Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba akifungua mkutano wa wadau
wa Mazingira Jijini Arusha. Mkutano huo
umeshirikisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali na zile zisizo za kiserikali
kwa lengo la kujadili changamoto ya mimea vamizi yenye athari hapa nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba akifuatilia mawasilisho ya
mimea vamizi kutoka kwa Mtaalamu wa COSTECH (hayupo pichani). Kulia ni Mhe.
Nape Nnauye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili.
Sehemu ya Washiriki wa
Mkutano wa wadau wa kujadili changamoto za mimea vamizi. Mkutano umefanyika
katika ukumbi wa AICC jijini Arusha. Mstari wa mbele katika picha ni
waheshimiwa wabunge waliohudhuria.
Na.Lulu Mussa.
Katika jitahada za
kupambana na mimea vamizi nchini ambayo kwa kiasi kikubwa ina athari kwa uchumi
wa Nchi yetu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.
January Makamba hii leo amewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali, asasi za
kiserikali na zisizo za kiserikali, Wenyeviti wa Kamati za Bunge za Ardhi na
Maliasili, Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Kilimo, Mifugo
na Maji ili kwa pamoja waweza kujadili namna bora ya kupambana na mimea vamizi
ambayo imetapakaa kwa kasi katika maeneo mbalimbali hapa nchi.
“Pamoja na kwamba viumbe vamizi wageni ni janga
kwa makazi asilia ya viumbe, lakini hatujalishughulikia kikamilifu, kuweka
mikakati madhubuti ya kuzuia na kukabiliana na viumbe hivi.
Kwa muktadha huo,
leo tumepata fursa adimu na adhimu kutafakari kuhusu hali ilivyo kwa sasa,
changamoto zilizopo na kujadili mikakati madhubuti ya kukabiliana na tatizo la
viumbe vamizi wageni hapa nchini” Makamba alisisitiza.
Wadau waliohudhuria
mkutano huo wameitaka Serikali kuongeza nguvu katika kupambana na tatizo hilo
kwa kuibua miradi mbalimbali kote nchini ili kwa pamoja kuwa na mkakati wa kitaifa
wa kupambana na hali hiyo ambayo ina athari kubwa kiutalii.
Mhe. Innocent
Bashungwa Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na
Mazingira amesema kuwa suala kubwa ni kuuongeza bajeti kila mwaka katika sekta
ya usimamizi wa mazingira pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Mazingira
Nae Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Murad Sadick amesema
kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais iunde kikosi kazi cha kusimamia jambo husika na
kulipa kipaumbele kama hatua za haraka, ikiwa ni pamoja na kuitaka Serikali
kutenga fedha nyingi katika suala la utafiti ambao utasaidia kuja na suluhu
katika changamoto hiyo.
Wakati huo huo, Mwenyekiti
wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mahmoud Mgimwa amesema kuwa kwa
uwakilishi wao wa Kamati hizo tatu, jumla ya wabunge 75 kutoka Kamati wanazo ziongoza
wameshafahamu tatizo hilo.
“Sisi tuko tayari kuunga mkono upatikanaji wa fedha
ili kuendesha tafiti mbalimbali, kama hatua za dharura na kuhakikisha Sheria
iliyounda Mamlaka ya Ngorongoro inapitiwa upya ikiwa ni pamoja na kutokujenga
majengo ya kudumu ili kutoathiri ikolojia ya eneo hilo.”
Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Maliasili na Utalii Mhe. Nape Nnauye amesema Kamati yake ya
Maliasili na Utalii na Bunge kwa ujumla watachukua hatua kama janga la Kitaifa,
“Tunazungumzia uhai wetu sisi, athari za mimea na wanyama zinaathiri binadamu,
hivyo lazima tupambane kwa nguvu zote kutokomeza hili jambo, madhara yake ni
makubwa kwetu sisi binadamu”
Mhe. Nnauye
amewataka watafiti kutumia uzoefu kutoka nchi nyingine kuleta uhalisia katika nchi
yetu na kuondoa dhana potofu ya kuamini kuwa kila tatizo jibu lake ni siasa.
“Nyinyi wasomi, wataalamu andaeni majibu ya matatizo, nashauri kiundwe kikosi
kazi na kuandaa majibu kwa makundi, sera, sheria, kanuni, bajeti, hamasa na
usimamizi” Mhe. Nape alifafanua.
Waziri
Makamba amesema kuwa pamoja na kwamba zipo Sera na Sheria mbalimbali zinazo
simamia udhibiti wa viumbe vamizi wageni nchini ikiwemo sekta za Kilimo,
Misitu, Uvuvi, Wanyamapori, Mifugo na Mazingira na Kanuni za Udhibiti wa Magugu
Maji (2001), lakini suala hili halijapata utatuzi mahiri, hivyo msukumo zaidi
na ushirikiano wa pamoja wa sekta zote katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto
hii unahitajika.
Mhe. Makamba amesema kuwa yeye kama Waziri mwenye
dhamana ya Mazingira anayo mamlaka kupitia sheria ya mazingira kifungu cha 66 3
(a) “Waziri kwa kushauriana na Wizara ya
sekta husika anaweza kutunga kanuni zinazo agiza kutengeneza mikakati. Programu
na mipango ya kitaifa ya hifadhi na matumizi endelevu ya bioanuai”.
Aidha,
kifungu cha 67 2 (f) “Waziri kwa
kushauriana na Wizara ya sekta anaweza kuandaa kanuni zinazoweza kubainisha
ukarabati na urejeshaji mifumo ikolojia iliyoharibiwa na kuendeleza urejeshwaji
wa sipishi zilizoko hatarini, pamoja na mengineyo, kwa kuendeleza na kutekeleza
mipango, mikakati mingine ya usimamizi” .
Mwenyekiti wa Kikao
hicho Waziri Makamba amesema mkutano huo ni mwanzo wa suluhisho la kudumu la
kupata majawabu katika kuratibu utokomezaji wa mimea vamizi.
“Nitaunda kikosi
kazi cha kitaifa ndani ya wiki moja ijayo ili kiweze kushughulikia jambo hili
na kuleta mapendekezo yatakayoleta andiko la kuchukua kama hatua za haraka, kwa
mwezi mmoja” Makamba alisisitiza.
Changamoto ya viumbe vamizi wageni inagusa sekta muhimu kwa uchumi wetu
ikiwemo kilimo, misitu, uvuvi, mifugo, wanyamapori, utalii na hata shughuli za
uchukuzi majini.
No comments:
Post a Comment