Habari za Punde

DKT. KIJAJI AWATAKA WANAFANYABISHARA KIGOMA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIBISHARA NA NCHI JIRANI ZA BURUNDI NA RWANDA

 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati), akiwaasa wafanyabiashara wa Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma (hawapo pichani) kutumia fursa zilizopo katika nchi jirani ikiwemo Burundi kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani ili kukuza uchumi wa Wilaya hiyo, alipofanya mkutano na Wafanyabiashara hao Wilayani hapo, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala, na kulia ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kakonko Bw. Kadudusi Bunabuna.
 Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma, Kanali Hosea Ndagala, akiwataka wafanyabiashara wa Wilaya hiyo kuzingatia taratibu za kibiashara na kuhakikisha wanajipanga kuanzisha viwanda vidogo ili kuongeza thamani ya bidhaa wanazouza nje ya nchi, wakati wa mkutano kati ya Wafanyabiashara wa Wilaya hiyo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa pili kushoto).
 Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA anaye shughulikia mapato ya ndani Bw. Elijah Mwandumbya, akifafanua masuala mbalimbali ya kikodi kwa wafanyabiashara wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipokutana na wafanyabiashara hao kujadili fursa na changamoto wanazopata.
 Wafanyabiashara Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma wakimsikiliza kwa Makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani), alipofanya mkutano ulioangazia namna bora ya kuboresha mazingira ya kibiashara katika Wilaya hiyo.
 Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango walioko kwenye msafara wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakifuatilia mkutano kati ya Serikali na wafanyabiashara wa wilaa ya Kakonko mkoani Kigoma.
Mfanyabiashara wa Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma Bw. Musa Ndiliwe, akieleza kuhusu kuimarishwa kwa mazingira bora ya kibiashara katika Soko la Ujirani mwema kati ya yao na wenzao wa Nchini Burundi kwa lengo la kukuza biashara, wakati wa mkutano kati ya wafanyabiashara hao na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Wilayani hapo.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

Na.Benny Mwaipaja, Kakonko, Kigoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, 
amewashauri wakazi wa Wilaya ya Kakongo na mkoa wa 
Kigoma kwa ujumla kuchangamkia fursa za biashara kati ya 
mkoa huo na nchi jirani za Rwanda na Burundi kwa kuuza 
mazao ya kilimo  yaliyochakatwa likiwemo zao la muhogo ili 
waweze kunufaika na biashara hiyo ya mipakani.
Dkt. Kijaji ametoa rai hiyo mjini Kakonko baada ya kukutana 
na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa wilaya 
hiyo,mkutano uliolenga kujadili fursa na changamoto za 
ufanyaji biashara katika eneo hilo yakiwemo masuala ya 
kikodi.
"Nakuomba Mkuu wa Wialaya ya Kakonko uwakutanishe na 
kuwaunganisha wafanyabiashara hawa ambao nafurahi 
wengi wao ni vijana ili waandae andiko la namna ya 
kununua mashine za kuongeza thamani ya mazao ili wauze 
nje yakiwa yamechakatwa badala ya mfumo wa sasa ambao 
wanauza mazao ghafi nje ya nchi na hivyo kupata hasara" 
alisisitiza Dkt. Kijaji
Awali, wafanyabiashara wa Kakonko walimweleza Naibu 
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu kijaji, 
aliyeambatana na Kamishna wa Mapato ya ndani wa 
Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Elijah 
Mwandumbya, kwamba, bei ya zao la muhogo imeshuka 
kutoka shilingi 600 kwa kilo katika msimu uliopita hadi 
kufikia shilingi 150, hali iliyowasababishia wakulima 
maumivu makubwa.
"Wafanyabiashara wanaonunua mazao yetu kutoka Burundi 
ni watu wa kati kwa maana ya madalali ambao wananunua 
mazao yetu kwa bei nafuu na kuyapeleka n hini kwao ambako 
huyachakata na kuyauza kwa bei kubwa nchini mwao na 
nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo, 
hivyo tunaiomba Serikali itupatie mikopo kupitia Benki ys 
Kilimo ili tusnzishe viwanda vya kuchakata mazao yetu" 
alieleza mfanya biashara Dkt. Brighton Gwamagobe
Akizungumza katika Mkutano huo, Kamishna wa TRA wa 
Mapato ya Ndani Bw. Elijah Mwandumbya, pamoja na kutoa 
ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kodi, ametoa wito kwa 
wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha 
Serikali kupata fedha za kuhudumia jamii ikiwemo ujenzi wa 
miundombinu ya barabara, afya, maji na mambo mengine 
kadha wa kadha.
Alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya 
ukusanyaji kodi na kutatua kero mbalimbali za 
wafanyabishara pamoja na kuongeza wigo wa walipa kodi ili 
kuimarisha mapato ya nchi
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, yuko 
katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma ambapo anakagua 
miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatiwa fedha na 
Serikali pamoja na kuzungumza na jumuiya ya 
wafanyabiashara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.