Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na mgeni wake Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Balozi Dan Kazungu, alipofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha na kufanya mazungumzo leo
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Kenya
na Zanzibar zinauhusiano wa kihistoria hivyo ushirikiano katika sekta ya
biashara kati ya pande mbili hizo utakuza uchumi na kuuendeleza udugu wa damu uliopo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa Kenya katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dan Kazungu aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Kazungu kuwa Zanzibar na Kenya zina uhusiano
na ushirikiano wa kihistoria hasa katika sekta ya biashara ambapo Zanzibar
ilikuwa ndio kitovu kikuu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki tokea
karne ya 19.
Dk. Shein alieleza
kuwa kuna kila sababu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na
Kenya katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ambapo kwa upande wa
sekta ya biashara ndio sekta pekee yenye historia kati ya pande mbili hizo.
Alisema kuwa wananchi
wa Kenya na Zanzibar wana udugu wa damu na kutokana na matukio kadhaa ya
kihistoria yakiwemo Watawala waliozitawala nchi hizo yamejenga ukaribu mkubwa
na kumpelekea Dk. Shein kusisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein aliunga mkono wazo la Balozi huyo wa Kenya la kuwekwa utaratibu
maalum wa kuzidisha ushirikiano huo katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya
biashara kati ya Kenya na Zanzibar kwa lengo la kukuza uchumi na kuinua ustawi
wa maisha ya wananchi wa pande mbili hizo.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuipongeza Kenya kwa kununua karafuu za Zanzibar hivi sasa
hatua ambayo imesaidia katika kupambana na vita ya biashara ya magendo ya
karafuu iliyokuwa ikiendeshwa na wabadhirifu wa uchumi hapo siku za nyuma.
Akizungumza kuhusu
sekta ya utalii, Rais Dk. Shein alisema kuwa kuna haja pia, ya kuimarisha
ushirikiano kati ya Zanzibar na Kenya katika kuendeleza sekta hiyo hasa
ikizingatiwa kuwa Kenya imepiga hatua katika sekta ya utalii ikilinganishwa na
Zanzibar.
Dk. Shein aliongeza
kuwa kutokana na kuwepo kwa tamaduni zilizofanana kati ya Kenya na Zanzibar, ni
vyema pia, katika upande huo kukawepo mashirikiano kama ilivyokuwa hapo siku za
nyuma sambamba na kuwepo mashirikiano ya miji ya Unguja na Mombasa.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa ushirikiano katika sekta ya uvuvi kati ya
Kenya na Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na kupambana na
umasikini hasa ikizingatiwa kuwa pande mbili hizo zimepitiwa na Bahari ya Hindi
na Zanzibar imezungukwa na Bahari hiyo.
Alisisitiza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi za makusudi katika
kuhakikisha sekta ya uvuvi hasa ule wa kisasa ukiwemo wa bahari kuu inaimarika
kwa lengo la kukuza kipato cha wavuvi na kuimarisha uchumi wa Zanzibar kupitia
sekta hiyo.
Nae Balozi wa Kenya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dan Kazungu alimpa Rais Dk. Shein salamu za Rais wa Kenya Uhuru Kenyata na
kumueleza azma ya kiongozi huyo kukuza uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo
kati ya Zanzibar na Kenya.
Balozi Kazungu
alimueleza Rais Dk. Shein hamu na nia ya Kenya kukuza uhusiano na ushirikiano
na Zanzibar katika sekta ya biashara kwa kutambua sifa na historia kubwa
iliyonayo Zanzibar katika sekta hiyo.
Kiongozi huyo,
alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Kenya ina mambo mengi ya kushirikiana na
Zanzibar katika sekta ya biashara na iko tayari kuanzisha taratibu
zitakazosaidia zaidi kuwepo kwa ushirikiano huo hasa ikizingatiwa kuwa lengo la
viongozi wote wa Afrika ni kushirikiana
katika kuendeleza mataifa yao na watu wake.
Balozi Kazungu
alieleza kuwa mbali ya kuwepo kwa ushirikiano katika sekta ya biashara pia, ipo
haja ya ushirikino katika sekta ya uvuvi ambapo katika kuipa kipaumbele sekta
hiyo, Balozi huyo alisema kuwa Kenya kwa kushirikiana na Canada hivi karibuni
imeandaa mkutano nchini Kenya utakaozungumzia juu ya uchumi wa Bahari “Blue
economy” ambapo alisisitiza kuwa ushiriki wa Zanzibar katika mkutano huo una umuhimu mkubwa.
Aliongeza kuwa katika mkutano
huo miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na kuangalia rasilimali za
bahari zinatumika vipi katika kusaida kukuza uchumi.
Pamoja na hayo, Balozi
huyo alisisitiza kuwa ushirikiano katika sekta ya utalii una umhimu mkubwa kati
ya Kenya na Zanzibar hasa ikizingatiwa kila uchao Zanzibar imekuwa ikiimarisha
miundombinu yake ya kiuchumi ili kukuza sekta ya utalii ikiwemo ujenzi wa jengo
jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume.
Aidha, alieleza kuwa
kutokana na sifa nyingi za kitalii zilizopo Zanzibar watalii wengi wanaokwenda
Kenya wakiwemo wale wanaofika miji mbali mbali ya Kenya ukiwemo mji wa Malindi uliopo Kenya huwa na hamu ya kuja
kuitembelea na Zanzibar.
Sambamba na hayo,
Balozi huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Timu ya Taifa ya Zanzibar “Zanzibar
Heroes” kwa kandanda safi iliyoonesha katika fainali ya ubingwa wa Vyama vya
Soka Afrika Mashariki na Kati “CECAFA”, kati ya timu hiyo na timu ya Taifa ya
Kenya ambapo kwa maelezo ya Balozi huyo timu ya Kenya ilipata ushindi kwa tabu
pamoja na kujawa na hofu kubwa kutokana na kandanda safi lililooneshwa na
vijana wa ‘Zanzibar Heroes’.
Balozi huyo pia, aliipongeza
Zanzibar kwa kuendelea kuhifadhi na kulinda mazingira ya Zanzibar na kutoa
zawadi ya picha aliyomkabidhi Rais Dk. Shein ya marehemu Profesa Wangari
Maathai wa Kenya ambaye alipata tunzo ya amani ya Nobel mwaka 2014 kufuatia
juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment