Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein Amtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwaza Mhe. John Mongela Kufuatilia Ajali ya Kuzama Kivuko cha MV. Nyerere, Iliozama Ziwa Victoria Mkoani Mwanza.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere iliyotokea katika Ziwa Victoria Mkoa wa Mwanza na kusababisha vifo pamoja na majeruhi.

Dk. Shein alieleza kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya ajali ya kuzama kivuko hicho na kueleza kuwa yeye binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla wamegubikwa na simanzi nzito kufuatia msiba huo mkubwa wa kitaifa.

“Kwa hakika msiba huu umetugusa Watanzania sote, ni msiba wetu kwa sababu waliofikwa na janga hili ni ndugu zetu, Watanzania wenzetu”, ilieleza sehemu ya salamu hizo za rambirambi alizozituma Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa vile ajali ni moja kati ya matukio ambayo mwanaadamu hana budi nayo alimuomba Mwenyezi Mungu azijaalie roho za wale wote waliopoteza maisha zipumzike mahala pema.

Kwa wale ambao kwa nguvu za Mola Muumba wameweza kuokolewa wakiwa hai, alimuomba Mwenyezi Mungu awape nafuu kutokana na msukosuko mkubwa uliowapata ili waweze kurudi katika hali zao za kawaida kiafya na waendelee na shughuli zao za kila siku za kujenga nchi yao.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa wananchi wote wa Tanzania Zanzibar wanaungana na Mkuu wa Mkoa huo, Uongozi wa TEMESA, ndugu jamaa na marafiki wa marehemu na wanusurika wa ajali hiyo katika huzuni kubwa za msiba huo.

“Watanzania tunatakiwa kuendelea kuwa na utulivu, umoja na mshikamano wakati huu ambapo jitihada za kutafuta miili zaidi ya waliopata ajali hiyo zikiendelea”,alieleza Dk. Shein katika taarifa hiyo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka Watanzania kuendelea kuwa na ustahamilivu wakati huu ambapo uchunguzi wa sababu za tukio hilo ukifanyika na bila shaka taarifa kamili zitatolewa hapo baadae.

Rais Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu awape Watanzania wote na wanafamilia nyoyo za subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Ajali ya kuzama kwa kivuko hicho ilitokea katika Ziwa Victoria katika eneo la Ukerewe wakati kilipokuwa katika safari yake ya kutoka Bugorola kwenda kisiwa cha Ukara saa sita mchana hapo jana.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.