Habari za Punde

Taasisi na mashirika zaombwa kuchangia katika sekta ya Afya

Na Takdir Ali, Maelezo
   Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Zanzibar Bw.Salum Abdallah Hassan ameziomba Taasisi na Mashirika yanayoingiza kipato kupitia Wananchi kutoa michango yao katika sekta ya afya ili iweze  kukabiliana na matatizo mbali mbali yanayozikabili sekta hizo.
  Amesema huduma za Afya ni muhimu katika jamii hiyo inahitaji kusaidiwa kwa hali na mali ili ziweze kutoa hutuma nzuri kwa Wananchi hususan wa kipato cha chini ambao ndio tegemeo la wanyonge katika kupata matibabu ya afya zao.
   Akikabidhi vifaa vya usafi Katika Kituo cha Afya Mpendae na Shauri moyo Wilaya ya Mjini amesema Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ni Shirika la Serikali na limekuwa likichangia katika huduma  za kijamii na Taasisi kwa lengo la kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi.
    Amesema Vituo vya Afya vimekuwa vikihitaji vifaa vya kufanyia usafi na ndio wakaamua kukabidhi vifaa kama vile Viatu vya mvua, Sabuni na Dawa za kusafishia vyoo vyenye thamani ya sh.laki nane kwa makusudio.
    Amefahamisha kuwa kila mwaka wamekuwa wakichangia na kutoa misaada kwa washirika wao pale hali inavyoruhusu na kusema matumaini yao ni kuona vinasaidia katijka masuala ya usafi katika vituo hivyo na kuwaomba Wananchi waendelee kuliunga mkono Shirika hilo ili iweze liweze kutoa huduma bora kwa wateja wao.
    Kwa upande wake Daktari Dhamana wa Wilaya ya Mjini Dkt. Ramadhani Mikidad  Suleiman amelipongeza Shirika la Umeme Zanzibar kwa kutoa msaada huo na na kusema utawasaidia katika kufanyia usafi na kuweza kujikinga na maradhi ya mripuko yanayoweza kujitokeza kutokana na mazingira machafu.
       Dkt. Mikidadi amewaomba zeco kuzidi kuwaangalia kwa jicho la huruma sekta za Afya kwani zinazokabiliwa na matatizo mbali mbali zinazopelekea kushindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi.
  Amesema jukumu la kuhudumia masuala ya Afya sio la Serikali pekee hivyo ni vyema kwa Mashirika,Taasisi au Watu binafsi kujitokeza kuziunga  mkono ili ziweze kuwa endelevu.
      Mkuu wa kituo cha Mpendae Hamad Khamis Ali na Afisa wa Afya Rauhia Zamani Mshenga wameahidi kuvitunza na kuvienzi na kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi katika hali inayoridhisha na kuwaomba wananchi wanaotumia vituo hivyo kuwaunga mkono.
                  Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.