STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Jakarta,
Indonesia 02.08.2018

RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewakaribisha wafanyabiashara
na wawekezaji wa nchini Indonesia kuja kufanyabiashara na kuwekeza Zanzibar
kutokana na fursa mbali mbali zilizopo.
Dk. Shein aliyasema hayo
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Wafanyabiashara na
Wenyeviwanda ya Indonesia (KADIN), huko katika ukumbi wa ofisi ya Jumuiya hiyo
iliyopo mjini Jakarta Indonesia.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuna sababu mbali mbali ambazo wawekezaji wanaweza
kuichagua Zanzibar kama ni sehemu pekee ya kuekeza ikiwa ni pamoja na kuwepo
mazingira mazuri ya uwekezaji yaliowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja
na kuwa na soko kubwa la kibiashara linalojumuisha nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, Rais Dk. Shein
aliwaeleza wanajumuiya hiyo kuwa miongoni mwa sababu kubwa ambayo Zanzibar
pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia ni kuwepo kwa amani,
usalama na utulivu mkubwa nchini Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
Dk. Shein alieleza kuwa
uchumi wa Zanzibar umekuwa ukiimarika ambapo mnamo mwaka 2017 ulifikia asilimia
7.5 ikilinganishwa na mwaka 2016 ambapo ulifikia asilimia 6.8 huku akieleza
azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka
2020.
“Tupo hapa kwa ajili ya
kukukaribisheni mje Zanzibar kufanya biashara na kuwekeza katika sekta mbali
mbali…..kihistoria Zanzibar ilikuwa ni kituo maalum cha biashara ndani na nje
ya Bara la Afrika”,alisema Dk. Shein.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa kunaweza kuimarishwa uhusiano madhubuti kati ya taasisi zinazomilikiwa na
Serikali zote mbili katika maeneo ya biashara na uendelezaji wa miundombinu
ambapo uhusiano kama huo pia, unaweza kuanzishwa kati ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na kampuni mbali mbali za binafsi za nchini Indonesia.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa kumekuwa na mahusiano ya karibu na ya muda mrefu kati
ya Zanzibar na Indonesia na kusema kuwa tokea mwanzoni mwa miaka ya 50
Indonesia ilianza urafiki na nchi nyingi katika bara la Afrika ikiwemo
Tanzania.
Aliongeza kuwa uhusiano
huo, uliimarika zaidi mara baada ya Mkutano wa Bandung uliofanyika mwaka 1955 mjini
Jakarta Indonesia ambao ulikuwa muhimu na kuweza kuongeza chachu katika nchi
zisizofungamana na upande wowote na hatimae mnamo mwaka 1964 muungano wa nchi
hizo uliimarishwa katika kkutano uliofanyika huko Bilgrade, mjini Yugoslavia.
Akitangaza fursa za
uwekezaji zilizopo Zanzibar katika sekta mbali mbali za uchumi, katika mkutano
huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar
(ZIPA) Salum Khamis Nassor alieleza kuwa Zanzibar ni eneo la pekee lenye
matumaini katika kuekeza sekta kadhaa za uchumi.
Akizitaja sekta hizo alisema
ni sekta ya utalii, kilimo, uvuvi, biashara, nishati, usafiri na usafirishaji
pamoja na sekta ya uendeshaji wa miji mipya.
Mkurugenzi huyo wa (ZIPA), akizielezea
fursa hizo alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi
kubwa katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na biashara ili
kuwawezesha wawekezaji na
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara kwa faida kwa manufaa
yao na ya nchi kwa jumla.
Aliongeza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kusimamia mazingira ya uwekezaji kwa kuona
kwamba wawekezaji wanashirikiana vyema na Serikali katika kuimarisha uchumi ikiwa
ni pamoja na kuanzisha ajira kwa vijana.
Nao
viongozi na Wanajumuiya ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda ya Indonesia
(KADIN), walileza mafanikio waliyoyapata katika Jumuiya yao hiyo na kuahidi
kuitumia vyema fursa ya kuja kuekeza na kufanya biashara Zanzibar ikiwa ni
kuitikia wito wa Rais Dk. Shein wa kuwataka
kuekeza Zanzibar.
Mara baada ya mkutano
huo, Rais Dk. Shein alikutana na uongozi wa Kampuni ya mafuta na gesi ya Pertamina
ya nchini humo ambao ulimueleza mafanikio iliyoyapata katika shughuli zake kwenye
sekta hizo na kueleza kuwa tayari imeshaanza kufanya shughuli zake huko Tanzania Bara katika maeneo ya Lindi na Mafia.
Hivyo, kutokana na mkutano
huo Kampuni hiyo ilivutika na kuahidi kuitumia fursa hiyo ili kuangalia
uwezekano wa kuanzisha mashirikiano na kuja kuekeza Zanzibar hasa ikizingatia
uzoefu na mafanikio iliyoyapata katika sekta hizo.
Mapema katika ukumbi wa
Hoteli ya Borobudur, Rais Dk. Shein alikuna na kufanya mazungumzo na Meya wa Jimbo
la Gorontalo, Profesa Nelson Pomalingo ambapo Rais Dk. Shein na kiongozi huyo
walieleza haja ya kuimaisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Indonesia katika
sekta ya kilimo hasa kilimo cha minazi.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo historia ya mafanukio iliyokuwa nayo
Zanzibar katika kilimo cha zao hilo ambalo hivi sasa limekuwa adimu kutokana na
sababu mbali mbali zikiwemo athari za kimaumbile na zile zinazofanywa na
binaadamu ikiwemo kuikata kwa makusudi licha ya kuwepo kwa maradhi
yanayoiathiri minazi kwa hivi sasa.
Nae kiongozi huyo wa
Jimbo la Gorontala alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Indonesia na Zanzibar ni
maeneo yaliyofanana kijiografia hivyo kushirikiana katika sekta ya kilimo kuna
weza kuongeza tija na hatimae kuleta mafanikio kwa pande zote mbili.
Hata hivyo, kiongozi huyo
alimueleza Rais Dk. Shein kuwa katika kilimo cha minazi licha ya kuwa
changamoto zilizopo katika kilimo hicho kwa upande wa Indonesia zinafanana na
zile za Zanzibar lakini hata hivyo nchi hiyo imeweza kupata mafanikio makubwa
katika kilimo cha minazi.
Katika mazungumzo hayo,
kiongozi huyo wa Gorontalo aliahidi kuanzisha na kuendeleza uhusiano na
ushirikiano uliopo na kusisitiza kuwa atahakikisha mashirikiano yanafanyika
katika kuhakikisha kilimo hicho kinaimarika katika visiwa vya Zanzibar.
Wakati huo huo,
viongozi na watendaji wakuu wa Serikali walioambatana na Rais Dk. Shein katika
ziara yake hiyo walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na watendaji
wenzao wa nchini Indonesia katika ukumbi wa hoteli ya Borobudur.
Katika mikutano hiyo
iliyofanyika kwa nyakati tofauti, viongozi na watendaji hao walieleza haja ya
kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja sambamba na kubadilishana uzoefu na utaalamu katika
kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiweko sekta ya utalii, uvuvi na
kilimo.
Pamoja na hayo, mazungumzo
hayo yalionesha pande zote mbili kukubaliana na hoja ya kuimarisha ushirikiano
katika sekta hizo ambazo zimekuwa ni sekta muhimu kwa nchi zote mbili na
zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na kuchangia pato la
Taifa.
Rajab
Mkasaba, Jakarta, Indonesia
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment