Habari za Punde

Wazazi Wahamasisheni Watoto Wenu Kupenda Kujisomea Vitambu na Magazeti Kupatra Uelewa.

Mwanafunzi akijisoma katika moja ya Maktaba ili kupa upeo zaidi wa masomo yake na kumrahisishia kufanya kazi za darasani kwa kusoma vitabu mbalimbali.
Na.Hanifa Salim -Pemba.
WAZAZI na walezi wanawajibu mkubwa wa kusimamia na kuhamasisha watoto kusoma vitabu, ili kumsaidia kujua kusoma, kuongeza elimu na kumsaidia kuweza kujiamini anapokuwa darasani. 
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Pemba Yussuf Mohamed Ali, wakati alipokua akizungumza na wafanyakazi wa Maktaba, wazazi na wanafunzi katika ukumbi wa Maktaba Kuu Chake Chake, ikiwa ni shamra shamra za siku ya kujua kusoma na kuandika Duniani.
Alisema kuwa iwapo wazazi na walezi watatekeleza hayo na kuyasimamia ipaswavo, watoto wataweza kujengeka katika utaratibu mzuri, kwani watoto wanaojengwa kupitia muongozo huo huwa na utekelezaji mzuri wa kazi.
“Kila kwenye watu wazima watano basi mmoja wao atakua hajui kusoma na kuandika, robo mbili ya watu hawa ni wanawake hizi ndizo takwimu zinavotuonesha, kwaio wanawake ni imani yangu mutaichukua changamoto hii na kuhakikisha, kwamba inaondoka kwetu na vizazi vyetu vijavyo” alisema.
Hata hivyo alisema, vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa na ndio taifa la baadae, bado wamekua na changamoto hiyo ya kutokujua kusoma na kuandika, kwani hali hiyo ni janga linaloikabili dunia kwa sasa, huku ikiwa elimu ndio msingi wa maisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la huduma za Maktaba Zanzibar, Sichana Haji Foum alisema Maktaba zina mchango mkubwa katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma vitabu na machapisho mengine, kwani kusoma ndio chanzo cha kujifunza ujuzi wa aina mbali mbali.
“Si rahisi mzazi kuweza kumiliki vitabu vyote kumnunulia mtoto wake, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kulijua hili, ndipo ikaweza kuanzisha hizi maktaba za jamii, ili kusaidia vijana wetu waweze kupata fursa ya kusoma vitabu” alisema.
Hata hivyo alisema, kusoma vitabu kunaweza kumnyanyua mwanafunzi kielimu, kiuchumi, siasa na kiutamaduni pia na kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Mwanafunzi Rashid Salum Masoud wa Skuli ya Shamiani alisema, usomaji wa vitabu unapelekea ufaulu bora kwa wanafunzi,  upatikanaji wa habari tofauti katika magazeti, ambayo wanayapata kupitia Maktaba na kupata mafunzo mengine mbali mbali, ikiwemo kupiga vita rushwa na utawala bora.
Akitoa neno la shukurani Mjumbe wa bodi wa Shirika la huduma za Maktaba Pemba, Abdulla Omar Masoud, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuhakikisha wanafunzi wanapata muendelezo wa kielimu na kuwasaidia ufaulu bora wa wanafunzi katika mitihani yao.
Mapema mgeni rasmi ambae ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Pemba, katika shamra shamra za siku ya kujua kusoma na kuandika duniani, aliweza kukagua Chumba cha Computer, Adult library, Children Corner, American Corner, Youth library na maonesho ya vitabu katika Maktaba kuu ya Chake Chake, kila ifikapo Sptemba 8 ya kila mwaka, huazimishwa siku kujua kusoma na kuandika duniani, kauli mbiu ya mwaka huu ni “kusoma na kuendeleza ujuzi “.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.