Habari za Punde

WAZIRI MPINA ARUHUSU UINGIZAJI WA NYAVU ZA KUVULIA SAMAKI NA DAGAA KUTOKA NJE YA NCHI.


Na.Mwandishi Maalum.Dodoma.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameruhusu uingizaji wa vyavu za kuvulia samaki na dagaa kutoka nje ya nchi baada ya kubaini kuwa viwanda vya kuzalisha nyavu hizo vilivyopo nchini kushindwa kuhimili mahitaji ya soko la ndani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wavuvi.
 Akizungumza katika kikao cha tathmini ya operesheni Sangara 2018 jijini Dodoma, Waziri Mpina amemuagiza Katibu Mkuu- Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatama kuhakikisha kuwa katika kipindi cha siku 14 awe amekamilisha kupitia maombi na kuruhusu uingizaji wa nyavu hizo kutoka nje ya nchi. Pia kuweka utaratibu ambao hautaathiri soko la viwanda vya ndani.

Mbali na hilo Waziri Mpina ameigiza wizara yake kuandaa mkakati wa kudhibiti upotevu wa mapato, usimamizi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi nchini ili kuondoa mianya yote  ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuweka ulinzi thabiti wa rasilimali za uvuvi.
Pia ametaka Wizara hiyo kufanya mapitio ya mkakati wa ufugaji wa samaki kwenye maji, kufufua  vituo vya kuzalisha vifaranga na kufanya tathmini ya uwekezaji wa sekta binafsi na kuainisha mahitaji ya sasa ili kuongeza uzalishaji utakaochangia kupunguza nguvu ya uvuvi kwenye maziwa na  hivyo kutokomeza uvuvi haramu, kuongeza ajira na upatikanaji wa malighafi za viwanda nchini.
Akizungumzia matokeo ya operesheni Sangara 2018, Waziri Mpina alisema jumla ya watuhumiwa 3,998 walikamatwa kwa makosa mbalimbali na kutozwa faini na wengine kufikishwa Mahakamani,
nyavu haramu 575,152, makokoro 11,144 na kamba za kokoro zenye urefu wa mita 859,304 zilikamatwa na kuteketezwa kwa moto.Pia ndoano 1,910, 135 zisizoruhusiwa kisheria ziliharibiwa.
Pia kilo 359,869 za samaki wasioruhusiwa zilikamatwa na kutaifishwa na Serikali ambapo kilo 176,780 za samaki wachanga na wazazi ziligawiwa bure kwenye taasisi mbalimbali zikiwemo shule,magereza,hospitali na watu wenye mahitaji maalum huku kilo 183,059 za samaki wakavu (kayabo) pamoja na kilo 5,889 za mabondoziliuzwa kwa njia ya mnada.
Alizungumzia mafanikio ya operesheni hiyo, Waziri Mpina alisema miezi 6 (Julai-Disemba 2017) kabla ya operesheni Sangara 2018 jumla ya sh. Bilioni 8.5 zilikusanywa ikilinganisha na jumla ya sh. Bilioni 17.7zilizokusanywa miezi 6 (Januari- Juni 2018) kipindi cha operesheni.
Akitolea mfano Soko la Samaki la Kirumba jijini Mwanza, Waziri Mpina alisema mapato yake yameongezeka kutoka sh milioni 206.3 katika kipindi cha Julai-Dis 2017 kabla ya kuanza operesheni na kufikia sh milioni 848.3 katika kipindi cha Januari hadi Juni 2018 baada ya kuanza operesheni hii inaonesha kuwa kwa kipindi cha miezi sita mapato katika soko hilo yameongezeka mara nne.
Alisema jumla ya makusanyo ya sh.bilioni 26.3 yalikusanywa katika mwaka wa fedha 2017/2018 ukilinganisha na makusanyo ya jumla ya shilingi bilioni 18.5 yaliyokusanywa katika mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha katika kutekeleza operesheni hiyo jumla ya sh. Bilioni 9.3 zilikusanywa na Serikali kutokana na tozo,faini na mauzo ya mazao ya uvuvi yaliyotaifishwa na Serikali.
Pia mauzo ya sangara nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 26,000 mwaka 2016/2017 na kufikia tani 26,700 katika mwaka 2017/2018,urahisi wa upatikanaji wa samaki wenye ukubwa unaokubalika kisheria, kuongezeka kwa ukubwa wa samaki wanaochakatwa viwandani huku mahitaji ya vyavu halali yameongezeka  na wananchi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono vita ya uvuvi haramu kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu.
Aidha Waziri Mpina alisema katika operesheni hiyo walibainika baadhi ya watendaji wa Serikali,Madiwani,Wenyeviti wa Halmshauri,Wabunge wakihusika kufadhili uvuvi haramu na kwamba tayari majina ya viongozi hao yameshawasilishwa kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi huku kwa upande wa watumishi wa wizara hiyo 12 wakisimamishwa kazi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais(TAMISEMI), Suleiman Jafo aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kuwabainisha kwa majina watumishi wote wa Serikali ngazi ya Serikali za Mitaa waliohusika kushiriki ama kufadhili uvuvi haramu na kuyafikisha ofisini kwake ili aweze kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Waziri Jafo alisema suala la ulinzi wa rasilimali za Taifa ni watanzania wote hivyo kama kuna baadhi ya watumishi wanashiriki hujuma katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya tano hawatapata nafasi kwani uvuvi ni miongoni mwa sekta inayotegemewa hasa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
‘Kama Taifa tuna kila sababu ya kuungana katika mapambano ya uvuvi haramu hasa katika kipindi hiki cha uchumi wa viwanda,ofisi yangu haitasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu kwa watumishi wote watakaobainika kutajwa kushiriki uvuvi haramu”alisema Jafo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge,Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa alimtaka Waziri Jafo kusimamia kikamilifu agizo lake kwani baadhi ya watendaji walioko chini ya wizara yake ndio wafadhili wakubwa wa mtandao wa uvuvi haramu na kukwamisha juhudi za Serikali za kumaliza tatizo hilo.
Mgimwa alisema mapato mengi ya uvuvi yalikuwa yanaishia mifukoni mwa watu wachache lakini kwa juhudi na ubunifu mpya uliofanywa na Waziri Mpina na wizara yake umewezesha kukusanya sh.  bilioni 9.3 katika kipindi cha miezi sita na fedha hizo zimeingia mfuko mkuu wa Taifa na kwenda kusaidia kwenye ununuzi wa ndege,ujenzi wa reli, umeme,maji,elimu bure na uboreshaji wa sekta ya afya.
 Kamanda Mkuu wa Operesheni Sangara 2018, Emanuel Bulai alisema operesheni hiyo imebaini kuwepo uvunjifu mkubwa wa sheria ikiwemo matumizi ya zana haramu za uvuvi, utoroshaji mkubwa wa mazao ya uvuvi na raia wa kigeni kuingia nchini na kufanya biashara ya samaki na mazao na yake bila kufuata Sheria za nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.