Habari za Punde

Rais Dk Shein atoa salamu za mwaka mpya 2018


 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                    31.12.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato zimeiwezesha Serikali anayoiongoza kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ya kupandisha mishahara ya kima cha chini kwa asilimia mia kutoka TZS 150,000 mpaka TZS 300,00 kwa mwezi kwa watumishi wa Serikali.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2018 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kuongeza pesheni kwa wastaafu na kuendelea kutoa fedha za Pensheni ya Jamii kwa wazee wote wanaostahiki.

Alieleza kuwa tangu mwezi April, 2017 walengwa wa nyongeza hizo wamekuwa wakifaidika na neema hiyo ambapo pia, katika mwaka 2017 Serikali imezidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi wanaopata mshahara wa kima cha chini jambo ambalo ni faraja kuona waajiri wengi katika sekta hiyo wameshaitikia wito licha ya kuwepo baadhi waliotaka kurejesha nyuma juhudi hizo za serikali.

Aliongeza kuwa uchumi wa Zanzibar unaendelea kuimarika na katika robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2017 (Januari-Machi), kasi ya ukuaji uchumi ilifikia asilimia 6.3 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 5.2 kwa kipindi kama hicho cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2016 ambapo katika kipindi cha robo mwaka ya pili (Aprili-Juni) kwa mwaka 2017 ukuaji wa uchumi nao uliimarika na kufikia asilimia 8.2.

Hivyo, Dk. Shein alieleza kuwa ni jukumu la kila mmoja katika mwaka huu mpya wa 2018 la kuongeza juhudi ili kuhakikisha kuwa yanaendelea kutekelezwa vizuri malengo hayo yaliobainishwa kwenye MKUZA III na mipango mengine ya maendeleo.

Dk. Shein aliendelea kutoa pongezi kwa wananchi wa Mikoa yote ya Zanzibar kwa juhudi zao kwa maendeleo ya kutia moyo yaliyopatikana katika sekta mbali mbali za maendeleo kwenye ziara za Mikoa aliyofanya Unguja na Pemba zikiwemo sekta za kiuchumi na kijamii ikiwa ni katika kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA 111 na Malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa  katika ujenzi wa miundombinu mbali mbali katika sekta ya afya na hivi sasa juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuimarisha huduma pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa vya utibabu katika hospitali na vituo vya afya.

Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha uliomalizika 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya TZS 7.0 bilioni kwa ununuzi wa dawa na vifaa vya utibabu, sawa na ongezeko la asilimia 42.9 ikilinganishwa na kiwango kilichotengwa kwa mwaka 2016/2017.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Dk. Shein alisema kuwa ikiwa tayari serikali imeshaanza ujenzi wa mradi wa skuli 9 za ghorofa katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba, ili kuimarisha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi hapa nchini ambapo ujenzi wa skuli hizo utagharimu jumla ya TZS 24.4 bilioni ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa OPEC dhamira ikiwa ni kumaliza ujenzi wa skuli hizo ifikapo Januari mwaka 2019.

Dk. Shein alieleza kuwa katika sherehe za Elimu bila ya malipo zilizofanyika tarehe 23 Septemba, 2017 alitangaza rasmi kuondoa michango katika elimu ya Sekondari kuanzia mwezi wa Julai, 2018 hatua iliyolenga kuendeleza utoaji wa elimu bila ya malipo kwa skuli zote za msingi na sekondari kwa watoto wote kwa misingi ile ile iliyoanzishwa na waasisi wa nchi hii.

Alieleza kuwa mwaka 2017 unamalizika ikiwa tayari kazi ya kulishuhulikia tatizo la kupoteza fedha za mishahara kwa wafanyakazi wanaochukua likizo bila ya malipo, wanaotoroka kazini, wanaolipwa kinyume na utaratibu (hewa), ambapo taarifa rasmin itatolewa na Serikali muda mfupi ujao.

Aliongeza kuwa katika mwaka 2018, Serikali inaendeleza utafiti wa mafuta na gesi kwa kutegemea taarifa itakayotolewa na wataalamu na kutoa wito kwa wananchi kuwa watulivu na Serikali itatoa taarifa rasmi ya matokeo ya utafiti huo unaofanywa kwa maslahi ya Zanzibar.

Aliwataka wananchi kutosikiliza maneno ya mitaani na kwenye mitandao wakati serikali yao ipo na kuwataka kuendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuiendeleza sekta yua Mafuta na Gesi Asilia.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Mpango Maalum wa Kulifufua Zao la Karafuu ulioanzishwa mara tu baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kuingia madarakani mwaka 2010 kwa kupanda mikarafuu mipya limeanza kutoa matokeo mazuri.

Alisema kuwa hadi tarehe 20 Disemba, 2017 wakulima wa karafuu walikuwa wameshauza karafuu ZSTC zenye thamani ya TZS 108.8 bilioni ambapo  kiwango hicho cha fedha kimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mzunguko wa fedha na kukuza sekta nyengine za kiuchumi.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote wanaendelea kuwakumbuka wakati wote wanajeshi 15 wa Jeshi la Wanachi wa Tanzania waliofariki huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako walikuwa katika shughuli za kusimamia amani chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupanga na kutekeleza mikakati mbali mbali ya kulinda na kudumisha amani nchini, Barani Afrika na duniani kote kwa jumla.

Dk. Shein pia, aliwasisitiza wananchi wakati wakiupokea mwaka mpya wa 2018, kila mmoja aweke dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuongeza jitihada za kuongeza kipato na kupambana na umasikini.

Aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuimarisha utawala bora, kukuza uadilifu na uwajibikaji na kusimama imara kwa vitendo katika mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu wa uchumi na dawa za kulevya, sambamba na kujidhatiti katika kuvitokomeza vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kuanza kusherehekea mwaka mpya 2018 kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 2018 pamoja na kushiriki katika ufunguzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi mbali mbali ya maendeleo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.