Habari za Punde

KAMATI YA RAIS YA KUCHUNGUZA BIASHARA YA MADINI YA TANZANITE YAANZA MAZUNGUMZO NA KAMPUNI YA TANZANITE ONE

Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi   akisalimiana  jijini Dar es salaam leo Januari 17, 2018   na wawakilishi wa kampuni ya Tanzanite One kabla ya kuanza na mazungumzo ambayo yanalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na rasilimali ya madini hayo ambayo yanachimbwa nchini Tanzania pekee. Picha na IKULU

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Description: Description: Description: Description: Description: Description: Coat of ArmsKURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz              

Faksi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
      IKULU,
 1 BARABARA YA BARACK OBAMA,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite imeanza kufanya mazungumzo na kampuni ya Tanzanite One.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema mazungumzo hayo yaliyoanza tarehe 16 Januari, 2018 yanalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na rasilimali ya madini hayo ambayo yanachimbwa nchini Tanzania pekee.
Prof. Kabudi amesema mazungumzo yameanza vizuri ambapo pande hizo mbili zinapitia matatizo yote yanayohusu biashara ya madini ya Tanzanite, utekelezaji wa sheria na kanuni mbalimbali za madini na mapato ya rasilimali hiyo, ili hatimaye zikubaliane namna bora itakayohakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzanite One Bw. Faisal Juma Shahbhai amesema Tanzanite One ipo tayari kwa majadiliano hayo na inaunga mkono juhudi za kuhakikisha madini hayo yanainufaisha Tanzania tofauti na ilivyo sasa ambapo yanazinufaisha zaidi nchi nyingine ambazo hazizalishi Tanzanite.
Bw. Shahbhai ameongeza kuwa Tanzanite One itatoa taarifa zote zinazohitajika na wakati wote itatoa ushirikiano wenye lengo la kufanikisha mazungumzo hayo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
17 Januari, 2018


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.