Habari za Punde

Tamasha la Mzanzibari Kurindima Wiki Ijayo Katika Viwanja Vya Mapinduzi Square Michenzani Zanzibar. Tarehe 19-25/7/2018.

Na Mwashungi Tahir   Maelezo.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi  anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika  tamasha la Mzanzibar  ambapo linatarajiwa  kufanyika tarehe 19-25 mwezi huu  ambapo tamasha hilo hufanyika kila mwaka ifikapo mwezi wa saba. .
Hayo amesema Katibu mkuu wa Wizara ya  Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo  Hassan Omar  huko katika ukumbi wa mkutano ulioko Migombani wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu utaratibu mzima utaofanyika wa tamasha la Mzanzibar linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Alisema tamasha hilo la 23 la Mzanzibar hufanyika kila mwaka ifikapo mwezi huu kwa lengo kuu la  kukuza mila , silka na  utamaduni  wa kizanzibar baada ya kuona vijana wetu wengi mambo ya zamani hawajui.
Pia alisema mambo mengi ya kizanzibar ya kiasili yamebadilika hivyo kufanyika kwa tamasha hili  kutaweza kujulikana mambo mengi kwa vijana wetu ambapo walikuwa hawayajui zikiwemo ngoma za asili, vyakula  na baadhi ya mambo mengine ya kiasili.
Aidha aliwaomba wananchi washiriki kwa wingi katika tamasha hilo litalofanyika  katika Mapinduzi Square hapo Michenzani  ambapo kutakuwa na fensi, kazi za mikono za wajasiriamali maulidi ya home na mambo mengi ya kiasili ambayo mpaka wageni wetu wa utalii watafurahishwa na mambo hayo.
Vile vile alisema pia tunashirikiana na kamisheni ya utalii hivyo wageni wetu watapata fursa ya kuona mambo ya kizanzibar ambayo huwavutia sana  ambapo wazanzibar tunajivunia na mambo yetu ya kiutamaduni.
Alisema suala utamaduni ni muhimu ikiwemo lugha fasaha ya Kiswahili kwa kukizungumza na kuandika , aliomba tuikuze lugha yetu hii kwani kila siku Rais wetu anaipia kelele kwa lengo la kukithamini lugha yetu ya Kiswahili.
“Ni lazima tukienzi , tukithamini kwa kuandika , kuzungumza na hata kukitangaza Kiswahili chetu kwani Mh Rais wetu Dkt Ali Mohammed Shein anatuhimiza kudumisha matumizi ya Kiswahili sahihi” Alisema  Katibu huyo.
Alieleza utamaduni  unaporomoka  hivyo tuache kuiga mambo yasiyofaa na kuyadumisha mambo yetu ya kiasili kwa lengo la kukuza mambo yetu ya kiasili .
Alifahamisha tamasha hilo pia litakuwa na taarabu asilia, kongamano la wasanii, mchezo wa Ngo’mbe ambao utafanyika Pemba  na mabo mengi ya utamaduni wa kizanzibar yataweza kuonekana .
KAULI MBIU YA MWAKA HUU NI UTAMADUNI NI NGAO KWA USTAWI WA MAISHA YETU.
MWISHO.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.