Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Mtukufu
Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu
Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya (UAE)wakiwa katika ukumbi wa makadhi
ya Kiongozi huyo Nchini Abu Dhabi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh Mohammed
bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu
wa Vikosi vya Ulinzi wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo viongozi
hao wamekubaliana kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo hasa
katika sekta za maendeleo zikiwemo za kijamii na kiuchumi.
Viongozi hao walifanya
mazungumzo hayo katika ukumbi wa Makaazi ya Sheikh Mohammed bin Zayed Al
Nahyan, mjini Abu Dhabi, mazungumzo yaliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa
ngazi za juu wa Abu Dhabi wakiwemo Mawaziri, Spika wa Abudhabi pamoja na
viongozi wengine wa ukoo wa Sheikh ZaUAE pamoja na wageni waalikwa.
Katika mazungumzo hayo viongozi
hao walikubaliana kwa pamoja kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kidugu na
kihistoria uliopo kwa muda wa miaka 44 hivi sasa hatua ambayo imeleta manufaa
makubwa kwa pande zote mbili.
Sheikh Mohammed bin
Zayed Al Nahyan, kwa upande wake alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Abu Dhabi
itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na iko tayari kutoa ushirikiano wake katika
kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo za kiuchumi na kijamii.
Aidha, Sheikh Mohammed, alieleza
kuwa Abu Dhabi inathamini sana uhusiano na ushirikiano huo na iko tayari kuunga
mkono vipaumbele vyote vilivyowekwa na Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali
mbali ya maendeleo.
Pamoja na hayo, Kiongozi
huyo alimpongeza Dk. Shein kutokana na juhudi zake za kuendelea kuiongoza vyema
Zanzibar na kusisitiza kuwa kutokana na juhudi hizo kuna kila sababu za yeye
kumuunga mkono ili wananchi wa Zanzibar wazidi kupata maendeleo endelevu.
Aidha, Sheikh Mohammed
bin Zayed Al Nahyan alimuhakikishia Dk. Shein kuwa uongozi wa Taifa hiyo unaona
fahari kuwa na mashirikiano na uhusiano na ndugu zao Zanzibar na kueleza kuwa
Abu Dhabi itahakikisha inaukuza na kuuendeleza uhusiano na ushirikiano huo
ambao anaamini utakuwa na tija kubwa kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake Dk.
Shein, alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukurani Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, kwa
mualiko wake aliompa nchini humo pamoja na mapokezi makubwa aliyoyapata yeye na
ujumbe wake na kueleza kuwa ziara hiyo ni kichocheo kikubwa cha mashirikiano
kati ya Zanzibar na Abu Dhabi.
Dk. Shein, alimuhakikishia
Sheikh Mohammed kuwa Zanzibar imepata matumaini makubwa kutokana na hatua za
kiongozi huyo za kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar ili izidi kupata
manufaa katika sekta zake za maendeleo zikiwemo za kiuchumi na kijamii.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa ziara hiyo ni kielelezo cha urafiki, heshima na udugu baina
ya Tanzania ikiwemo Zanzibar na Abu Dhabi pamoja na wananchi wake wote ambapo
pia, itasaidia sana kukuza uhusiano na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano.
Dk. Shein alieleza kuwa
Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Abu
Dhabi hasa
ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika sekta zote za kiuchumi,
kijamii na nyenginezo.
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein
alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Abu Dhabi
katika ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya “Jumeirah Etihad Towers” mjini Abu
Dhabi ambapo katika mazungumzo hayo Mkurugenzi huyo alimueleza Dk. Shein azma
ya Mfuko huo katika kuiunga mkono Zanzibar.
Katika maelezo yake,
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Mfuko huo uko tayari kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo
miundombinu pamoja na miradi mengine ya kijamii na kiuchumi.
Nae Dk. Shein kwa upande
wake aliupongeza Mfuko huo kwa kuonesha kuwa tayari kuiunga mkono Zanzibar katika
kuendeleza miradi yake ya maendeleo huku akieleza historia ya Mfuko huo katika
kuiunga mkono Zanzibar.
Mapema Dk. Shein akiwa
na ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein, alitembelea Mji mpya wa kisasa wa
Masdar unaoendelea kujengwa kwa dhamira ya kuufanya kuwa ni mji wa kipekee
duniani unaotumia nishati mbadala hasa umeme wa jua katika shuhuli zake zote
zinazohitaji nishati.
Akiwa katika mji huo
ulioko umbali wa kilomita 17 kutoka mjini Abu Dhabi, Dk. Shein alipata maelezo
kutoka kwa uongozi wa Mradi huo Mkurugenzi Mkuu Yousef Baselaib na Meneja
Msaidizi wa Mradi huo Fatma Al Shaigy walimueleza dhamira ya ujenzi huo ikiwa
ni pamoja na kuendeleza miji inayoweka uhifadhi wa mazingira kwa kutumia
nishati mbadala duniani na kumtajia nchi ambazo tayari zimeanza kufaidika na
teknolojia hiyo kupitia taasisi yao.
Pia, alitembelea Msikiti
Mkuu wa Abudhabi ambao unajulikana kwa jina maarufu la “Sheikh Zayed Grand
Mosque” na kusali sala ya Adhuhuri, ambapo Dk. Shein akiwa katika msikiti huo
alidhuru kaburi la Baba wa Taifa hilo na muwasisi wa Muungano wa nchi za Umoja
wa Falme za Kiarabu (UAE) Marehemu Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan, na
kumuombea dua.
Kwa mujibu wa maelezo ya
uongozi wa msikiti huo, ulieleza kuwa msikiti huo uloianza kujengwa mnamo mwaka
1996 hadi 2007 msingi wake uliwekwa na Marehemu Sheikh Zayed akiwa na lengo la
kuanzisha sehemu maalum ambayo itakuwa kiungo cha kuwaunganisha Waislamu wa
Madhehebu mbali mbali duniani, ambapo msikiti huo una uwezo wa kusali watu
40,000 kwa wakati mmoja.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment