Habari za Punde

MMEWAZA waanza kugawana fedha za masomo


 NA HAJI NASSOR, PEMBA

MFUKO wa Maendeleo ya Elimu kwa Wanahabari Zanzibar ‘MMEWAZA ‘wenye makao makuu yake kisiwani Pemba, umeanza kutoa fedha za masomo kwa wanachama wake, baada ya kukusanya fedha hizo kwa kipindi cha miezi mitatu iliopita.

 Kwa hatua za awali wanachama watano wanaosoma kwenye vyuo mbali mbali, ambao waliwasilisha majina yao kwa uongozi wa Mfuko, ndio waliopatiwa fedha hizo kwa ajili ya kuongeza fedha za masomo.

Akizungumza kabla ya ugawaji wa fedha hizo, mweka hazina wa Mfuko huo Raya Ahmada, alisema kutokana na makusanyo kutofikia lengo walilokusudia, walilazimika kuweka kiwango cha shilingi 400,000 kwa kila mwanachama.

Alisema awali, walitarajia kufikia wanachama 50, ili wakusanye shilingi 1500,000 (milioni moja na laki tano) kwa mwezi, ambapo miezi mitatu baadae, wajikusanyie shilingi milioni 4. 5 ili kuwapatia shilingi milioni moja kwa wanachama wanne kila miezi mitatu, ingawa mipango yao ilikuwa tofauti.

Mwekahazina huyo, alisema kutokana na kukosa idadi kubwa ya wanachama kwa hatua za awali, ndio maana wakalazimika kukusanya shilingi 690,000 kila mwezi kwa idadi ya wanachama 23, kwa wastani wa shilingi 30,000 kwa mwanachama mmoja.

Hivyo alisema wametumia shilingi milioni 2, kwa kuwakabidhi wanachama watano shilingi 400,000 kila mmoja, ili kuendelea mbele na masomo.
“Leo (jana) tumeshawakabidhi wanachama wetu watano wa ‘MMEWAZA’ shilingi 400,000 kila mmoja, ambao hawa kwanza wako masomoni, na ndio walioleta majini yao mwanzo”,alifafanua.

Hata hivyo Mwekahazina huyo, alisema haina maana kuwa mwanachama ambae hasomi kuwa, hatofaidika na mchango, bali kwanza ni kuwapatia wale walioko vyuoni ili wapate utulivu wa masomo.

Katika hatua nyengine, Mwekahazina huyo wa ‘MMEWAZA’ aliwataka wale waliopatiwa fedha hizo, kuzitumia kwa lengo lililokusudiwa, ili kutimiza ndoto zao za kujisomea, pamoja na malengo ya Mfuko kama ulivyoanzishwa.

Mapema Katibu wa Mfuko huo Salmin Juma, alipongeza hatua ya ustahamilivu kwa wanachama hao, hadi kufikia kupatiwa fedha hizo kwa ajili ya kujisaidilia kimasomo.

Alisema, ipo mifuko kadhaa huanzishwa kwa lengo kama hilo, ingawa huwa hayafikii kugawana kutokana na kujitokeza kwa mambo tofauti, ingawa kwa ‘MMEWAZA kwa hatua za awali, umeanza vizuri.

“Ni jambo la faraja kuona mfuko umeanza kugawa mapato kwa wanachama husika, maana ipo mengi ambayo huanzishwa na kisha kuhesabu migogoro”,alifafanua.

Baadhi ya wanachama waliokabidhiwa fedha hizo na kutopenda majaina yao yatajwe, walisema wamefarajika kuona viongozi wamefikia malengo hayo.
Walisema, ni wakati mwafaka kwa ambao hawajiunga kuhakikisha ukimalizika mzunguruko wa kwanza, kujiunga ili wawe na uhakika wa kujipatia fedha zao, hasa kwa wale wanaosoma.


Mfuko wa Maendeleo na Elimu kwa Wanahabari Zanzibar ‘MMEWAZA’ ambao umeanzishwa mwezi Juni, mwaka huu unawanchama 23, ambao kila mwezi hukusanya shilingi laki 690,000 na lengo kuu, ni kuwasaidia fedha za ada wanachama wao ambao wengi ni waandishi wa habari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.