Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Akatisha Ziara Yake Mkoani Dodoma, Aenda Ukerewe *Ni Kutokana na Ajali ya Kivuko cha MV Nyerere.


WAZIR MKUU Kassim Majaliwa amekatisha ziara ya mkoa wa Dodoma na kuelekea Ukerewe Mwanza kuwafariji wananchi waliopatwa na maafa kutokana na ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa na ziara ya kikazi ya siku saba katika mkoa wa Dodoma, ametangaza uamuzi huo leo mchana (Ijumaa, Septemba 21, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chandama, wilayani Chemba ambao walisimamisha msafara wake ili wamweleze kero kubwa ya maji inayowakabili.

“Nimelazimika kukatisha ziara yangu na wala sitaenda Kwa Mtoro ili niende kuwafariji wenzetu waliopatwa na msiba wa kupoteza ndugu zao kutokana na ajali iliyotokea jana usiku. Idadi ya waliopoteza maisha imefikia 91, ni msiba mkubwa kwa Taifa letu,” amesema Waziri Mkuu kwa masikitiko.

Waziri Mkuu alikuwa akitokea kijiji cha Itolwa kata ya Jangalo ambako alikuwa na mkutano wa hadhara, aliwaeleza wananchi wa vijiji vya Itolwa, Mapango na Chandama kwamba Serikali imetenga sh. bilioni 5.6 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji kwenye wilaya hiyo.

Akijibu kero kuhusu ubovu wa barabara, Waziri Mkuu alisema amebaini ukubwa wa tatizo la barabara hiyo yenye urefu wa km.10.3 lakini imetengewa sh. milioni 833 ambazo alisema hazitoshi.

“Mhandisi wa TARURA nenda ukakae na timu yako, inabidi mfanye upya mahesabu yenu kwa sababu barabara hii ni ndefu na ina madaraja mengi lakini pia inapita kwenye vijiji vingi. Wenzenu Kondoa wamepata sh. bilioni saba, sasa hii sh. milioni 800 hata sijui itaanzia wapi,” alisema.

“Barabara hii inapita kwenye vijiji vingi vikubwa na wakazi wa huku ni wengi. Hata kama kwa sasa hatuwezi kuijenga kwa kiwango cha lami, inapaswa ijengwe vizuri kwa kiwango kinachoweza kupitika kwa mwaka mzima,” alisema.

Aliwasisitiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba waache tabia ya kupenda kukaa ofisini na badala yake waende vijijini ili wakawasikilize wananchi na kutatua kero zao.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
IJUMAA, SEPTEMBA 21, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.