NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MOHAMED Bakar Mshindo (56) mkaazi wa
Kangagani Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, anatuhumiwa kumbaka mtoto wa
miaka tisa, huko katika nyumba anayoishi Kangagani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, wanafamilia wa
mtoto huyo, Mjini ole Wilaya ya Chake Chake, walisema kuwa, mzee huyo alikuwa
akimchukuwa mtoto wao skuli wakati wa mapunziko (rises), na kwenda naye
nyumbani kwake kimfanyia udhalilishaji.
Walisema kuwa, ni zaidi ya miezi miwili tokea kuripoti
tukio hilo kituo cha Polisi Mchangamdogo, ingawa hakuna hatua yoyote
iliyochukuliwa na kupelekea mtuhumiwa kupita mitaani na kujigamba kwamba yeye
ni mwenye pesa na hawezi kutiwa hatiani.
Akielezea tukio hilo mlezi wa mtoto huyo (60) alisema
kuwa, mtoto wake alitoka kwenda skuli na aliporudi akamuona hali yake sio ya
kuridhisha, ambapo alimuuliza kama anaumwa ampeleke hospitali.
“Aliniambia anaumwa na jipu na ndipo nilipomwambia
asiende skuli na nilimtafutia dawa ili ajipake, ingawa hali ilizidi na kuwa
mbaya na kutaka kumpeleka hospitali kwa siku ya pili”, alisema mlezi huyo.
Alieleza kuwa, siku ya pili kabla ya kupeleka hospitali
alikwenda mazikoni na kupewa taarifa na mwalimu wake wa darasa kwamba amekuwa
na matumizi makubwa, jambo ambalo lilimshitua na kuanza kumpeleleza kwani yeye
alikuwa akimpa si zaidi ya shilingi 200.
Kwa upande wake mama mdogo wa mtoto huyo (19) alieleza
kuwa, walipomgundua mtoto wao siku aliyokwenda pwani na watoto wenzake kuvua
kaure, ambapo hakuweza kuokota kutokana na maji chumvi kumuumiza sehemu
alizoathirika.
“Aliporudi pwani hali yake ilikuwa mbaya hata kwenda
alikuwa hawezi na ndipo tulipotumia nguvu kumuangalia, tukamuona kwamba tayari
ameshaathirika”, alisema mama huyo.
Alieleza kuwa, walimuuliza aliyemfanyia kitendo hicho na
kusema kuwa ni Muhamadi Bakar Mshindo mkaazi wa Kangagani, ambaye alikuwa
akimchukuwa skuli wakati wa mapumziko na kwendanae, katika nyumba anayoishi na
kumbaka.
Bibi wa mtoto huyo (40), alisema kuwa, baada ya kuwaeleza
hivyo walikwenda kituo cha Polisi Mchangamdogo, ingawa hadi leo haijachukuliwa
hatua yoyote ya kisheria kesi hiyo.
Nae mtoto (9) aliyefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa,
babu huyo alimfanyia kitendo hicho mara mbili na alikuwa akimfunga matambara ya
mdomo, pamoja na kumuwekea panga kwa kumtishia ili asiseme.
“Alikuwa akinipa chipsi, pesa na akija skuli kunita
wakati wa mapumziko (rises) mimi na mjukuu wake, lakini siku aliyonibaka
alinivuta ndani na akaziba matambara na baadae mjukuu wake alikimbia”, alisema
mtoto huyo.
Mratibu wa wanawake na watoto Shehia ya Kangagani Awena
Salim Kombo alieleza kuwa, kesi hiyo ipo kwa muda mrefu sasa na imeshafikishwa
kituo cha Polisi Mchangamdogo, ingawa hakuna chochote kilichoendelea zaidi ya
mtuhumiwa kupita mitaani na kujigamba.
Sheha wa shehia ya Mjiniole Khamis Shaaban Hamad alieleza
kuwa, pamoja na matukio ya udhalilishaji kutokea lakini wananchi wamehamasika
kuyaripoti kupitia elimu waliyopatiwa na mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na
kuwawezesha wanawake GEWE.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba
Haji Khamis Haji alisema kuwa, upelelezi wa kesi hiyo tayari umekamilika na
tayari jalada lishapelekwa kwa Mkurugenzi wa mashitaka.
Kamanda huyo alisema kuwa tukio hilo liliripotiwa Kituo
cha Polisi Mchanga mdogo Oktoba 13 mwaka huu, ingawa lilikaa mda mrefu kabla
halijaripotiwa na kuwataka wanajamii kuripoti kuharakisha kuripoti matukio
yanapotokea.
Jumla ya matukio manne yametokea ndani ya kipindi cha
miezi miwili katika shehia sita zilizopata elimu kupitia mradi wa GEWE, juu ya
kuviripoti vitendo vya udhalilishaji vinavyotokea katika jamii, ikiwemo
Kangagani, Mjiniole, Mchangamdogo, Kinyikani, Kiungoni na Shengejuu Wilaya ya
Wete.
No comments:
Post a Comment