata maradhi ya sukari ni kunasababishwa na kutumia vyakula vya sukari  na vyenye mafuta mengi zikiwemo ambavyo mara nyingi huchangia ongezeko la sukari .

Ameishauri jamii kutumia vyakula vya asili ambavyo vinapatikana kwa wingi Zanzibar na kupunguza matumizi ya vyakula vya mafuta na vyakula vya makopo ambavyo ni hatari kwa afya zao.

Mwakilishi wa shirika la Afya Duniani (WHO ) Zanzibar Dkt.  Ghirmay Andemichael alisema kwa mujibu wa shirika la kimataifa linaloshughulikia maradhi ya sukari  (IDF) hadi kufikia mwaka  2015 kulikuwa na wagonjwa million 415 wa kisukari duniani kote idadi hii inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia million 642 ifikapo mwaka 2040 iwapo nchi hazitoweka mikakati madhubuti ya kudhibiti ugonjwa huu.

Alisema shirika la IDF pia limeripotiwa vifo million tano vitokanavyo na ugonjwa wa kisukari kwa mwaka 2015 takwimu ambazo ni kubwa ikilinganishwa na vifo vinavyotokana na maradhi mengine yanayoonekana hatari  ikiwemo maradhi ya ukimwi kifua kikuu na malaria
Kila ifikapo tarehe  14 Novemba dunia huadhimisha siku ya ugonjwa wa kisukari na kauli mbiu ya mwaka huu ni CHUKUA TAHADHARI ILI KUJIKINGA NA KISUKARI

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.