Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar , Johari Masoud Sururu alipokuwa akizungumza na watumishi wa Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja alipofanya ziara ya kikazi Mkoani humo tarehe 21 – 22 Novemba, 2017.
Kamishna
wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, amewataka watumishi wa
Uhamiaji Zanzibar kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu sambamba
na Maadili ya Kazi. Aliyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Uhamiaji
Mkoa wa Kusini Unguja alipofanya ziara
ya kikazi Mkoani humo tarehe 21 – 22 Novemba, 2017.
Aidha,
katika kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata huduma bora na stahiki toka Idara
yake, aliwaasa Watumishi kuacha tabia ya kufanyakazi kwa mazowea na kuhakikisha
kwamba kila siku wanafanyakazi kwa juhudi, maarifa na uweledi wa hali ya juu.
Kamishna
Sururu, alitumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa Uhamiaji Mkoani humo, kusimamia vyema majukumu yao kwa mujibu ya
Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. “Nawasihi na kuwataka muelewe kuwa sisi
tumepewa dhamana na Serikali kuwatumikia wananchi, hivyo nidhamu na heshima ya
kazi ndio msingi wa mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yetu”. Ni vyema
kila mtumishi kwa nafasi yake atambue wajibu wake na muda wote tuzingatie
maadili ya kazi, nidhamu na uwajibikaji”. “Tuache kufanya kazi kwa mazowea na
tutoe huduma bila ya upendeleo wa aina yoyote” “Narudia hizi ni nasaha zangu
kwenu, kila mmoja ajitambue na kujua wajibu wake, toeni huduma bila ya
upendeleo, tutumie lugha nzuri na za heshima muda wote” alisema Kamishna
Sururu.
Kwa
upande wa watumishi hao, waliahidi kutekeleza maagizo na maelekezo yaliyotolewa
na Kamishna Sururu kwa vitendo. Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja, Naibu
Kamishna wa Uhamiaji, Mkemimi Mohamed Mhina wakati akitoa taarifa ya utendaji
kazi wa Mkoa huo, alisema “Kipaumbele cha Mkoa wetu ni kuondoa malalamiko
kutoka kwa Wateja na wananchi kwa ujumla, Mkoa wangu umedhamiria na unatekeleza
kwa vitendo dhamira hiyo”
Ofisi
ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja imeboresha Utoaji wa Huduma mbali mbali sambamba
na kusimamia vyema udhibiti wa wageni, kwani Mkoa wa Kusini Unguja ni Mkoa
wenye miradi takriban 162 ya uwekezaji zikiwemo takriban Hoteli
na nyumba za kulala wageni. “Pamoja na changamoto ya uwepo wa Bandari
Bubu zipatazo ishirini na nne (24) na madiko ishirini (20), Udhibiti tunaofanya,
Misako na Doria vimesaidia katika kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya serikali,
kwa kipindi cha mwezi Mei – Oktoba, 2017 tumefanikiwa kukusanya Dola za
Kimarekani 17,500 USD na Shilingi 13,710,000/=” alisema “Naibu
Kamishna Mkemimi.
Kamishna
wa Uhamiaji Zanzibar, akihitimisha ziara yake Ofisini hapo, alisema
“Nimefarijika sana kuona kwamba suala la ukusanyaji wa mapato linapewa uzito
unaostahiki. Tunaelewa Serikali zote mbili zinahimiza ukusanyaji wa maduhuli
ili Serikali ziweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wake na kuwaletea
maendeleo wanayotarajia. Dhamira hiyo haitofikiwa ikiwa sisi watumishi
tutafanya uzembe unaosababisha uvujaji wa maduhuli ya serikali na ubadhirifu wa
fedha kwa kufanya matumizi yasiyo ya lazima”.
Aidha,
Kamishna Sururu, katika ziara hiyo alipata nafasi ya kutembelea maeneo kadhaa
yaliyopo Wilaya ya Kusini na Wilaya ya Kati na kushuhudia Viwanja vilivyotengwa
kwa ajili ya miradi ya uendelezaji Majengo ya Ofisi na Makaazi ya Askari wa
Uhamiaji Mkoani humo.
Idara
ya Uhamiaji pamoja na juhudi hizo zinazolenga kuboresha utoaji wa Huduma zake
kwa Jamii na Wageni kutoka Mataifa mbali mbali duniani, imelipa kipaumbele
suala la kuboresha Makaazi ya Askari wake, Vitendea kazi sambmba na kuweka
mifumo ya kisasa ya kielektroniki ambayo imekuwa nyenzo kubwa katika utoaji wa
huduma unaozingatia viwango vya Kimataifa.
“Idara yetu imekuwa na hadhi kubwa katika
medani za Kimataifa, kwa kutumia mifumo ya teknolojia ya kisasa, tumeweza
kusimamia na kudhibiti Uingiaji, Ukaaji na Utokaji holela wa watu katika mipaka
yetu. Hii ni hatua ya kujivunia sana kwetu na kwa serikali zetu zote mbili”
alisema Kamishna Sururu.
Imetolewa
na: KITENGO CHA UHUSIANO, AFISI KUU YA
UHAMIAJI ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment