Habari za Punde

TRA Yaendelea Kutoa Huduma Mbalimbali Katika Maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi ambaye pia ni Mratibu wa Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Bi. Honester Ndunguru (kushoto) akijadiliana jambo na Maafisa wa Kodi wakati wa maonyesho hayo yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Afisa wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Judith Lwaikondoakimhudumia mwanachi aliyetembelea Banda la TRA kwa ajili ya kupata huduma wakati wa Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Afisa wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Mercy Macha akitoa elimu ya kodi kwa wananchi waliotembelea Banda la TRA katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayofanyika katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akizungumzia juu ya TRA ilivyojipanga katika kutoa huduma kwa wananchi katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yaliyoanza tarehe 28 Julai, 2018 jijini Dar es Salaam.


Na Veronica Kazimoto. Dar es Salaam.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea maoni na mrejesho kutoka kwa wananchi, usajili wa walipakodi na kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla.

Akizungumzia juu ya TRA ilivyojipanga katika kutoa huduma kwa wananchi katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo amesema kuwa, wananchi watumie fursa hii kujifunza masuala mbalimbali ya kodi ili kuongeza uelewa na uhiari wa ulipaji kodi.

"Sisi kama Mamlaka tumejipanga kuhakikisha kuwa, tunatoa huduma kwa kila mwananchi atakayetembelea banda letu na tunapokea maoni na mrejesho kutoka kwa wananchi.

Vilevile tunasajili walipakodi, tunawaelimisha wananchi umuhimu wa kulipa kodi, tunaelezea haki na wajibu wa Mlipakodi kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Huduma na Mlipakodi pamoja na kuwaonyesha makusanyo yote ya miaka mitatu ya fedha iliyopita yaani kuanzia 2015/16, 2016/17 na 2017/18," alisema Kayombo.

Kayombo ameongeza kuwa, makusanyo yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ndiyo hutumika katika kutoa huduma mbalimbali za jamii ikiwemo miundombinu ya barabara na umeme, maji safi na salama, elimu pamoja na huduma za afya.

Naye Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi ambaye pia ni Mratibu wa maonyesho hayo kwa upande wa TRA Bi. Honester Ndunguru ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika banda la TRA ili waweze kupata elimu sahihi ya kodi na hatimaye waweze kulipa kodi stahiki na kwa wakati.

"Kila mwaka tunashiriki maonyesho haya ya Sabasaba lakini kwa mwaka huu tumejipanga vizuri zaidi hivyo nachukua fursa hii kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika banda letu ili tuwahudumie na kuwaelimisha juu ya masuala mbalimbali ya kodi na hatimaye waweze kulipa kodi sahihi na kwa wakati unaotakiwa," alisema Ndunguru.


Banda la Mamlaka ya Mapato Tanzania linapatikana ndani ya viwanja vya Sabasaba na lipo mkabala na banda la Azam ambapo wananchi wanaendelea kupata huduma mbalimbali zinazotolewa ndani ya banda hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.