Habari za Punde

Wahitimu Darasa la Saba Kunolewa Kambini Siku Tatu Jijini Dar es Salaam.

Na Dotto Mwaibale

Huduma ya kiroho ya Grow in Christ Children Ministry imeandaa kambi ya mafunzo ya siku tatu kwa ajili ya kuwanoa wanafunzi waliohitimu darasa la saba wa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Mratibu wa kambi hiyo Pastor Mercy Sang'enoi (pichani) alisema kambi hiyo itaanza Septemba 10,2018 hadi Septemba 13 na kuwa itafanyika katika Hosteli za Magufuli Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo mada mbalimbali zitatolewa.

Sang'enoi alisema mbali ya mada za kiroho pia watatoa mada zingine mbalimbali zitakazohusu namna ya kumuandaa mwanafunzi huyo kabla ya kuanza masomo yake ya sekondari ikiwa ni njia ya kumjengea uwezo wa kujitambua. 

"Watoto wengi wanao hitimu elimu ya msingi bado umri wao ni mdogo hivyo wanahitaji kuelekezwa mambo muhimu kabla ya kuanza kidato cha kwanza ndio maana tumeona tuweke kambi ya siku tatu ili kuwanoa " alisema Sang'enoi.

Alisema katika kambi hiyo watoa mada watakuwa ni yeye, Mwalimu  Asanterabi Sang'enoi, Msaikolojia Bupe Mwabenga, Mwalimu Apaisaria Minja na Shadrack Mgonja.

Alisema wanafunzi wataohudhuria kambi hiyo kila mmoja atalazimika kuchangia huduma za chakula na mambo mengine ambapo atachangia sh.50,000.

Pastor Sang'enoi aliongeza kuwa huduma hiyo ya Grow in Christ hushirikiana na madhehebu mbalimbali ya kikristo kama Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania 
(KKKT), Anglikana, Moravian, Pentekosti na Kanisa la CCT Chuo Kikuu.

Alisema kuwa wapo tayari kushirikiana mtu na taasisi yoyote yenye kuwiwa kuhudumia watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.