Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Afungua Jengo la Mahakama ya Wilaya Mwanakwerwkwe Zanzibar leo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Jengo Jipya la Mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Mahkama ya Wilaya Mwanakwerekwe kutatoa fursa kwa Mahakimu watakaoitumia Mahkama hiyo kufanya kazi kwa bidii, weledi sambamba na kufuata maadili ya kazi zao.

Rais Dk. Shein ameyasema hayo leo mara baada ya kulizindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe, mjini Unguja baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa.

Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza Mahakimu kuwa hivi sasa watafanya kazi zao kwa furaha kwani kila Hakimu atakuwa na ofisi yake tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo walikuwa wakikaa zaidi ya mmoja na kuwa kikwazo katika utendaji wao wa kazi.

Alisema kuwa jengo hilo litatoa changamoto kwao kwani hapatarajiwi kuwa na ucheleweshaji wa mashauri ambao si utaratibu mzuri kwa mahakama.

Dk. Shein alisema kuwa Mahkama ni chemchem ya kutoa haki na kila mtu anayekwenda Mahkamani anakwenda kufuata haki, hivyo ni juu ya Mahakimu kufanya haki katika kesi wanazozihukumu na wasikurupuke wala kubabaisha.

Alieleza kuwa mara nyingi haki hukosekana kutokana na vitu vingi ikiwemo suala la rushwa ambalo Serikali yake inalipiga vita kwa nguvu zote sambamba na kuwepo suala la kujuana ambalo nalo husababisha mwenye haki kunyimwa haki na kupewa ndugu au rafiki.

Aidha, alieleza kuwa Serikali ina wajibu wa kutayarisha sera na sheria zinazoimarisha na kukuza fursa ya kupata haki nchini sambamba na kuwa na wajibu mkubwa wa kuziimarisha na kuziwezesha Taasisi mbali mbali za Serikali zenye majukumu ya kutoa na kupanua fursa za kupata haki.

Aliwasihi wananchi wote wasichelewe kufika Mahkamani kudai haki zao pale wanapohisi wamedhulumiwa haki zao na waepuke kwenda sehemu nyengine ambazo haziwezi kusaidia au kuweka pembeneni uamuzi uliotolewa na chombo hicho.

Pia, aliwataka wananchi washirikiane na wahusika mbali mbali hasa wanapotakiwa kutoa ushahidi katika kesi za jinai zinazofunguliwa Mahkamani kuhusu kesi za ubakaji, udhalilishaji dawa za kulevya na nyenginezo. “ushahidi ni jambo muhimu sana unaosaidia hukumu ifanyike kwa haraka”,alisisitiza Dk. Shein.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kushikamana na kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, dawa za kulevya na maovu mengine yanayodhorotesha maendeleo katika jamii.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza juu ya jukumu la mahakama la kuwaelimisha wananchi juu ya shughuli inazozifanya pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana huku akiuhakikishia umuhimu huo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha zinajengwa mahakama za kisasa pamoja na kuwa na utaratibu wa kudumu wa kuzifanyia ukarabati mahkama hizo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inajenga haraka jengo la Mahkama Kuu huko Tunguu ambapo mnamo mwaka 2020 yeye mwenyewe akalizindue tena si zaidi ya hapo kwani mda haupo.

Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alisema kuwa uzinduzi wa Mahkama hiyo ni miongoni mwa muendelezo wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Sheria, Zanzibar kwa mwaka huu wa 2018.

Alieleza kuwa uzinduzi huo ni muhimu sana kwa sababu inabeba wananhi wengi wanaokuja kupata huduma kutoka Wilaya ya Mjini na Magharibi ambapo kutokana na wingi wa kesi zilizopo wamelazimika kuweka Mahakimu wengi ili waweze kuhudumia vyema wananchi.

Alisema kuwa kwa sasa Mahkama hiyo ina Mahakimu wa Wilaya sita wanaume wanne na wanawake wawili na Mahakimu wa Mahkama ya Mwanzo saba wanaume watano na wanawake wawili na kueleza kuwa kutokana na wingi wa Mahakimu na uchache wa vyumba baadhi ya Mahakimu walilazimika kutumia ofisi moja kwa Mahakimu wawili.

Hivyo, kutokana na hali hiyo ndio walipokuja na wazo hilo la kuifanya upanuzi wa jengo kwa kuongeza vyumba, ghala, vyoo na ofisi nyenginezo huku akieleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni furaha kwao lakini changamoto kwa Mahakimu wa Mahkama hiyo kwani sasa watatakiwa kuonyesha jitihada zao za kazi za kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi kwa haraka.

“Uongozi wa Mahkama utafuatilia kwa karibu sana shughuli za Mahkama hii ili kuhakikisha kuwa ni za ufanisi. Mahkama hii itatoa nafasi nzuri ya kuwapima Mahakimu wetu katika kuamua mashauri kwa usahihi na kwa wakati”,alisema Jaji Makungu.

Aidha, Jaji Makungu alisema kuwa tatizo la udhalilishaji wa watoto na wanawake nalo ni miongoni mwa kesi nyingi zilizofunguliwa katika mahkama kwa mwaka uliomalizika ambapo takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka 2017 zilipokelewa kesi 105 za udhalilishaji Mahakamani Unguja na Pemba na kati ya kesi hizo 57 zilimalizwa na zilitolewa hukumu.

Mapema Kaimu Mrajis  wa Mahkama Kuu, Isaya Kayange akitoa taarifa ya matengenezo ya jengo hilo alisema kuwa matatizo makubwa ambayo yalikuwepo kabla ya matengenezo hayo ya hivi sasa ilikuwa ni uchache wa ofisi za kufanyia kazi kwa kutumiwa na Mahakimu na wafanyakazi wengine, kuvuja kwa jengo na mfumo mbovu wa majitaka na umeme.

Alisema kuwa kutokana na ubovu wa jengo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilitenga bajeti kwa lengo la kulifanyia matengenezo makubwa jengo hilo na mnamo tarehe 20 Februari, 2017 wafanyakazi wa Mahkama hiyo walihama kwa ajili ya kupisha ujenzi huo.

Kwa maelezo ya Kaimu huyo Mrajis, alieleza kuwa ujenzi huo ulisimamiwa na Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo mjenzi aliechaguliwa kufanya kazi hiyo ni Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), ambapo gharama ya ujenzi huo ni TZS Milioni 176.4

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine ambapo kikundi cha Black Root kinachoongozwa na msanii Makombora kilitumbuiza kwa mchezo wa kuigiza unaoendana na masuala ya sheria pamoja na uzinduzi wa jengo hilo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.