Habari za Punde

OCD Kyerwa Atuhumiwa Kusindika Kahawa ya Magendo *Waziri Mkuu Aagizwa Achukuliwe Hatua


Na. Khadija Mussa OWM.                                                                                 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi awachukulie hatua askari polisi wote wa wilaya ya Kyerwa wanaotuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo inayouzwa nchi jirani akiwemo Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, Justin Joseph.

Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Oktoba 7, 2018) baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilaya Kyerwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera. Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameambatana na Mkewe Mama Mary Majaliwa.

“Askari polisi wa wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao wanatuhumiwa kusindikiza kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi ya jirani kupitia njia mbalimbali zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na Omukatoma.”

Waziri Mkuu amesema ni jambo la hatari kama askari Polisi wanasindikiza kahawa inayouzwa kwa magendo, hivyo ameagiza jambo hilo lidhibitiwe haraka.”Marufuku kupeleka kahawa nje ya nchi kwa njia ya magendo na polisi msishiriki katika butura.”

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema kuanzia msimu ujao wa kahawa, minada yote ya kahawa inayozalishwa mkoani Kagera itafanyika ndani ya mkoa huo badala ya kufanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu amesema minada yote ya kahawa ikifanyika mkoani Kagera itawawezesha wakulima kulipwa fedha zao kwa muda mfupi na pia itapunguza makato  yasiyokuwa ya lazima ambayo ni kero kwa wakulima.

“Wanunuzi watafuata kahawa ilipo, utaratibu huu utawawezesha wakulima kulipwa fedha zake kwa wakati. Mnada ukifanyika katika maeneo ya uzalishaji utamuwezesha mkulima kujua bei, tofauti na unavyofanyika Moshi kwani ni rahisi mkulima kuibiwa.”

Waziri Mkuu amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuwaletea maendeleo na kwamba itahakikisha kila mmoja anapata haki yake wakiwemo wakulima ambao watasaidiwa katika kutafutiwa masoko ya mazao yao.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 7, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.