Habari za Punde

Serikali yaendelea kugawa Makamusi ya Kiswahili fasaha Maskulini ,Wilaya ya Kati


Na Khadija Khamis–Maelezo  28/11/2017

Afisa Elimu Wilaya ya Kati Makame Steni Haji amewataka Walimu kuvitumia vitabu vya makamusi kwa kuwasomesha wanafunzi katika maskuli ili kwenda sambamba na lugha fasaha ya Kiswahili kama inavyotakiwa kutumika katika jamii.

Akiyasema hayo huko katika ukumbi wa Kituo cha Mafunzo ya Walimu Wilaya ya Kati  Dunga  wakati alipokuwa akigawa makamusi kwa walimu wa skuli mbali mbali za wilaya hiyo .

  Alisema kamusi la kiswahili fasaha ni muongozo wa lugha ya Kiswahili katika nyaja tofauti za lugha ya Kiswahili kuandika kutamka na kuzungumza kitu ambacho humfuza mwanafunzi  na kumpa muongozo wa lugha hiyo kama inavyohitajika kutumiwa

“Makamusi yatatusaidia katika shughuli za ufundishaji  wanafunzi kwa kuweza kuwapa  uwelewa wa lugha katika kukuza msamiati pamoja na kupata marejeo ya lugha hiyo ili kupata usahihi wa maneno.”alisema Afisa huyo 
.
Aidha alisema  makamusi yatumike kwa kuwasaidia wanafunzi na walimu kuweza  kujifunza mambo mbali mbali isiwe yanawekwa makabatini kuingia fumbi jambo ambalo sio lengo lililokusudiwa .

Afisa huyo alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt  Ali Mohamed Shein kwa jitihada yake ya kujali maendeleo ya nyanja mbali mbali ikiwemo sekta ya elimu.

Aliwataka walimu kuyatunza  kuyasimamia  na kuyasoma  makamusi hayo ili kuweza kuwapa upeo na uwelewa wanafunzi kwa kuijua lugha hii kiufasaha na kuweza kudumu kwa muda mrefu .

Hata hivyo Afisa huyo alitoa shukrani kwa wale wote walioweza kuwasaidia hadi kufanikisha kupata makamusi hayo na kuiomba Serikali na Wadau mbali mbali wenye uwezo kwa kuwasaidia vifaa vya masomo ya sayansi ili kuweza kufanikisha kuwapatia wanafunzi elimu iliyo bora .
Nae katibu Mtendaji wa baraza la Kiswahili (BAKIZA) Mwanahija Ali Juma alisema  lengo la  makamusi haya ni kuwahamasisha wanafunzi, walimu pamoja na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu ambayo ndio njia sahihi ya kuifahamu, kuitumia na kuiendeleza lugha ya Kiswahili fasaha  na utamaduni wake.

“Makamusi haya yaliandikwa kuanzia mwaka 2003 hadi 2010 ikiwa ni muda wa miaka  saba na waliyoyaandika hawakupoteza bali historia itabakia na itawakumbuka kwa namna wanavyoisaidia jamii ya Wazanzibari,” aliongeza Katibu huyo .

Alieleza kuwa Kiswahili ni nyenzo muhimu inayohifadhi utamaduni kupitia msamiati, hivyo iko haja ya kukienzi, kukitunza na kukifahamu kwa ufasaha.

Aidha alisema makamusi  885 yenye thamani ya shilingi milioni 15,450,000 yametolewa na serikali kwa  skuli zote ili kuwawezesha wanafunzi kupata msingi muhimu wa kujifunza lugha ya Kiswahili.

Skuli za sekondari zilizonufaika na mgao huo katika skuli za sekondari za wilaya ya kati  ni Skuli ya Sekondari Mpapa,Mwera, Uroa,Jendele,Jumbi, Chwaka Kibele Uzi, Skuli ya sekondari ya Umoja Uzini,  Kikungwi Marumbi na nyenginezo

Kwa upande wa Skuli za Msingi, Wilaya ya kati ni Skuli ya Msingi Bungi,Jendele Dunga,Jumbi,  Koani, Mseweni, Ndijani, Cheju, Gana Kidimni na nyenginezo.

Nae Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Uzi Abdalla Ali Haji alisema nia ya Serikali ni nzuri ya kuweza kuwapatia makamusi hayo ambayo yatawasaidia kuwapatia uwelewa  kwa walimu na wanafunzi kuifahamu lugha ya Kiswahili fasaha na kuahidi watayatunza  watayahifadhi pamoja na kuyafanyia kazi ipasavyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.