Habari za Punde

Serikali yaendelea kutoa elimu juu ya fursa katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki

Na Miza Kona - Maelezo 
SERIKALI ya Mapinduzi ya Mapinduzi imesema inaendelea kutoa elimu ya masuala ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na fursa zinazopatikana katika maeneo mbali mbali nchini.
Elimu hiyo hutolewa kwa wajasri amali, wafanyabiashara na makundi mengine ya wananchi katika mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba ambayo imeleta mwamko kwa Wazanzibar kutumia soko la Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Issa Haji Ussi (Gavu) huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni Mhe. Miraji Khamis Mussa aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani ya kuwafikishia wananchi wake taarifa muhimu za kimaendeleo zinazopatikana kwenye vikao vya jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waziri Gavu alieleza kuwa kuna fursa mbalimbali ambazo wananchi wa Zanzibar wanafaidika na mtangamano wa Jumuiya hiyo ni pamoja na kubadilishana utaalamu katika sekta za elimu, afya, nishati na mazingira kwa nchi wanachama , kuwepo Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili duniani, utalii na ajira.
“Hivi karibuni lilifanyika kongamano kubwa la matumizi ya lugha ya Kiswahili hapa Zanzibar ambapo wataalamu mbalimbali kutoka nchi wanachama walishiriki  pamoja na wajasiriamali wapatao 33 wa Zanzibar wataungana na wenzao wa Jumuiya Jumuiya ya Afrika Mashariki huko Burundi katika maonesha ya Juakali, Nguvu Kazi,” alieleza Waziri Gavu.
Wakati huo huo Waziri Gavu alisema Serikali imepitisha Sera ya Diaspora Zanzibar na kuagiza utekelezaji wake tangu mwezi wa Julai 2017 hatua zinazoendelea hivi sasa ni Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni kuitangaza sera hiyo pamoja na kukutana na wahusika wote ili kurahisisha utekelezaji wake jambo ambalo litatekelezwa katika mwaka huu wa fedha.  
Alieleza kuwa  sio kweli kuwa Wanadiaspora wamekosa kiunganishi kizuri katika kuwaunganisha kati yao na serikali ambapo kuinganishi kikubwa ni uwepo wa Idara Maalum wamekuwa washirikiana vizuri takriban kipindi cha miaka minne wamekuwa wakiandaa makongamano kwa ajili ya kubadilishana mawazo na serikali.
“Ni imani yetu kwamba Ofisi zetu za Kibalozi nje ya Nchi na Asasi na Jumuiya za Diaspora hao kikanda tutaendekea kuimarisha mahusiano yetu, upatikanaji wa sera hii ya Diaspora Zanzibar ndio uthibitisho tosha wa utayari wa Serikali katika kushirikiana na wenzetu hao,” alifahamisha Waziri Gavu.

Waziri Gavu alisema kwa upande wa Jumuiya za Wanadiaspora serikali inashirikiana nazo ni Jumuiya ya Wazanzibar wanaoishi nchi za Scandinavia (ZANDIAS), Jumuiya ya Wazanzibar wanaoishi Canada (ZACADIA), Jumuiya wa Zanzibar wanaoiishi Marekani (DICOTEA), Jumuiya wa Wanzibar wanaoishi Maryland Marekani (HEAD INC), Jumuiya  ya Wazanzibar wanaoishi nchini Uiengereza (ZAWA) pamoja na Jumuiya Wazanzibar wanaoishi Binmingham nchini Uiengereza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.