Na Salum Vuai, ZANZIBAR
MABARAZA ya Manispaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kushirikiana
na Mamlaka ya Mazingira Zanzibar, wanaandaa mkakati maalumu wa ukusanyaji taka
ili kuuweka mji katika usafi wa kudumu.
Mabaraza hayo ni ya manispaa za Mjini pamoja na Magharibi ‘A’ na
‘B’.
Tayari mabaraza hayo yameandaa kanuni ndogondogo zinazolenga
kuchukua nafasi ya zile za zamani, ambazo zinatoa miongozo juu ya namna ya
kuimarisha usafi kwenye manispaa hizo.
Katika kikao cha kupitia kanuni hizo kilichofanyika mwishoni mwa
wiki mjini Zanzibar, wajumbe walitoa maoni mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha
kanuni hizo zinatekelezeka.
Awali, akifungua kikao hicho, Sheha Mjaja Juma ambaye ni
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA), alisema
kumekuwa na tatizo kubwa la usimamizi wa taka ndani ya manispaa hizo.
Alifahamisha kuwa, tatizo hilo linasababishwa na mambo mbalimbali,
ikiwemo kutokuwepo kwa kanuni au sheria ndogo ndogo zinazotoa usimamizi mzuri
wa kupunguza tatizo la utupaji taka ovyo.
“Baadhi ya watu wanapokwenda kutupa taka hawatumii makontena
maalumu yaliyowekwa kwa ajili hiyo, na badala yake huzimwaga ovyo ardhini hata
kama kontena halikujaa, na hata katika misingi ya maji ya mvua au machafu na
kusababisha kuziba,” alifahamisha.
Mkurugenzi huyo pia alisema kanuni hizo pia zinalenga kuwadhibiti
watu waache kutupa taka majiani, kama vile mabaki ya vyakula na matunda, chupa
tupu hasa wanapokuwa ndani ya magari.
Kwa hivyo, alisema kuundwa kwa kanuni hizo kunajielekeza katika
kutoa majibu ya matatizo hayo, ili manispaa hizo na Zanzibar kwa jumla ziwe
mfano bora wa usafi Afrika Mashariki na duniani kote.
Alitoa mfano wa miji ya Moshi na Arusha ambayo alisema imefanikiwa
katika jambo hilo kutokana na kuwa na kanuni bora.
“Tuipitie kwa kina na kuichangia rasimu hii, ili baadae
tuwe na kanuni itakayokuwa rahisi kwetu ili hapo baadae kusiwepo tena mtu
anayetupa taka kwenye misingi, magofu au katika ukanda wa pwani na mito, wala
mtu anayesubiri mvua inyeshe ili atupe taka zake,” alieleza
Mjaja.
Akizungumzia kanuni hiyo inayohusu uhifadhi wa taka, Mwanasheria
wa Manispaa ya Magharibi ‘A’ Zainab Makame Mussa, alikiri kuwa ukusanyaji wa
taka ni tatizo sugu linaloiumiza kichwa manispaa yake.
Alieleza matarajio yake, kuwa kupatikana kwa kanuni mpya ambayo
itawahusisha wananchi na taasisi mbalimbali ambazo ndio wazalishaji wakubwa wa
taka, kutaleta ufumbuzi wa kuzihifadhi taka ili zisisambae ovyo na kupoteza
haiba ya miji.
Aidha alisema, ili kanuni hiyo iwe na nguvu na iweze kutekelezeka,
ni lazima kutolewe elimu kwa wananchi, na kuwepo ushirikiano kati yao na
manispaa, katika jitihada za kuimarisha huduma za miji na kuiondoshea Zanzibar
aibu ya uchafu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mjini Aboud Hassan
Serenge, alisema suala la kuuweka mji usafi na utunzaji mazingira kwa jumla,
sio la manispaa au serikali pekee, bali ni la kila mwananchi.
Alisema kanuni inayojadiliwa ili iweze kufanywa sheria ndogo,
itakuwa tiba ya tatizo la uchafu, ambapo kutakuwa na uchambuzi wa taka za aina
mbalimbali, utakaonzzia katika nyumba za wakaazi kabla hazijakusanywa na watu
watakaopewa jukumu hilo.
Mpango huo unaendeshwa chini ya ushauri na usimamizi wa kituo cha
sayansi na mazingira kutoka India, ambapo Naibu Meneja wake Dkt. Sonia Devi
Henam alishiriki kikao hicho kuzipitia kanuni hizo na kutoa mapendekezo
kadhaa.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
25 AGOSTI, 2018
No comments:
Post a Comment