Habari za Punde

200 Kukimbiza Baiskeli Jumapili hii

Na.Mwunyimvua Nzuki, Zanzibar.
Zaidi ya washiriki 200 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki mbio za baiskeli za ‘North Zanzibar Sportive 2018’ zitakazofanyika Agosti 19 mwaka huu katika kijiji cha Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mkurugenzi wa mbio hizo Abrahman Hussein kutoka klabu ya mbio za baiskeli ya Dar es salam ijulikanayo 'DARVELO' alisema resi hizo zina lengo kuibua na kuviendeleza vipaji vya wakimbizaji baskeli na kuisaidia jamii ya maeneo ya mkoa huo katika sekta mbali mbali za kijamii.

Alisema mbio hizo zitakazoanzia na kumalizikia katika kijiji hicho, zitawashirikisha waendesha baskeli wanawake na wanaume katika umbali wa kilometa 50 na 100 zitasaidia kupatikana kwa fedha zitakazotumika katika ujenzi wa Skuli ya Chekechea ya kijiji cha Nungwi.

Hussein alieleza kuwa mashindano hayo yatasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza pato la taifa kutokana na maombi ya washiriki kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Afrika Kusini na nchi nyengine za Ulaya.

“Hatukulenga kupata kipato bali kuongeza umaarufu wa hii resi hizi tunazozifanya kwa mara ya pili na kuvutia watalii ambao watasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wetu na kukuza uchumi wan chi yetu”, alieleza Abdulrahman.

Aidha Mkurugenzi huyo alieleza kuwa katika mbio hizo kutakuwa na timu maalum ya wakimbiza baskeli kutoka mwanza inayofadhiliwa na Darvelo Cycling Club ya Dar es salam ili kuwahamasisha wanawake wa Zanzibar kushiriki katika mchezo wa mbio za baiskeli.

Aliwapongeza wadhamini mbali mbali waliojitokeza kudhamini mashindano hayo na kueleza kuwa ufadhili wao utaongeza ushindani miongoni mwa wananmichezo hao ambapo mshindi wa kwanza, wa pili na watatu watapatiwa pamoja na zawadi nyengine, watapatiwa zawadi za fedha taslim.

Kwa upande wake Msemaji wa chama cha Baskeli Zanzibar (CHABAZA) Saleh Kijiba alisema mashindano hayo mbali ya wageni kutoka nje yatahusisha wachezaji kutoka Unguja na Pemba wakiwemo vijana wa chini ya miaka 20 ambao watakimbia kwa umbali wa kilomita 50 pekee.

Msemaji huyo aliwashukuru waandaaji na wadhamini wa mbio hizo ambazo alisema zinaunga mkono juhudi za chama chake katika kuuendeleza mchezo huo ambao umeonekana kudorora katika miaka ya hivi karibuni.

“Mchezo huu una gharama na mara nyingi tumekuwa tukifanya mashindano madogo madogo yanayoshirikisha wakiambiaji wa ndani tuu ila kupitia mbio hizi wakimbiaji wetu watapata kujifunza na kuona changamoto zitakazoimarisha viwango vyao”, alieleza kijiba na kuwataka wadhamini wengine kujitokeza kudhamini shughuli za chama chake.


Mashindano hayo yanatarajiwa kuaanza asubuhi kesho (agosti 19) katika kijiji cha Nungwi kupitia Kiwengwa, Pwani Mchangani hadi Pongwe mbio za kilomita 100 kisha kurejea tena Nungwi kwa kupitia njia hiyo hiyo.

Mbali ya zawadi ya medali na vyeti wakatazopatiwa washiriki wote, washindi watatu wa mwanzo watapatiwa zawadi za fedha taslimu kuanzia shilingi Milioni 1, 500,000 na  na 300,000 kwa Wanaume na Wanawake zilizotolewa na wadhamini wa mashindano hayo ambao ni Mfuko wa hifadhi ya jamii zanzibar (ZSSF), Darvelo cycling club na kampuni ya inayojishughulisha na utunzaji wa mazingira na uoto wa asili ya Kilombero Mitiki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.