Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Awatunuku Stashahada, Shahada na Uzamivu Wahitimu wa SUZA leo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA) Dk. Ali Mohamed Shein, akiwahutubia na kutowa nasaha zake kwa Wahitimu wa SUZA wakati wa hafla hiyo ya Mahafali ya 13, yaliofanyika katika Ukumbi Mpya wa Chuo hicho uliofunguliwa leo na kuita Dk. Ali Mohamed Shein Hall Tunguu.(SUZA)

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Tume ya Mipango kufahamu mahitaji ya Serikali kwa kila fani kwa kila mwaka.

Kwa kufanya hivyo, Serikali itafahamu idadi halisi ya wanafunzi wanaohitajika na kuweza kujua namna ya kuwaajiri vijana, vyenginevyo wakifundishwa vijana bila ya mpango Serikali itajikuta ina idadi kubwa ya wahitimu bila ya ajira.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika Mahafali ya Kumi na Tatu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), huko katika ukumbi wa Chuo hicho Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hotuba hiyo, Dk. Shein alitoa indhari hiyo ili kuepuka kupata matatizo ya kuwa na wasomi wengi ambao hatimae watakuwa hawana kazi za kufanya, “lazima tuwe na malengo na mipango madhubuti...tusifanye kwa pupa, kasi wala papara”,alisisitiza.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kukiagiza Chuo hicho kushirikiana na BAKIZA pamoja na Taasisi mbali mbali zinazoshughulikia maendeleo ya Kiswahili katika kuimarisha ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni hapa Zanzibar na kukitaka Chuo hicho kujiandaa, kujitangaza na kujitahidi ili maendeleo yanayotarajiwa yapatikane.

Agizo hilo limekuja baada ya kuwepo idadi ndogo ya wanafunzi wa kigeni chuoni hapo ambapo idadi hiyo haitoi picha nzuri kwani inaonesha idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaojiunga inashuka mwaka hadi mwaka badala ya kupanda hasa ikitiliwa maanani kuwa Zanzibar inategemewa kushika usukani wa kukuza lugha ya Kiswahili.

Hivyo, Dk. Shein alieeleza kuwa SUZA kupitia Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni lazima ifanye utafiti na kuandaa mikakati itakayosaidia kukiimarisha Kiswahili na kuongeza idadi iliyopo hivi sasa ya wanafunzi wa nje wanaojiunga na masomo ya Lugha ya Kiswahili.

Dk. Shein aliwatoa wasi wasi wanafunzi wote waliofaulu na wanaoendelea kusoma Shahada ya “Environment Health” kwamba Serikali inashughulikia suala la mafunzo ya mazoezi yaani “intership” na kuiagiza Kamati ya Wataalamu wa Wizara ya  Elimu na Mafunzo ya Amali, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Wizara ya Afya, ili mazoezi hayo yaanze hivi karibuni hapa hapa Zanzibar.

Alisisitiza kwamba hapana hata mwanafunzi mmoja atakaekoseshwa nafasi hio na hapatakuwa na haja ya wanafunzi kusafiri kwenda sehemu nyengine kwani wamefundishwa Zanzibar na mipango yao itaandaliwa Zanzibar na yale yanayohitajika katika mazoezi hayo, yatatekelezwa hapa hapa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kufarajika kwa kuazishwa fani tatu mwaka huu baada ya kupata vigezo vya Tume ya Vyuo Vikuu vya Tanzania (TCU), ambazo ni Shahada ya Uzamili ya Sayansi na Tabianchi na Usimamizi wa  Rasilimali, Shahada ya Uzamili ya Elimu ya Vijana, Jisnia na Maendeleo na Shahada ya kufundisha Lugha ya Kiswahili kwa Wageni.

Dk. Shein alieleza kuwa fani zote zinazosomeshwa Chuoni hapo ni muhimu na zimeanzishwa kwa wakati mzuri hasa katika kuipatia nchi wataalamu wa kuisaidia kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya tabianchi na kupata wataalamu watakaochochea maendeleo ya vijana na masuala ya jinsia katika kukabiliana na changamoto zilizopo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wana “Diaspora” ambao ni wataalamu wa lugha kwa mapenzi na uzalendo wao kwa nchi yao kwa kumkubalia kuja nchini kuendesha mafunzo ya Shahada za Juu za Lugha ya Kiswahili katika chuo hicho.

Alieleza  kuwa Serikali tayari inakamilisha Sera ya “Diaspora” na itaanza kutumika, ili iweze kutoa mwongozo ili wana “Diaspora” washiriki katika maendeleo hapa Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa mwaka huu wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Utalii na Masoko wameanza kupatikana  hatua ambayo ni muhimu katika kuendeleza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii.

Hivyo, hali hiyo itapunguza na hatimae kuondoa tatizo linalolalamikiwa kwa muda mrefu kwamba vijana wa Zanzibar wanakosa fursa bora za ajira katika mahoteli mbali mbali ya Kitalii yanayoanzishwa hapa Zanzibar kwa kigezo cha kukosa sifa zinazohitajika.

“Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo italazimika iandae utaratibu, ili wahitimu hawa waweze kutumika katika kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini”,alisisitiza Rais Dk. Shein.

Rais Dk. Shein, alikipongeza Chuo cha SUZA, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Fedha kwa kutekeleza agizo lake la kujengwa kwa ukumbi huo mpya ambao kwa mara ya kwanza hivi leo umeanza kazi na kuahidi kuwa utaendelezwa ili uzidi kukidhi haja. Pia, aliwapongewa wahitimu wote waliomaliza masomo yao leo.

Mapema Rais Dk. Shein aliuzindua ukumbi mpya wa Chuo hicho ulioitwa jina la Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein na kupata maelezo juu ya hatua za ujenzi wa ukumbi huo.

Pamoja na hilo, Dk. Shein aliwatunuku wahitimu watano Shahada za Uzamivu za Kiswahili, 21 Shahada za Uzamili za Kiswahili, Sayansi za Mazingira na Kemia, asilimia 37.6 ya wahitimu aliwatunuku Shahada za Kwanza, asilimia 46.3 ni wahitimu ngazi za Stashahada na asilimia 14.2 ni ngazi ya Cheti.

Pia, Rais Dk. Shein aliwatunuku zawadi wanafunzi bora wa Chuo hicho kwa mwaka huu ambapo mwanafunzi bora zaidi alikuwa ni Aisha Ali Abdallah ambae ni Mhitimu wa Shahada ya Tehama na Uhasibu.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Idris Rai alieleza kuwa ukumbi huo umegharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo mpaka uliofikia umeshagharimu shilingi za kitanzania bilioni moja ambao unachukua watu zaidi ya 300.

Aidha, Profesa Rai, alieleza kuwa jitihada za kukikuza Chuo zinaonekanwa kupitia ongezeko la wahitimu wa SUZA ambapo katika Mahafali ya tisa yaliofanyika mwaka 2010, idadi ya wahitimu wa ilikuwa 320 na mwaka huu imefikia 2099.

Makamu Mkuu huyo aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa michango yake katika kukiendeleza Chuo hicho pamoja na Rais Dk. Shein mwenyewe binafsi kwa kuipa elimu ya Juu kipaumbele inachostahiki.

Kaimu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali ambaye pia, ni Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alimpongeza Dk. Shein kwa kuziunganisha Taasisi za Elimu ya Juu za Serikali kuwa sehemu ya Vitengo vya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.