Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seid Akutuna na Balozi wa China Nchini Tanzania Ofisini Kwake Vuga Zanzibar.

Balozi wa China Nchini Tanzania Bibi Wang Ke akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha Rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mabalozi wa China Nchini Tanzania na yule aliyepo Zanzibar.Wa kwanza kutoka Kushoto ni Balozi wa China Nchini Tanzania Bibi Wang Ken na wa kwanza kutoka Kulia ni Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiuowu.
Balozi Seif akiagana na Ujumbe wa Kidiplomasia wa Ubalozi wa China Nchini Tanzania na Ule wa Zanzibar mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akiagana na Balozi wa Tanzania Nchini Misri Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor aliyekaa upande wa Kulia yake na Balozi Abdulrahman Kaniki aliyekaa upande wa Kushoto walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika nyadhifa hizo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan Kolimba Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa Zanzibar na Ujumbe wake kufuatilia rasimu ya Utawala Bora  Afrika kwa Wizara za SMZ.

Balozi Seif akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhan Muombwa Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kati kati yao ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan Kolimba.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan Kolimba kutoka Kushoto akimfafanulia jambo Balozi Seif wakati ujumbe aliouongoza wa Wizara yake ukiwa Zanzibar kufuatilia rasimu itakayozaa Ripoti ya  Utawala Bora  Afrika kwa Wizara za SMZ.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na. othman Khamis OMPR.
Balozi wa China Nchini Tanzania  Bibi Wang  Ke  alisema kukamilika kwa utanuzi wa ujenzi wa  Eneo la Maegesho ya Ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar  utatoa fursa ya kuongezeka kwa huduma za usafiri  wa anga baina ya Zanzibar na Mataifa mengine Duniani.


Alisema matayarisho ya ujenzi huo katika hatua za awali za Awamu ya Pili  aliyoyashuhudia baada ya kushuka kwenye Uwanja huo wa Ndege wa Zanzibar yamempa faraja yeye pamoja na Uongozi mzima wa Benki ya Kimataifa ya Exim ya Nchini China iliyoridhia kugharamia Mkopo wa ujenzi huo.

Balozi  Wang  Ke alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Kidiplomasia.

Alisema Zanzibar inaweza kurejesha  Heshima yake ya kuwa Kituo cha Kibiashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki  chenye uwezo wa kutoa huduma za Kibiashara kupitia mfumo wa kisasa wa Mawasiliano kupitia usafiri wa anga badala ya ule uliozoeleka wa  Baharini.

Alieleza kwamba zaidi ya Watalii  70,000 kutoka  Nchini Jamuhuri ya Watu wa China wanaweza kuitembelea Zanzibar kila Mwaka kupitia usafiri wa anga na hata ule wa Baharini iwapo yataandaliwa mazingira mazuri katika Sekta ya Utalii baada ya kuongezeka kwa huduma za Mawasiliano ya usafiri.

Bibi Wang Ke aliyeanza majukumu yake Nchini Tanzania Mwezi Mmoja sasa  aliahidi kwamba  Nchi yake iliyopiga hatua kubwa Kiuchumi ndani ya kipindi cha Miaka 30 itaendelea kuiunga mkiono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuona maendeleo ya Kiuchumi yanakua na kushirikisha wananchi wote siku hadi siku.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza faraja yake katika kuona Viongozi wote waliiopo hivi  sasa kati ya China na Tanzania bado wanaheshimu ushirikiano wa Mataifa hayo mawili ulioasisiwa na waanzilishi wake Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na Hayati Mao Tse Tung.

Balozi Seif  alisema  mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na China kupitia Makampuni na Mashirikia yake mbali mbali umeiwezesha Tanzania kukuwa Kiuchumi na kustawisha Jamii mambo yanayokwenda sambamba na kupungua kwa kasi ya ukali wa Maisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza na kumuomba Balozi huyo wa China Nchini Tanzania kwamba Zanzibar  bado inaendelea kuhitaji Wawekezaji pamoja na Watalii kutoka Nchini China katika azma yake ya kuimarisha uchumi hasa kwenye Sekta ya Utalii.

Balozi Seif  ameishukuru Serikali ya China kwa misaada yake mikubwa  inayotowa na kumuhakikishia kwamba uhusiano wa Kihitoria uliopo wa Mataifa hayo rafiki utaendelea kudumu kila Mwaka.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Mabalozi Wapya Wawili wa Tanzania Nchini Misri na Zambia walioteuliwa hivi karibu na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.

Mabalozi hao ni Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor anayeiwakilisha Tanzania Nchini Misri na Balozi Abdulrahman Kaniki anayekwenda  Nchi jirani ya  Kusini mwa Tanzania ya Zambia.

Katika mazungumzo yao Balozi Seif  aliwakumbusha Mabalozi hao kuzingatia zaidi  suala ya Doplomasia ya Kiuchumi ambalo  kwa sasa limechukuwa nafasi ya pekee  tofauti na lile ya Kisiasa lililozoeleka katika mabadiliko ya Kiuchumi yaliyopo Ulimwenguni.

Alisema matunda  makubwa ya uwakilishi wa Mabalozi hao yataonekana katika kasi ya ongezeko la Miradi ya Uwekezaji kutoka katika Mataifa wanayokwenda  kufanya kazi.

Mapema Balozi wa Tanzania Nchini Misri  Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor kwa niaba  ya Mwenzake Balozi Abdulrahman Kaniki anayekwenda Nchini  Zambia alisema wanaahidi kuitanga Tanzania katika Mataifa hayo rafiki yenye Uhusiano wa muda mrefu.

Meja Jenerali Nassor aliziomba Taasisi zinazozimamia Sekta ya Utalii Nchini kuwa wazi kwa masuala yanayohitajika katika kuimarisha Sekta hiyo kupitia Wawekezaji na Mikataba ya uanzishwaji wa Miradi ya Hoteli.

Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Naibu Waziri wake Dr. Suzan Kolimba.

Katika mazungumzo hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan alisema  wako Zanzibar kufuatilia Rasimu ya Matayarisho ya Ripoti ya Utawala Bora  Barani Afrika kwa upande wa Zanzibar inayotakiwa kutayarishwa na Wizara zilizo chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dr. Suzan alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba  Ripoti ya Utawala Bora  Barani Afrika itakuwa ndio Mpango Kazi kwa Maraisi wa  Mataifa ya Bara la Afrika watakayoiwakilisha katika  Kikao cha Umoja wa Afrika {AU} kinachotarajiwa kufanyika Mwezi Febuari mwaka 2018.

Alisema hatua ya awali ya matayarisho ya Ripoti hiyo imeonyesha  mafanikio kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa kuwa  mfano bora wa Rasimu yake ya Utawala Bora  kiasi cha Wataalamu wa masuala ya Kisiasa  wa Bara la Afrika kushauri iwe kigezo cha kuigwa na Mataifa mengine Barani Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.