Habari za Punde

Matayarisho ya Maandalizi ya Ujenzi wa Jengo la Beit Al Jaib Zanzibar.



Na Mwashungi Tahir        Maelezo           23-7-2018.
Matayarisho ya matengenezo ya Jengo la Kihistoria la Mji mkongwe la Beit el Ajaib yameanza rasmi kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Oman
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe Issa  Makarani Sariboko alieleza hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya maandalizi yanavyoendelea katika jengo hilo Forodhani.
Alisema ujenzi wa jengo hilo mashuhuri katika Ukanda wa Afrika Mashariki lililoporomoka mwaka 2012 litagharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni nne na nusu na matengenezo yake yatachukua miezi 18.
Aliwaeleza waandishi wa habari kwamba  wataalamu wazalendo wamemaliza  kufanya  uchambuzi wa matengenezo hayo na kazi ya ujenzi wa jukwaa  kuelekea sehemu ya juu unaendelea.
“Tayari wataalamu wetu wamemaliza kufanya ufafanuzi wa jumba lote kuanzia  sehemu ya juu iliyoporomoka, sehemu za ndani na eneo la chini ya ardhi ya jengo hilo’’, alisema Mkurugenzi Makarani.
Alisema kutakuwa na mchanganyiko wa timu ya wataalamu kutoka nchi za nje na wataalamu wazalendo wa Zanzibar ili kupata ufanisi mzuri wa ujenzi huo.
Nae Mkurugenzi  wa Makumbusho Salim Kitwana Sururu alisema Serikali ya Oman ilifikia makubaliano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya kulifanyia matengenezo jengo hilo la kihistoria lililohifadhi kumbukumbu muhimu za tawala zilizopita.
Muhandisi wa Mji Mkongwe  Suhad Sultani Alawi alitoa wito kwa wananchi wanaotumia eneo hilo kuwa tahadhari kubwa wakati wa matengenezo ya jengo hilo kwa kulinda usalama wao.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.