Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Katika Maadhimisho ya Miaka 73 ya UN Ukumbi wa Serena Shangani Zanzibar.

Balozi Seif wa Nne kutoka Kulia akiwa pamoja na Viongozi wa Serikali na Taasisi za Umoja wa Mataifa kwenye maadhimisho ya siku ya Umoja huo kutimia Miaka 73.
Balozi Seif akimpongeza Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana unaofungamana na Umoja wa Mataifa katika kusaidia kUndi hilo {UNA} Bwana Rashid Mohamed baada ya kuwasilisha salamu za Vijana. 
Mratibu wa Mashiriki ya Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bwana Alvaro Rodriguez akitoa salamu za Umoja huo kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa.
Balozi Seif akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika katika Hoteli ya Serena Shangani Mjini Zanzibar akimuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alisema Dunia inaweza kuendelea kubakiwa kuwa salama, yenye Amani na ustawi  endapo Mataifa Wanachama yatazingatia  uzito wa Agenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa iliyojipangia kufikia Mwaka 2030.
Alisema ujenzi wa Uchumi imara unaozingatia uimarishwaji wa Sekta ya Elimu, Afya, ongezeko la fursa za Ajira, sambamba na mikakati ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi ni mambo yatakayowezesha kufanikisha Agenda hiyo muhimu ya Umoja wa Mataifa.
Dr. Ali Mohamed Shein alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa  kutimia Miaka 71 tokea ulipoasisiwa ambayo ilifanyika Hoteli ya Serena Shangani Mjini Zanzibar.
Alisema ushirikiano wa Kimataifa unahitajika baina ya Mataifa Wanachama, Mashirika na Taasisi za Kimataifa katika kuona zinasaidiana Kitaaluma, uzoefu ili kukabiliana na matatizo yanayoikabili Dunia hivi sasa yanayoweza kubakia kuwa historia baada ya mwaka 2030.
Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Umoja wa Mataifa ulioasisiwa mnamo mwaka 1945 ukiunda Taasisi zake mbali mbali likiwemo Baraza la Usalama na Umoja huo umeundwa kwa malengo ya kustawisha haki za Binaadamu ili kuifanya Dunia iwe mahali pazuri kwa kuishi.
Alisema jukumu la Umoja wa Mataifa linaendelea kutekelezwa kwa kiwango kikubwa kutokana na mikakati yake ya kusimamia Maendeleo ya Uchumi  pamoja na kutoa misaada ya kiutu kwa Watu na Familia zilizokumbwa na maafa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe.
“ Umoja wa Mataifa kupitia Mashirika na Taasisi zake imeweza kuokoa  Mamilioni ya Binaadamu waliokumbwa na kadhia tofauti ikiwemo njaa, umaskini sambamba na kuzuia vifo vilivyotokana na maradhi yanayotibika”. Alisema Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar aliwaeleza washiriki wa maadhimisho hayo ya Siku ya Umoja wa Mataifa kwamba Zanzibar  inaendelea kufaidika na miradi mbali ya maendeleo na ustawi wa Jamii iliyoanzishwa kwa msukumo wa Umoja huo kupitia Taasisi na Mashirika yake.
Alisema mpango wa pamoja wa  Ushirikiano Zanzibar ulioanzishwa Mnamo Tarehe 28 Agosti Mwaka 2018 ni moja miongoni mwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na Umoja wa Mataifa kupitia Mashirika yake katika Kuunga mkono jitihada za maendeleo za Nchi Wanachama.
Alisema Mpango huo umeelekeza nguvu zake katika uimarishaji wa huduma za Mama Wajawazito na Watoto, mapambano dhidi vitendo vya  Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto, kuwajengea uwezo wa Kiuchumi Wanawake pamoja na Mpango wa kupunguza umaskini Zanzibar {MKUZA 111}.
Dr. Shein alifahamisha kwamba Mpango huo wa Miaka Minne ulioanzia Mwaka Mwaka huu wa 2018 hadi 2021 Umoja wa Mataifa tayari ulikwishaahidi kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  katika kuona malengo ya Mpango huo yanafanikiwa vyema ili yalete faraja kwa Wananchi walio wengi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kufarajika kutokana na mfumo wa utanuzi wa mikakati unayochukuliwa na Umoja wa Mataifa umewezesha kuyajenga nguvu na uwezo zaidi wa mabadiliko ya Uchumi wa Nchi Wanachama.
Akizungumzia Agenda ya Maendeleo Mapya ya Umoja wa Mataifa iliyoteua wajibu Mpya wa Vijana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema jukumu la Umoja huo limekuja wakati muwafaka katika kuliokoa kundi hilo la Vijana linalokadiriwa kufikia Bilioni 1.8 Duniani hivi sasa.
Dr. Shein alisema Zanzibar kama sehemu ya Dunia kupitia Serikali yake ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukuwa juhudi kubwa katika njia za kuwajengea uwezo Vijana utakaowasaidia kubuni mbinu za miradi inayoweza kuwaunganisha katika masuala ya kujitegemea Kimaisha.
Alisema Idadi ya Vijana wanaomaliza masomo yao ya Sekondari hivi sasa kinaongezeka kila Mwaka na wengi kati yao wakiwa na matumaini ya kutaka kupata ajira katika Taasisi na Mashirika ya Umma ambazo upotikanaji wake ni hafifu.
Dr. Shein alieleza kwamba Sera ya Ajira Zanzibar iliyoainishwa katika Mpango wa kupunguza Umaskini Zanzibar {MKUZA111} imekuwa muongozo wa Serikali  katika jukumu la kubuni mazingira yatakayoongeza fursa za ajira kwa Wananchi wake ikizingatia zaidi Kundi la Vijana.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana kwa pamoja na Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi zake wakiwemo washirika wa Maendeleo ili kuwa na nguvu za pamoja zitakazowekezwa kwa ajili ya fursa zaVijana katika sekta za Teknolojia na  Uwezeshaji Kiuchumi.
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja unaojishughulikia masuala ya Vijana Zanzibar  {UNA}wenye mafungamano na Umoja wa Mataifa Bwana Rashid Mohamed alisema Kundi la Vijana limebarikiwa kuwa na nguvu, Mawazo na uwezo wa kulitumikia Taifa katika misingi ya Kizalendo iwapo litapatiwa fursa ya kushirikishwa.
Rashid alisema uamuzi wa Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi na Mashirikia yake  umezingatia kulipa msukumo kundi la Vijana baada ya kubaini robo ya Wakaazi wa Dunia hii ni wao wanaokadiriwa kufikia Bilioni 1.8.
Alisema yapo mafanikio makubwa yaliyoanza kujitokeza miongoni mwa Jamii kufuatia msukumo wa Vijana kuanza kushirikishwa na hatimae kufanya vyema hata katika kazi za ubunifu, uzalishaji na Ujasiriamali.
Katibu Mkuu wa UNA alieleza kwamba  Mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali, Wizara ya Elimu na Washirika wa Maendeleo yamewezesha  kumuibua Mwanafunzi Kijana Amina kushinda kwenye Maonyesho ya Biashara ya Mwezi Julai Mwaka huu wa 2018.
Alisema Mwanafunzi Amina alichukuwa ushindi wa Kwanza na kupata tuzo ya Shilingi Milioni 3,000,000/- baada ya kutumia Elimu na Maarifa yake yaliyomuwezesha kubuni Mradi wa Umwagiliaji.
Akitoa salamu za Umoja wa Mataifa Mratibu wa Mashirikia ya Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez alisema Taasisi hizo zitaendelea kushirikiana na Serikali Nchini Tanzania  katika kuuelimisha Umma juu ya malengo ya Agenda ya Maendeleo Endelevu { SDG’s} yenye mwaka mmoja sasa katika utekelezaji wake.
Bwan Alvaro alisema  Familia ya Umoja wa Mataifa iliyobeba Mashirika yake mbali mbali yanayofanya kazi chini ya mwamvuli Mmoja yanaendelea kuisaidia Zanzibar katika Mpango wake wa Taifa wa kupunguza Umaskini Zanzibar {MKUZA 111}.
Alisema Umoja wa Mataifa wenye Mataifa Wanachama 193 hautopenda kuendelea kuona udhalilishaji, majanga, Njaa na uvunjaji wa Haki za Bianaadamu unachukuwa nafasi katika kumdhalilisha Binaadamu wa Umoja huo.
Mratibu huyo wa Mashirika ya Umoja wa Mtaifa alifahamisha kwamba Taasisi zake kwa kuungwa mkono na Nchi Swanachama kama Japan naNorway zinaendelea kuunga mkono katika mapambano dhidi ya maradhi yanayowakumba Wajawazito na Watoto.
Katika kuupa nnguvu Mpango wake wa UNDAP 11 unaokwenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Miaka Mitano wa 2016 – 2021 {FYDP 11} unaotekelezwa Nchini Tanzania mafunzo yameanza kutolewa kwa kuwashirikisha zaidi Vijana watakaokuwa na nguvu na uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizowakumba Wazazi wao.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Alitembelea na kuona maonyesho  yaliyoandaliwa na Kundi la Vijana {UNA}lenye mafungamano na Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.