Habari za Punde

Balozi Seif afungua Mkutano Mkuu wa kuwachagua Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kaskazini Unguja

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Zanzibar  Mzee Ali Ameif Mohamed kabla ya kuufungua Mkutano wa Uchaguzi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Hapo Mahonda.
 Balozi Seif akiufungua Mkutano  Mkuu wa Uchaguzi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja uliofanyika Hapo Mahonda.
 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano  Mkuu wa Uchaguzi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wakifuatilia utaratibu wa Kikao chao cha kuwachagua Viongozi wao watakaowatumikia katika Kipindi cha Miaka Mitano ijayo
Balozi Seif  akiwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kaskazini Unguja akipiga kura kuwachagua Viongozi watakao uongoza Mkoa huo kwa kipindi cha Miaka Mitano ijayo.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Wanachama wanaochaguliwa katika nyadhifa tofauti ndani ya Chama hicho wanalazimika kufanya kazi muda wote ili kurahisisha utatuaji wa kero zinazowakabili Wanachama pamoja na Wananchi wanao wasimamia.

Alisema utendaji wao lazima uoane na kazi nzuri inayoendelea kufanywa  na Chama hicho chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi  Taifa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John  Pombe Magufuli.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa kuwachagua Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kaskazini Unguja uliofanyika kwenye Ofisi Kuu ya Mkoa huo iliyopo  Mahonda  Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alieleza kuwa Viongozi wanaopaswa kuchaguliwa  ndani ya Chama katika kipindi hichi cha mabadiliko ya kiutendaji ni wale wenye ubora wa kiutendaji watakaokuwa na uwezo sambamba na uzalendo wa kutumikia Sera na Ilani ya CCM.

“ Wanaoteuliwa au kuchaguliwa kupitia Mikutano tofauti ndani ya Chama  waelewe kwamba wana kazi ya kusimamia kazi zote za Chama cha Mapinduzi ndani ya Mikoa yao ”. Alisema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.

Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba wakati wa kuwa na Viongozi ndumi lakuwili kwa maana ya sura mbili kwa nyakati tofauti umekwisha na wala haufai tena kutegemea na kasi ya utendaji wa chama ulivyo hivi sasa.

Alisema nguvu za Chama cha Mapinduzi kufuatia chaguzi zake za ndani tayari zimeshaashiria ushindi mnono kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka 2020 na hata kwenye majimbo yanayoongozwa  na vyama vya upinzani Nchini.

Balozi Seif alieleza kwamba upinzani ndani ya ardhi ya Tanzania  hivi sasa hauna Hoja wala agenda  kutokana na matukio madogo madogo ya chaguzi ngazi ya Kata zilizofanyika hivi karibuni kwa upande wa Tanzania Bara ambapo CCM imeibuka kidedea kwa kushinda kwa asilimia kubwa.

Alisisitiza umuhimu wa kuepukwa mifarakano ndani ya chama  na kudumishwa kwa Umoja na Mshikamano utakaokuwa ngazi ya msingi ya Chama hicho ya kuongeza nguvu za kuelekea kuwa muhimili wa kusimamia Amani  na usalama Nchini Tanzania.

Akizungumzia miradi ya Chama Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Viongozi waliopewa kijiti cha kusimamia utendaji wa Chama hicho kuwa wabunifu wa miradi ya kuendesha Chama hicho.

Alisema ubunifu huo kwa kiasi Fulani utasaidia  kuondokana na dhana ya kuomba omba kwa vile Chama chenyewe  hivi sasa kina upungufu wa nguvu katika kujitegemea kiutendaji.

Balozi Seif alitolea Mfano Mkoa wa Kaskazini Unguja umebahatika kuwa na miradi mingi ya uchumi  inayoweza  kuendesha  chama, lakini tatizo liliopo ni usimamizi mzuri wa Miradi hiyo.

“ Wakati huu tunamalizia chaguzi zetu za ndani kupanga safu ya Ushindi kwa ajili ya mwaka 2020 tunapaswa kujipanga kwa kubuni Miradi ya Kiuchumi ndani ya kipindi cha  mwaka 2017 hadi 2020 ili iendeshe chama bila ya kutetereka ”. Alisema Balozi Seif .

Alifahamisha kwamba si vyema mzigo wa matatizo wakabebeshwa Waheshimiwa Wabunge wa Wawakilishi ambao tayari wamekabidhiwa majukumu yao wanayopaswa kuyatekeleza ya kuwahudumia Wananchi katika Majimbo yao.

Balozi Seif  alikemea kwamba Chama hakitosita kumchukulia hatua za nidhamu Kiongozi au mwanachama ye yote atakayeamua kula fedha za miradi ya Chama na kuishia mifukoni mwake.

Alisema ubadhirifu katika kipindi hichi cha ukweli na uwazi ndani ya Chama cha Mapinduzi haukubaliki na lazima upigwe vita kwa nguvu zote.

Mapema  katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Mula Othman  Zubeir  alisema chaguzi zote zimeshakamilika kuanzia Mashina 21, Matawi 102, Wadi 18 na kumalizia Wilaya Mbili zilizomo ndani ya Mkoa huo.

Nd. Mula aliwapongeza Viongozi na Wanachama wa Mkoa huo kwa kuhakikisha kwamba chaguzi zote zimeendeshwa katika misingi ya Amani, Haki na taratibu zilizowekwa ndani ya Katiba, Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza Muda wake wa Mkoa wa Kaskazini Nguja Nd. Haji Juma Haji aliwashukuru Viongozi na Wanachama wote wa CCM wa Mkoa huo waliomuwezesha kutekeleza majukumu yake katika kipindi chake cha Uongozi.

Nd. Haji alisema ushirikiano wa pande hizo ndio ulioleta mafanikio makubwa na kuwataka Viongozi wapya kuiga mfano huo kwa nia ya kujenga safu ya ushindi kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.