Habari za Punde

Taasisi ya Mo Dewji yatoa Milioni 125 kugharamia matibabu ya watoto wenye sarataniNa Mwandishi Wetu
Taasisi ya Mo Dewji imetoa msaada wa Tsh. 125 Milioni kwa kituo cha Tumaini la Maisha kilichopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ili kusaida kugharamia matibabu ya magonjwa ya saratani kwa watoto wanaopatiwa huduma katika kituo hicho.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Meneja Miradi wa Taasisi ya Mo Dewji, Rachel Chengula alisema msaada huo ni mwendelezo wa misaada ambayo imekuwa ikitolewa na taasisi kwa kituo hicho.

Alisema wanatambua hali ngumu ambayo wanapitia watoto hao wanapouguza magonjwa ya saratani, hivyo wanaamini msaada huo utasaidia kuboresha huduma kwa watoto waliopo kituoni hapo na kuwezesha watoto waliopo mikoani kusafirishwa ili kufikishwa hospitalini na wao wapatiwe matibabu.

“Kama upo hai na mwanao anapumua, mshukuru Mungu kuwa ana makusudi na wewe na ana makusudi na mtoto wako. Usikatishwe tamaa na magonjwa, tunaamini kwamba watoto hawa watapona na kurudi nyumbani, watasoma na watalitumikia Taifa letu,

“Kama mnavyofahamu Mohammed Dewji amekuwa akifanya kazi na Tumaini la Maisha tangu mwaka 2012 ili kusaidia watoto kupatiwa matibabu, na kupitia taasisi yake tutaendelea kushirikiana ili kusaidia watoto wetu wapatiwe matibabu,” alisema Chengula.

Naye Meneja wa Wafadhili wa kituo cha Tumaini la Maisha, Alex Kaijage aliishukuru Taasisi ya Mo Dewji kwa msaada ambao wamekuwa wakiwapatia na kuwaomba kuendelea kuwa na moyo huo wa kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani ili warejee katika hali ya kawaida na kuendelea na shughuli zingine ikiwepo kusoma.

“Tunajua kwamba tunahitaji sana sana hizi fedha kufanikisha matibabu ya hawa watoto, sio tu usafiri wa kutoka huko wanakotoka na kuja bali hata dawa ambazo tunazipata kwa sababu ya huu mchango ambao Mohammed Dewji ametuwezesha. Kwa sababu yenu watoto hawa wanapata matibabu, kwa sababu yenu wanapona kwahiyo tunawashukuru sana,” alisema Kaijage.

Kwa upande wa mmoja wa wazazi ambao mtoto wake anapatiwa matibabu katika hicho, Hamisi Samweli aliwataka wadau wengine wenye uwezo wa kifedha kuwa na moyo wa kusaidia kama anavyofanya Mohammed Dewji ili watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kifedha wapatiwe matibabu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.