Habari za Punde

Rais Dk Shein akutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Kushan Asia Aroma Cooperation kutoka China

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Kampuni ya "KUSHAN  ASIA AROMA COOPERATION LIMITED" kutoka  China Bw.Zhou Junxue akiwa na Ujumbe wa Viongozi aliofuatana nao leo walipofika Ikulu Mjini Zanzibar.[Picha na Ikulu] 09/04/2018.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza  Mwenyekiti wa Kampuni ya "KUSHAN  ASIA AROMA COOPERATION LIMITED" kutoka  China Bw.Zhou Junxue (katikati) walipokuwa katika mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni hiyo walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo.[Picha na Ikulu] 09/04/2018.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza  Mwenyekiti wa Kampuni ya "KUSHAN  ASIA AROMA COOPERATION LIMITED" kutoka China Bw. Zhou Junxue (kushoto) walipokuwa katika mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni hiyo walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo (katikati) Bw.Guang William-Meneja Mauzo,[Picha na Ikulu] 09/04/2018.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na  Mwenyekiti wa Kampuni ya "KUSHAN  ASIA AROMA COOPERATION LIMITED" kutoka China Bw.Zhou Junxue (kushoto) walipokuwa katika mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni hiyo walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo (katikati) Bw.Guang William-Meneja Mauzo,[Picha na Ikulu] 09/04/2018.


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                09.04.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Kampuni ya ‘Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China kwa uamuzi wake wa kuja kuekeza hapa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China ambayo imedhamiria kuekeza katika kiwanda cha Makonyo, kilichopo Wawi Pemba kwa kushirikiana na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliihakikishia Kampuni hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushirikiano wake mkubwa kupitia Wizara yake ya Biashara na Viwanda pamoja na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” chini ya Mwenyekiti wake Zhou Junxue kwa kusaini Makubaliano ya Awali kati ya Kampuni hiyo na Shirika la (ZSTC).

Aidha, Dk. Shein aliueleza ujumbe wa Kampuni hiyo kuwa Kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi ni cha muda mrefu ambacho kimekuwa kikizalisha mafuta ya aina mbali mbali hivyo, ushirikiano wa pamoja katika uzalishaji kiwandani hapo kutasaidia kuinua ubora wa kiwanda sambamba na kuongeza pato la Taifa na soko la ajira.

Alieleza kuwa uwamuzi wa Kampuni hiyo ni mzuri na umekuja katika wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, hivyo hatua hiyo itakuwa chachu katika kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na viungo vya vyakula vya aina nyingi ambavyo miongoni mwao vimekuwa vikitoa mafuta bora ambayo yamekuwa ni bidhaa muhimu iliyoingia katika soko la ndani na nje ya Tanzania yakiwemo mafuta ya makonyo, mafuta ya karafuu na  mafuta ya mikaratusi.

Hivyo, Dk. Shein aliongeza kuwa kuanza kwa uwekezaji huo kutazidi kuitangaza Zanzibar na kuwa kiwanda cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinachozalisha bidhaa hizo za mafuta.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya Kampuni hiyo kushirikiana na ZSTC katika kutekeleza makubaliano hayo yaliotiwa saini hapo jana ikiwa ni pamoja na kuongeza zaidi uzalishaji huku akisisitiza suala zima la ufanyaji utafiti katika kilimo cha mazao hayo yanazotoa mafuta.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza suala la mafunzo ambalo litasaidia sana kuendesha kiwanda hicho pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za aina mbali mbali za mafuta ya viungo kutoka katika kiwanda hicho cha Makonyo Wawi jambo ambalo pia, litaongeza soko la ajira hapa nchini.

Nae Mwenyekiti wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya China, Zhou Junxue alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar kwa kupitia sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vidogo na vya kati.

Mwenyekiti wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” alimueleza Rais Dk. Shein mikakati iliyowekwa na Kampuni yake katika kuhakikisha makubaliano waliyosaini yanatekelezwa kwa lengo la kuleta manufaa kwa pande zote mbili.

Junxue alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Kampuni yake itatoa mashirikiano makubwa kwa Serikali kupitia Shirika lake la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuhakikisha kiwanda hicho kinatoa mafuta yalio bora sambamba na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazozalishwa katika kiwanda hicho cha Wawi.

Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya nchini China ambayo ndio mnunuzi mkubwa wa mafuta ya viungo vya Zanzibar tokea Julai mwaka 2017, ilitiliana saini Makubaliano ya Awali na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuendesha mradi ndani ya miaka kumi utaohusisha uimarishaji wa utendaji na utaalamu katika kiwanda cha Makonyo Wawi.

Jambo jengine ni uendelezaji wa mazao ya karafuu na mikaratusi ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 60 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia tani 2,000,
ubadilishanaji uzoefu kati ya watendaji wa taasisi hizo, upatikanaji wa mafunzo, mbinu na upatikanaji  mbegu bora za mikaratusi ni miongoni mwa makubaliano hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.