Habari za Punde

Kongamano la kimataifa la kwanza la Kiswahili kufanyika Zanzibar

MWENYEKITI wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dk. Mohammed Seif Khatib, akizungumza na waandishi wa habari katika jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Kikwajuni, kuelekea kufanyika kwa kongamano la kimataifa la lugha ya Kiswahili linaloandaliwa na BAKIZA. (Picha na Kijakazi Abdalla- MAELEZO).

Na Khadija Khamis                      Maelezo               

BARAZA  la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA ) linatarajia kufanya Kongamano la kimataifa la kwanza la Kiswahili Zanzibar na kuhudhuriwa na Wataalamu mbalimbali wa Kiswahili kutoka nchi tofauti Duniani.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti  wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA )Dkt.  Mohamed Seif Khatib alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu Kongamano hilo katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Kikwajuni mjini Zanzibar.

 Alisema  Kongamano hilo la kimataifa linatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku mbili kati ya Disemba 19 na 20 mwaka huu katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani,Kikwajuni mjini Zanzibar.

Dkt. Seif alisema  lengo la kongamano hilo ni kuiendeleza lugha ya kiswahili ili itumike kwa ufasaha na usahihi pamoja na kuinua  vipaji  mbali mbali vya kuitumia lugha hiyo ikiwemo utungaji, usomaji na uzungumzaji fasaha wa lugha ya Kiswahili.

“Lengo lubwa ni kuibuwa Vipawa na vipaji  vya vijana wetu wawe  waandishi bora wa Riwaya, Mashairi ,utungaji wa tamthilia,  hadithi pamoja na Waandishi wa habari ili waweze  kuitumia kwa kuandika na kuizungumza sambamba na kutafsiri nyaraka za serikali na za watu binafsi“alisema Dkt  Seif.

Aidha alisema kuwa Kiswahili kimekuwa mali ya dunia nzima kutokana na kutumika kwa lugha hii katika sehemu mbali mbali duniani jambo ambalo limechangia kukitukuza na kwa kutumika katika vyombo vya habari vya nje ikiwemo Idha ya Kiswahili ya BBC

“Zanzibar kiswahili ndio kwao kwa sababu  mnamo mwaka 1930 chombo cha kuendesha Kiswahili kiliamua Kiswahili cha unguja mjini kiwe ndio  lugha rasmi ya kutumika  serikali za afrika mashariki na kuamua pia Zanzibar iwe ni makao makuu ya kamisheni ya Kiswahili sahihi na sanifu chini ya mwamvuli wa afrika mashariki “alifahamisha Dkt Seif .

Dkt Seif alifahamisha kuwa chimbuko la Kiswahili sanifu ni Unguja Mjini na kutoa rai kwa watu kuitumia ipasavyo bila ya kuipotosha heshima hiyo.

Amesema kuwa Makala zaidi 100 zinatarajiwa kuchambuliwa na wageni watakaoshiriki Kongamano hilo la Kiswahili ambapo Washiriki watatoka katika nchi tofauti ikiwemo Kenya, Misri ,Burundi, Ghana, Marekani, Ujerumani na Uengereza.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Mwanahija Ali Juma alisema maandalizi ya Kongamano hilo yanaendelea ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt Ali Mohamed Shein.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.