Habari za Punde

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Azungumza na Waandishi wa Habari Matayarisho ya Mkutano wa Baraza Kuanza Jumatano Wiki Hii.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na kuanza kwa Mkutano wa tisa wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (Picha na Kijakazi Abdalla Maelezo)
Na Kijakazi Abdalla - Maelezo  Zanzibar  5/02/2018
Mkutano wa tisa wa baraza la tisa la wawakilishi unatarajiwa kuanza siku ya Jumatano ya tarehe 7 Febuari 2018 .
Akizungumza na Waandishi wa habari huko ukumbi wa  Baraza la Wawakilishi Chukwani Mjini Unguja  Katibu wa Baraza la wawakilishi Raya Issa Msellem amesema kuwa jumla ya maswali 74 yanatarajiwa kujibiwa kwenye mkutano huo.
Amesema kuwa mbali na maswali hayo pia katika mkutano huo kutasomwa  miswada ya sheria iliyowasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Disemaba 2017 na itasomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa katika mkutano huo.
Aidha alisema kuwa miswada hiyo ni pamoja na Mswada wa sheria ya kufuta sheria ya kusimamia mwenendo wa biashara na kumlinda mtumiaji ya Zanzibar Nam 2 ya mwaka 1995 na kutunga sheria mpya ya ushindani halali wa biashara na kumlinda mtumiaji,kuweka masharti bora zaidi pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Pia alisema kuwa kutakuwa na mswada wa sheria ya kufuta sheria ya adhabu na kutunga sheria mpya ya adhabu,kuweka masharti bora zaidi pamoja na mambo mengine yanayohisiana na hayo.
Aidha alisema kuwa mswada wa sheria ya kufuta sheria ya mwenendo wa jinai Nam.7 ya mwaka 2004 na kutunga sheria mpya ya mwenendo wa jinai na kuweka utaratibu bora  upelelezi wa makosa ya jinai na usikilizaji wa kesi za jinai na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Sambamba na hayo pia alisema kuwa kutakuwa na ripoti za kamati za kudumu za baraza la Wawakilishi kwa mwaka 2017/2018, na taarifa ya Wabunge watano (5) wanaoliwakilisha Baraza katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano.
Pia kutakuwepo na Ripoti ya Serikali kuhusu hoja binafsi ya Mjumbe kuhusu kuweka Miundombinu  bora kwa watu wenye Ulemavu katika majengo,barabara,makaazi maeneo ya kupumzikia na maeneo mengine.
Aidha alisema kuwa pia kutakuwa na ripoti ya serikali kuhusu maombi ya wananchi wa Kisakasaka Zanzibar kuhusu namna wanavyoweza kufaidika kutokana na machinjio ya wanyama yaliyopo maeneo yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.