Habari za Punde

Mtandao wa JamiiForums wafunguliwa tena Tanzania

Jukwaa maarufu nchini Tanzania JamiiForums hatimaye limefunguliwa baada ya kufungwa kwa takriban wiki mbili, kufuatia kuanza kutekelezwa kwa sheria mpya za mtandaoni nchini humo.
Kulingana na ujumbe uliosambazwa katika ukurasa wa Twitter wa tovuti hiyo, kwa sasa ujumbe ambao ulikuwa umepakiwa awali unaweza kusomwa.
Mkurugenzi wa mtandao huo Maxence Melo aliyekuwa akijibu ujumbe wa mmoja wa wateja wake katika mtandao wa Twitter amenukuliwa katika ujumbe huo akisema hata hivyo kwamba watumiaji wa mtandao huo hawawezi kuchapisha ujumbe mpya kwa sasa.
Aliongezea kusema kwamba hatua za kurejesha operesheni zote kama ilivyokuwepo mwanzo zinaendelea.
Kwa sasa habari za mtandao huo ambazo zilikuwa zimechapishwa kuanzia 10 Juni kwenda nyuma kabla ya kufungwa kwa jukwaa hilo zinaweza kusomwa.
Hata hivyo haijajulikana ni lini operesheni kamili za mtandao huo zitaanza ili wasomaji kuanza kuchangia.
Walipofunga mtandao huo, taarifa zote zilizokuwa zimepakiwa kwenye mtandao huo zilikuwa hazipatikana.
Wasimamizi wake walikuwa wameweka tangazo la kuwajulisha kuhusu kuathiriwa kwa mtandao huo na kanuni mpya za serikali.
"Kwa wateja wetu walio nchi nyingine, huduma hii itarejea mapema zaidi lakini kwa walio Tanzania kurejea kwa huduma kutategemeana na matokeo ya hatma ya jitihada za wawakilishi wetu walio Tanzania," walikuwa wameandika.
"Tunasikitika kuwa tunalazimika kufikia hatua hii ghafla lakini ni matumaini yetu kuwa wateja wetu mtaendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki."
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA ilikuwa imetoa agizo kwa kwa wahudumu wote ambao bado walikuwa hawajapata leseni kukoma kutoa huduma zenye maudhui mtandaoni.
Mtandao huo wa Tanzania ni maarufu kwa kufichua mambo mbalimbali na kama jukwaa la watu kutoa maoni haswa wale walio nchini Tanzania na nchi za kigeni.
Sheria hizo mpya za TCRA ziliwahitaji wachapishaji wa mitandao na wanablogi kufichua wachangiaji na wamiliki kitu ambacho Bw Melo anasema kuwa ni kizingiti kwa kazi yao.
Hivi majuzi mtandao huo ulijitenga na mtandao mwengine unaotumia jina kama hilo nchini Kenya.
Mike Mushi, mwanzilishi mwenza wa Jamii Forums alikuwa awali ameambia BBC kwamba kanuni hizo za TCRA, ambazo zinawataka wachapishaji wa taarifa zenye maudhui mtandaoni kuhifadhi maelezo ya wachangiaji kwa miezi 12 huenda zikaathiri mtandao wa Jamii Forums.
"Sheria hizi zinaenda kinyume na jinsi sisi huendesha shughuli zetu. Huwa twawaruhusu watumiaji wetu kuandika ujumbe bila majina yao kutambulishwa, hivyo itatulazimu kufikiria kwa kina iwapo tutaweza kuendeleza kuendesha shughuli zetu."
Alisema mtandao huo kufikia Aprili ulikuwa na watumiaji 3.7 milioni kwa mwezi na walikuwa wanapokea ujumbe takriban 20,000 kila siku.
Na muda mfupi baada ya kufungwa kwa mtandao huo pamoja na tovuti nyengine tofauti nchini humo, Chama cha upinzani Tanzania ACT Wazalendo kilisema mwenendo wa serikali kudhibiti mitandao ya kijamii unaonesha nia ya kutaka kuminya haki zote za msingi za raia.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, Katibu Mwenezi wa chama hicho Ado Shaibu alisema ''taratibu kila mtu, haijalishi ni wa chama au cheo gani, atafikiwa na ukandamizaji huu wa serikali''.
Chama cha Upinzanzi nchini Tanzania, ACT Wazalendo, kilisema kuanza kwa kutekelezwa kwa kanuni za maudhui mtandaoni ni ishara nyingine ya jinsi ambavyo serikali nchini humo inaendelea kuminya uhuru wa habari na watu kujieleza.
Chanzo cha Habari BBC.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.