Habari za Punde

Taasisi ya Kiraia ya Zanzibar Relief And Development Foundation Yakabidhi Msaada wa Vyakula.

Mratibu wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinaadamu la Nchini Uturuki {TIKA} Bwana  Hikmat Ozdenoglu Kulia akimkabidhi Sadaka Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya Wazee wasiojiweza wa Jimbo lake.
Balozi Seif akiwakabidhi Sadaka za Vyakula Masheha wa Shehia zilizomo ndani ya Jimbo lake kwa ajili ya Wazee wasiojiweza wa Jimbo lake hapo Nyumbani kwake Kama.
Balozi Seif  kushoto akimkabidhi Vyakula Kiongozi wa Nyumba za Kurekebishia Tabia {Sober House}Nd. Sabri Omar Ali kwa ajili ya Matumizi ya Vijana waliopo kwenye Nuyumba hizo.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Taasisi, Mashirika na Watu wenye uwezo Kimaisha  bado wana wajibu wa kuendelea kuisaidia Jamii Duni  inayowazunguuka ili kuongeza upendo na ukaribu miongoni mwao.
Alisema hatua hiyo inayohitaji zaidi imani ya kweli inayojengeka ndani ya moyo huongeza baraka lakini kwa upande mwengine hutoa nafasi ya kuitakasa Mali wanayoichuma wenye uwezo katika harakati zao za kujitafutia Maisha.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo hapo Nyumbani kwake Kama Nje kidogo ya Kaskazini ya Mji wa Zanzibar wakati akiwakabidhi sadaka za vyakula mbali mbali Masheha waliomo ndani ya Jimbo la Mahonda kwa ajili ya Wazee wasiojiweza pamoja na Watu wenye mazingira magumu ili waweze kusherehekea vyema Siku Kuu ya Idd El – Fitri inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Wiki hii.
Msaada huo wa vyakula umetolewa na Ujumbe wa Viongozi wa Shirika  la Kimataifa la Misaada ya Kibinaadamu la TIKA kutoka Nchini Uturuki kwa kushirikiana na Taasisi ya Kiraia ya Zanzibar  Relief and Development Foundation { ZANRDEF}.
Balozi Seif ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliziongeza Taasisi hizo mbili kwa moyo wao wa imani unaowakumbuka Wazee pamoja na Watu wenye mazingira magumu wanaohitaji msukumo wa msaada katika kukidhi maisha yao.
Aliwanasihi Masheha waliokabidhiwa sadaka hiyo kuhakikisha kwamba unawafika walenga ili kuwapa nguvu zaidi wahisani wanaoamua kujitolea kwa lengo la kusaidia Makundi hayo Nchini.
Alisema haitopendeza kusikia kwamba wapo  Watu watakaopewa sadaka hiyo wakati wana nguvu kamili za kufanyakazi za kujitafutia riziki ya halali kwa sababu tu ya ukaribu wao na Masheha waliopewa dhamana na jukumu la kusimamia zoezi la ugawaji wa sadaka hiyo.
Mapema Naibu Katibu wa Taasisi ya Zanzibar  Relief and Development Foundation { ZANRDEF} Bwana Hamid Abdullah Hamid  alisema Taasisi yake imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinaadamu la TIKA kutoka Nchini Uturuki.
Bwana Hamid alisema ushirikiano huo tayari umeshaleta neema kubwa kwa Jamii kutokana na Miradi ya Taasisi hizo iliyolenga kusaidia Jamii hasa katika Sekta ya Maji na elimu ya Ujasiri amali inayoelekezwa kwa makundi ya Vijana na Wanawake.
Wakati huo huo Balozi Seif alikabidhi msaada wa vyakula mbali mbali kwa Vijana waliowahi kuathirika na matumizi ya Dawa za Kulevywa ambao kwa sasa wapo katika Nyumba za kurekebishia Tabia {Sober House} kwa matumizi yao ya kawaida.
Akimkabidhi Kiongozi wa Nyumba ya Kurekebishia Tabia Sabri Omar Ali,  Balozi Seif  aliendelea kuwakumbusha Viongozi hao kuzidisha juhudi kwenye eneo la uhamasishaji wa Vijana ili kundi hilo ambalo ndio nguvu Kazi ya Taifa  lijiepushe na  matumizi mabaya ya Dawa za kulevya.
Balozi Seif alieleza kwamba Jamii Mitaani imekuwa ikilidharau Kundi laWatu waliojiingiza katika Matumizi ya Dawa za kulevya hasa kutokana na vitendo vyao vinavyopelekea kuathirika Kiafya sambamba na kujiingiza katika vitendo vya Wizi na ujambazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.