Habari za Punde

KAMATI ya udhibiti na usimamizi wa ujenzi (DCU) Kusini Pemba

Na/HASINA KHAMIS--- PEMBA.

KAMATI ya udhibiti na usimamizi wa ujenzi (DCU) imezinduliwa rasmi katika  Mkoa wa Kusini Pemba, kwa  lengo la kudhibiti ujenzi wa kiholela pamoja na kuweza kulinda usalama wa majengo na kuboresha mji kuwa wenye kivutio.

Kamati hiyo ilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba,   Mwanajuma Majid Abdalla ,katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huyo Chake Chake Pemba.

Alisema hali ya mazingira Katika Mkoa wa Kusini   Pemba ni Milima, hivyo baadhi ya  Wananchi kukata milima ovyo na kusababisha mafuriko pamoja na maporomoko kwenye Milima.

“Zamani Pemba ni nadra kusikia milima kuporomoka au mafuriko lakini sasa baada ya kujenga bila kufuata sheria kumesababisha maafa, hivyo ninafarijika kwa kamati hii ya DCU kuzinduliwa na imani yangu itaweza kudhibiti hali hiyo “, alieleza.

Mkuu huyo wa Mkoa, alisema kumekuwa na tabia ya kujenga Wananchi kwa kutafuta kibali kwa Sheha ,Diwani na baada ya kupata huanza kujenga bila ya kufata taratibu nyengine za Baraza la mji .

Hivyo kusababisha maeneo ya kilimo kuweza kujengwa Nyumba za kuishi na kusababisha usumbufu kwa Serikali na Mabaraza ya mji.

Mwanajuma, aliahidi kushirikiana na kamati hiyo kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali ili kuona maendeleo ya Mji yanaonekana.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt, Muhammed Juma, alisema hali ya ujenzi kwa Zanzibar, imekuwa kwa kasi hivyo ni vyema kufuata taratibu zilizowekwa na DCU pamoja na kukata kibali cha ujenzi ili kuweza kuondoa usumbufu baada ya kujenga .

Alisema”kamati ya DCU, ina malengo ya kuweka miji ya Zanzibar na majengo yake kuwa imara na usalama wa hali ya juu,  mazingira ya kuvutia baadae, hivyo ni vyema kwa wananchi kufuata taratibu kwenye ujenzi”.

Mwenyekiti huyo, alisema ipo haja kwa Masheha na Madiwani kupewa elimu juu ya utoaji wa kibali kwani jamii inaona ikipata kibali kwa watu huo kuwa inatosha kwa kujenga bila ya kutaarifu Serikali za Mji.

Mipango Miji, imekuwa na nafasi kubwa ya kupambana na miji ili kuweza kuweka katika hali ya kuvutia na kuondoa migogoro ya ardhi kwa wananchi.
Muhammed Faki Machano, Mjumbe wa Sekreteriti ya Kamati alisema ni lazima kuondoa muhali pale panaposemwa kuwa sehemu haifai kujengwa kwani DCU inafata Sheria ya mipango miji na ipo kitaifa.

Hata hivyo alisema Serikali kuu na Serikali za mitaa zitafanya kazi pamoja kujenga Miji za Zanzibar  pamoja na kupeana  elimu na kutatua migogoro itakayo tokea ,ikiwa ni pamoja na mapato yatakayo kusanywa na kamati hiyo kulenga zaidi miradi ya Mabaraza na kubuni miradi ya maendeleo ya miji ambayo itaweza kuonekana moja kwa moja na Wananchi.
                                    


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.