WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo na Katibu Mkuu wa wake Khadija Bakari Juma (Kulia), kwa pamoja wakiwakabidhi wasanii wa kikundi cha taarab asilia ‘Siti And The Band’ shilingi 5,000,000 pamoja na Dola 300 za Kimarekani, walizotunukiwa na wafadhili wawili tafauti kukiunga mkono kikundi hicho baada ya kufanya vizuri kwenye maonesho ya utalii 2018 yaliyoandaliwa hapa Zanzibar. Hafla hiyo ilifanyika leo Oktoba 25, 2018 katika ofisi za wizara Kikwajuni Unguja.
MWIMBAJI na kiongozi wa kikundi cha ‘Siti And The Band’ Amina Omar Juma, akimzawadia fulana maalumu Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo, kuthamini mchango wake na wizara katika kukisaidia kikundi chao kinachoundwa na wasanii wachache vijana.
Picha zote na Salum Vuai, WHUMK.
Na Salum Vuai, WHUMK
BAADA ya kunogesha maonesho ya utalii Zanzibar
yaliyofanyika wiki iliyopita, wasanii wa kikundi cha muziki ‘Siti And The
Band’, leo Oktoba 25, 2018, wamekabidhiwa kitita cha shilingi 5,000,000
sambamba na dola 300 kutoka kwa wafadhili mbalimbali.
Fedha hizo walizoahidiwa siku ya kufungwa kwa
maonesho hayo kwenye hoteli ya Verde iliyoko Mtoni mjini Zanzibar,
zilikabidhiwa kwao na Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit
Kombo katika ukumbi wa wizira hiyo Kikwajuni.
Tunzo ya shilingi 5,000,000 imetolewa na mfadhili
kutoka nchi ya Oman, Ahmed Suleiman, wakati mfadhili mwengine ambaye hakutaka
kutajwa jina, amewatunuku vijana hao mahiri dola 300 za Kimarekani kwa lengo la
kukiendeleza kikundi chao.
Akizungumza katika hafla hiyo fupoi
iliyohudhuriwa pia na watendaji wakuu kadhaa wa wizara yake, Waziri Kombo amewaomba
Wazanzibari na wageni wengineo wanaofika nchini, kuwaunga mkono vijana hao na
wasanii wengine, kama anavyofanya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein katika
kukuza kazi za sanaa.
"Jambo walilolifanya katika tamasha la
utalii ni kubwa na lilileta msisimko kwa wageni wote waliohudhuria, akiwemo Rais
wa Zanzibar, ambaye daima amekuwa mstari wa mbele kuwawekea wasanii mazingira
mazuri ili waweze kujiajiri kupitia Sanaa zao," alisema Waziri huyo.
Alisema kikundi hicho kimekuwa kikifanya vizuri
katika muziki wa taarab kwa kutumia ala za asili kikiendeleza pia kazi za
wasanii wakongwe wa zamani marehemu Sitti Bint Saad na Fatma Baraka ‘Bi.
Kidude’ ambao wakati wa uhai wao, walifanya kazi kubwa kuitangaza Zanzibar
kupitia taarab asilia.
Aliwatakia kila la kheri katika jitihada zao za
kuendeleza muziki, akiahidi kuwasaidia kuwasafishia njia ya kupanda juu zaidi
ya walipo sasa.
“Nakupongezeni sana na ninakuombeni mkatumie fedha
mnazopewa ili zisaidie kukuleteeni maendeleo zaidi na zisigeuke kuwa fitna
zikaleta mfarakano,” alisisitiza Waziri Kombo.
Kiongozi na mwimbaji wa kikundi hicho Amina Omar
Juma, kwa niaba ya wenzake, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri wa Habari na
uongozi wote wa wizara kwa namna walivyojitoa kuwaunga mkono, na wameahidi
kutowaangusha.
Amina, maarufu ‘Sitti Amina’, amewataka wasanii
wenzake kushikamana na kufanya kazi kwa bidii, kwa kubuni njia za kujipaisha
badala ya kujikita kwenye kupikiana majungu, chuki na uhasama miongoni mwao.
Aidha, aliwasihi wajiepushe kuiga wasanii wa nje
hasa katika mavazi na mitindo ya nywele inayokwenda kinyume na maadili ya nchi
yao.
Aliwasisitiza watumie akili na maarifa yao kubuni
vya kwao, huku wakiendeleza sanaa za asili za Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Ikumbukwe kuwa, katika hafla ya kufunga pazia la
maonesho ya utalii usiku wa Oktoba 20, 2018, Rais Dk. Shein alikizawadia
kikundi hicho shilingi 6,000,000 na mke wake Mama Mwamwema, akiitononosha
zawadi hiyo kwa shilingi 4,000,000 na kufanya jumla kuwa shilingi 10,000,000.
No comments:
Post a Comment