Habari za Punde

Kamati maalum ya kutokomeza kipindupindu yakutana Zanzibar

 Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohammed Abdallah akiwasilisha mada kwa wajumbe wa kamati ya kutokomea Kipindupindu Zanzibar. 

 Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kutokomeza Kipindupindu Zanzibar wakisikiliza mada zilizokuwa zikiwakilishwa katika mkutano huo.
 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA Dkt. Yahya Hamad Shehe akiwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuhusu mradi wa kupiga ramani mpya ya Zanzibar kwa kutumia ndege maalumu kukusanya taarifa muhimu.
Afisa Habari wa Shirika la UNICEF kutoka Nairobi Maureen Khambira akitoa mchango wake katika mkutano wa kupambana na kipindupindu Zanzibar uliofanyika ukumbi wa uzazi salama Kidongochekundu.

Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhan Ali, Maelezo

Zanzibar itaendeleza juhudi za kupambana na  maradhi ya kipindupindu ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2027 maradhi hayo yanatokomezwa lakini nguvu za pamoja za Taasisi za ndani na nje ya nchi likiwemo Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) zinahitajika kufanikisha juhudi hizo.

Mkurugenzi Tiba na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohd Abdalla alieleza hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa siku mbili uliozishirikisha taasisi za Serikali na taasisi za kiraia katika ukumbi wa uzazi salama Kidongochekundu.

Alisema Wizara ya Afya imeamua kuunganisha sekta mbali mbali za Serikali, za kirai na washirika wa maendeleo wakielewa kuwa kipindupindu hakiwezi kumalizika kwa nguvu za Wizara peke yake.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kila mmoja kwa nafasi ya taasisi anayotoka kuandaa mpango mkakati utakaosaidia kumaliza kabisa kipindupindu Zanzibar ifikapo mwaka 2027.

Alisema Wizara ya Afya inafahamu uzito uliopo wa kufanikisha mpango huo ikiwemo miundombinu isiyoridhisha ya kupatikana maji safi na salama, ujenzi holela katika baadhi ya mitaa na jamii kutokuwa tayari kubadili tabia.

“Jamii kukubali kubadili tabia ili kwenda sambamba na mpango huu nina imani malengo ya kumaliza cholera yanaweza kufikiwa,” alithibitisha Mkurugenzi Tiba.

Dkt. Fadhil alikumbusha kwamba Wizara bado inaendeleza masharti ya afya katika kufanya biashara za vyakula na biashara za vinywaji ambayo ni moja ya vyanzo vikubwa vya kuibuka kipindupindu.

Akizungumza katika mkutano huo Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Ghirmay Andermichael aliwakumbusha wananchi kufuata masharti ya afya ikiwemo kutumia vyoo, maji yaliyochemshwa ama yaliyotibiwa na kunawa mikono kabla na baada ya kula.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha 
Zanzibar (SUZA) Dkt. Yahya Hamad Shehe alisema katika kuchangia kumaliza cholera, Chuo kinaendeleza mradi wa kupiga ramani  mpya ya visiwa vya Zanzibar kwa kutumia ndege maalumu ili kujua sehemu zinazopata maradhi hayo mara nyingi na sababu zake.

Alisema ramani hiyo mpya itakusanya taarifa zote muhimu za Wilaya, shehia na mitaa ili kupata  urahisi wa kushughulikia tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.