Habari za Punde

Wanaharakati Wanaotetea Haki za Wenye Ulemavu wa Akili Pemba, Watokwa na Machozi Kijana Mwenye Miaka 22 Kufungiwa Ndani.

Na.Abdi Suleiman, PEMBA
WADAU wa Jumuiya kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa akili Kisiwani Pemba (ZAPDD), wanaopinga vitendo vya udhalilishaji kwa walemavu wa akili, wamejikuta wakitokwa na machozi na huzuni ndani yake, baada ya mmoja ya mdau wa Jumuiya hiyo kutoa taarifa juu ya madai ya uwepo wa kijana mwenye miaka 22 kufungiwa chumbani kwa kipindi cha miaka minne.
Huzuni hizo zilitawala wakati mjumbe huyo alipokuwa akitoa taarifa juu ya kijana huyo, kufungiwa chumbani, wakati wakikao cha robo ya tatu cha wadau hao kilichofanyika mjini Chake Chake.
Mdau huyo alisema tukio hilo limetokea maeneo la Kiumbe Mzito Machomanne, Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba njia ya kuelekea Ndugu Kitu.
“Sisi tulipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, wakidai bindi amefungiwa chumbani na kufungwa mnyororo ndipo nilipotafuta wenzangu kufuatilia kwa kina tukio hilo”alisema.
Zuwena Hamad Ali kutoka Dawati la jinsia la Polisi Chake Chake, alisema hali halisi ya mazingira walioyakuta katika chumba ambacho mtoto huyo, anadaiwa kufungia hakiridhishi na hakifai kuishi binaadamu.
“Tulipofika nyumbani kwao huyo binti kwanza tuliomkuta alitudanganya baada ya kumuhoji sana, aliweza kutwambia na tukaenda kumkuta huyo binti ndani lazima uwashe tochi ndio uweze kumuona,”alisema Zuwena.
“Hali halisi tulioikuta ni mbaya sana, humo chumbani tulikuta kuku ana watoto, polo la mkaa, kitanda hakiko hadhiri, giza na tayari binti ameshapiga weupe na tukashauri apelekwe hospitali,”alisema.
Aidha mjumbe huyo aliitaka ZAPDD kushirikiana na wadau wengine, ikiwemo waratibu wa wanawake na watoto Wilaya, watu wa sheria kufunga safari ya kwenda kuonana na familia ya binti huyo, ili kuweza kuokoa maisha yake.
Mwenyekiti wa ZAPDD mkoa wa kaskazini Aziza Alawy Mussa, alisema tukio la kufungiwa ndani binti huyo ni unyama na udhalilishaji mkubwa, jambo ambalo halifai kufumbiwa macho hata mara moja.
“Kumfungia mtu ndani hata kama ni mzima basi utakuwa mgonjwa tu, leo wewe ufungiwe ndani basi itafika muda utakuwa katika hali mbaya,”alisema.
Mdau Amour Rashid Ali, alisema kitendo hicho kilichofanywa na wazazi wake ni kwenda kinyume na haki za biaadamu, kwani hakuna hata haki yake moja binti huyo aliyeipata.
Mjumbe kutoka Mtandao wa Pemba Today Haji Nassor Mohamed, aliwataka wajumbe hao wanapofanya ufuatiliaji kuhakikisha wanatumia vyombo vya habari, ili kuweza kutangaza taarifa zao na jamii kuweza kujuwa.
Hakimu wa mahakama ya Mkoa Chakechake, Khamis Ali Simai, aliishauri ZAPDD kuwa na mtu ambae atakaeweza kushuhulikia kesi za watu wenye ulemavu wa akili zinapofikishwa mahakamani.
Mratib wa mradi wa kuboresha mazingira ya upatikanaji haki kwa watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar Khamis Abdalla Sururu, alisema ipo haja kwa jamii kuendelea kupewa taaluma zaidi kwa jamii
“Haipendezi jamii hii yetu tulionayo ukasikia mtoto anafungiwa ndani miaka minne, huu ni udhalilishaji hili ni jambo ambalo halifai kufanyiwa binaadamu,”alisema.
Hata hivyo aliitaka jamii kuwajali watu wenye ulemavu wa akili na kuwa nao karibu, ili watu hao kuweza kupata haki zao kikamilifu pale zinapovunjwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.