Habari za Punde

Sakata la kusafirisha vipande vya madini ya dhahabu: Naushad ahukumiwa jela miaka mitano au faini Mil 6

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela  au kulipa faini ya  Sh 6 milioni, wafanyabiashara wawili, Naushad Mohammed Suleiman (63) na Ali Makame Juma (36) baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha vipande saba vya madini ya dhahabu  vyenye thamani ya Sh 989.7 milioni bila kuwa na leseni. 

Pia, mahakama hiyo imetaifisha dhahabu yote iliyokamatwa pamoja na mabegi mawili ya fedha mbalimbali kutoka nchi 15 duniani, walizokamatwa nazo, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume uliopo Zanzibar. 

Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi, Januari 11 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yanayowakabili. 

Wafanyabiashara hao maarufu  ambao ni wakazi wa Zanzibar, walikuwa wanakabiliwa na makosa mawili, ambayo ni kula njama na kusafirisha madini nje ya nchi kinyume cha sheria na bila kuwa na leseni kutoka mamlaka husika. 

Washtakiwa wanadaiwa kukamatwa Novemba 29, 2017, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume, wakisafirisha madini hayo kwenda Dubai katika Falme za Kiarabu. 

Washtakiwa hao hawajalipa faini na bado wapo katika mahakamani Kisutu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.