Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Balozi Seif Ali Iddi Akijumuika na Wazee wa Nyumba ya Wazee Sebleni katika Iftari Aliyowaandalia Jana.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wazee wanaotunzwa na Serikali katika Nyumba za Wazee Sebleni alipofika kufutari na pamoja ndani ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Baadhi ya Wazee wa Nyumba za Serikali za  kutunza Wazee zilizopo Welezo wakijipatia Futari pamoja na Wananchi waliojumuika nao pamoja ndani ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Baadhi ya Wazee waliojumuika pamoja na Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi wengine katika Futari ya pamoja hapo Nyumba za Wazee Sebleni Mjini Zanzibar.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya Futari ya pamoja katika Nyumba za kutunzia Wazee zilizopo Welezo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kusisitiza na kuwakumbusha Wananchi wote kutoa Taarifa mara moja katika vyombo vya  Ulinzi  pale wanapoona ishara ya Mtu au kikundi cha Watu wameonyesha cheche ya uvunjifu wa Amani hapa Nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kufutari pamoja na Wazee wanaotunzwa  na Serikali katika Nyumba za Wazee za Sebleni na Welezo kwa siku mbili tofauti ndani ya Kumi la Tatu la na la Mwisho la Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Balozi Seif  Ali Iddi ambae kauli yake hiyo imetolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema  Watoto wa sasa lazima warithishwe Utamaduni wa asili wa Kizazi chao katika kudumisha Umoja na Amani uliojengeka kwa Karne kadhaa zilizopita.
Alisema Serikali kamwe haitakubali kuruhusu baadhi ya Watu kuichezea Amani ya Taifa iliyopo ambayo inatoa fursa kwa kila mwana Jamii kuendelea na shughuli zake za Kimaisha bila ya bughudhiwa kama  wasi wasi  unavyowakumba  baadhi ya Watu kwenye Mataifa mengine Duniani.
Balozi Seif  kupitia Mkuu huyo wa Mkoa Mjini Magharibi alikumbusha Taarifa zitakazotolewa na Wananchi  dhidi ya wavunjifu wa Amani zikaenda sambamba pia dhidi ya Wafanyabiashara wanaoongeza bei za Bidhaa Muhimu hasa katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kwa makusudi kuondosha kodi kwa Bidhaa muhimu kama Mchele, Sukari, Unga, na bidhaa za nafaka kwa lengo la kuwarahisishia Wananchi kupata huduma hizo kwa unafuu zaidi.
Alisema Vyombo vya Ulinzi kwa kushirikiana na Masheha, Wakuu wa Wilaya na Mikoa watakuwa tayari kuwachukulia hatua za Kisheria Wafanyabiashara wote watakaoendeleza tabia hiyo mbaya na kijahili ya kuongeza bei za bidhaa bila ya kuwa na sababu za msingi.
Aliwawanasihi Wafanyabiashara  wote kuchukuwa wito wa Serikali pamoja na maelekezo ya Mafundisho ya Viongozi wa Dini yanayosisitiza umuhimu wa kuoneana huruma katika upatikanaji wa huduma muhimu.
Akigusia mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaoendelea ukiwa katika Kumi la Mwisho la Kuachwa Huru na Moto alisema Futari ya pamoja ni ishara ya upendo unaowaunganbisha Viongozi, Wananchi na Waumini wote bila ya kujali Uwezo, itikadi za Kisiasa na hata zile za Kidini.
Alisema utaratibu wa kula pamoja huleta baraka ambayo hutoa fursa kwa Wananchi wasio na uwezo kujumuika pamoja mfumo unaojenga mazingira  ya mahusiano ya karibu zaidi.
“ Mkusanyiko unaopatikana katika futari ya pamoja huleta ladha ya upendo kwa vile hujumuisha pia Wananchi na Waumini wasio na kitu na wale wa Dini nyengine”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akigusia suala  la Afya  Bora Balozi Seif Ali Iddi aliwahimiza Wananchi kuchukuwa tahadhari ya Afya muda wote licha ya kwamba Taifa kipindi hichi halijakumbwa na miripuko  ya maradhi ya kuambukiza.
Alisema Serikali Kuu kupitia Wizara inayosimamia masuala ya Afya imekuwa ikitoa Elimu na tahadhari kwa Wananchi juu ya kujikinga na maradhi mbali mbali lengo likiwa kuwa na Taifa lenye Afya Bora na Ustawi unaokubalika Kidunia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.