Habari za Punde

TAMWA Yampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Ali Mohamed Shein.

TAMWA yampongeza Dk. Shein

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA, Zanzibar) kinampongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein kwa kuteua mwanamke mmoja kuwa mjumbe katika Tume ya Uchaguzi, Zanzibar (ZEC).

Kuteuliwa kwa mwanamke huyo kumefanya Tume hiyo iliyopata wajumbe wapya karibu na uchaguzi wa mwaka 2020 kuwa na asilimia 14.2 ya uwakilishi wa wanawake.Hali hiyo imeimarisha Tume iliyopita iliyofanya kazi tokea mwaka 2013 ambayo haikuwa na mwanamke hata mmoja.

Hivyo, TAMWA, Zanzibar inachukua nafasi hii kumpongeza pia mjumbe huyo (Bi Jokha Khamis Makame) aliyeteuliwa na kumtakia kila la kheri, busara, uweledi na haki katika utendaji wake.

Usawa wa kijinsia ni suala muhimu katika kipindi hiki hasa kwa vile kwa miaka mingi wanawake waliachwa nyuma katika ngazi za mbali mbali za uongozi, hivyo kubaki nyuma katika maendeleom pia, pamoja na kuwa wao wako zaidi ya asilimia 50 ya watu nchini.

Kutokana na hali ya kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia, mipango mbali mbali ya kitaifa, kikanda na kinchi imeandaliwa ili kufikia usawa wa kijinsia na hivyo kuleta uwiano katika jamii. 

Kwa mfano Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kipengele cha 12 (1) kinaeleza kuwa nchi zitahakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015, asilimia 50 ya nafasi zote za kitaifa na kibinafsi zinashikiliwa na wanawake.

Hivyo, TAMWA, Zanzibar inapenda kumkumbusha Mheshimiwa Rais pamoja na jamii kwa ujumla kuhusu wajibu huu mkubwa wa nchi katika kufikia malengo ya usawa wa kijinsia ambapo Zanzibar bado iko nyuma sana hasa katika nafasi zinazohusiana na masuala ya kisiasa.Ni vyema pia vyama vya siasa kuanza kujitafakari na kuangalia kuwa wanawake ni wadau wa maendeleo kama wanaume hivyo wanahitaji kushika nafasi muhimu za maamuzi ndani ya vyama vyao.

Dk Mzuri Issa,

Mkurugenzi,

TAMWA, Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.