Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiondoa kipazia kuashiria kuizindua Klinik ya Mane katika Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja.kushoto Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametangaza rasmi kuwa Hospitali ya Kivunge na
Hospitali ya Makunduchi ambazo zote ni Hospitali za Koteji zifutwe na ziwe Hospitali
za Wilaya kuanzia leo kutokana na sifa, mwelekeo na vigezo ilivyovifikia.
Rais Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika uzinduzi wa Kitengo cha Kinywa na Meno kiliyoko katika huko
Hospital ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja ambayo ilihudhuriwa na viongozi
mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali akiwemo Balozi wa Uturuki nchini
Tanzania Ali Govutogh pamoja na wananchi wa Mkoa huo.
Rais Dk. Shein aliongeza
kuwa kwa huduma zake tayari hospitali hizo ni za Wilaya ambapo tayari jengo
jipya la mama wajawazito na watoto linajengwa jambo ambalo aliielekeza Wizara
kuwa lengo lake ifikapo mwaka 2020 hospitali hizo ziwe za Mkoa kwani tayari
kuna mambo yamekamilika.
Aliwataka Mkuu wa Mkoa
wa Kaskazini Unguja na Waziri wa Afya kuanza kufikiria nafasi ya ili hospitali hiyo izidi kupanuka zaidi na
kuwataka kuzungumza na Wizara nyengine ili watu wa Kaskazini Unguja wapate
hospitali ya kisasa ambayo itakayokuwa inatoa huduma bora na kulaza wagonjwa
pamoja na kutoa huduma bora za meno.
Aliwataka viongozi hao wakutane
na Kamati zao na watendaji wao kutafuta nafasi ya kuipanua Hospitali ya Kivunge
kwani Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeweka lengo kuwa Hospitali hiyo iwe ya Wilaya
ifikapo 2020 kwa kupanda daraja
“Naiagiza Wizara ya Afya
kuwa jina la Hospitali hii ya Koteji ya Kivunge lifutwe na andikeni Hospitali
ya Kivunge ya Wilaya na Hospitali na ile ya Makunduchi andikeni Hopatali ya
Makunduchi ya Wilaya na mwaka 2020 zitakuwa hospitali za Mkoa”,alisisitiza Dk. Shein.
Alisema kuwa Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume yeye ndio msingi wa yote mazuri yanayofanyika na chanzo
cha kutangazwa na huduma bure za afya ambayo yote hayo yalitokana na Mapinduzi ya
Januari 12, 1964 ambayo yalikuwa na lengo la kuondosha dhiki na dhulma kwa mwenye
nacho na asiyekuwa nacho kwani yameleta usawa.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Mapinduzi Daima ina maana ya kuwa yale yote yaliyokuwa si mema na
yanakwenda kinyume na matakwa ya Wazanzibari yataondoshwa, kwani huduma za afya
zilikuwa zikipatikana kwa ubaguzi na hali kwa sekta hiyo na sekta ya elimu
haikuwa nzuri.
Akitoa historia fupi ya
sekta ya afya, Dk. Shein alisema kuwa tarehe 3 Julai mwaka 1964 ndio ulipowekwa
utaratibu mpya wa misingi ya Afya ambapo Marehemu Mzee Aboud Jumbe Mwinyi alipeleka
warka maalum namba 37 katika Baraza la Mapinduzi (BLM) pamoja na mambo mengine
17 ambapo mambo yote yanayofanyika hivi sasa msingi wake ni huo.
Aliongeza kuwa hatua
hiyo ndiyo iliyompekekea Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kutangaza afya bure
siku ya tarehe 3, Machi, 1965 ambapo kwa mujibu wa Rais Dk. Shein Sera hiyo
bado inaendelezwa hadi hivi leo katika uongozi chini ya CCM.
Alisema kuwa kutokana na
changamoto ya ongezeko la idadi ya watu hapa Zanzibar ndio ilipelekea mambo
mengi kutotosha kutokana na kuongezeka mara kumi zaidi katika eneo la Kivunge
jambo ambalo linahitaji kuwepo mpango madhubuti na sio kama Serikali inashindwa
kutoa huduma hizo.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kueleza historia ya afya hapa Zanzibar na kusema kuwa wakati wa ukoloni ambapo
Zanzibar ilikuwa na watu 320,000 na vituo vya afya vilikuwa 32 Unguja na Pemba ambapo
hivi sasa vipo karibu vituo 150 pamoja na hospitali kuwa zenye mambo mengi na
huduma za kisasa licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya watu.
Alisema kuwa Serikali
imejidhatiti kuhakikisha haiba ya hospitali ya Kivunge inabadilika kwa kuongeza
na kupanua huduma zote za afya na kuupongeza Mradi wa Kuimarisha Afya Zanzibar
(HPZ) kwa kujenga kituo hicho“abebwae hujikaza hivyo na sisi tutajikaza ili
kuhakikisha huduma za meno hapa Zanzibar zinaimarika” alisema Dk Shein.
Alisema kuwa kituo hicho
ni mwanzo katika huduma za meno na kuahadi kuwa Serikali itapanua njia zaidi na
kuunga mkono ambapo kwenye Bajeti ya Serikali hapo mwakani itaongeza vifaa na nafasi
katika kitengo hicho cha meno pamoja na huduma nyengine katika hospitali hiyo.
Alisema kuwa kuna
uhusiano mzuri baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uturuki na Zanzibar
na Uturuki na kutumia fursa hiyo kueleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na
ziara aliyoifanya mwezi Februari 2011 alipofanya mazungumzo na Rais wa nchi
hiyo Abdullah Gul wakati huo ambapo katika maeneo waliyoahidi kushirikiana ni
pamoja na sekta ya afya.
Dk. Shein pia, alieleza
hatua alizozichukua akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa
kuanzisha Kitivo cha Madaktari katika chuo hicho huku akieleza azma ya
kuanzisha kufundishwa kwa Madaktari wa
meno hapa Zanzibar.
Rais Dk. Shein aliwahakikishia
viongozi na Wanajumuiya wa mradi wa (HIPZ) kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kushirikiana nao kwa kasi, ari na nia ile ile na kuendelea
kushirikiana nao kwa yote wanayoyafanya kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.
Alisema kuwa huduma hizo
za afya za meno katika hospitali hiyo hazikuwepo hapo kabla ambapo hivi sasa
mambo yameongezeka na vifaa vya kisasa vya Digital vipo vya kutosha na kuwataka
wananchi wa eneo hilo kuitumia vyema bahati na neema hiyo.
Alisisitiza haja ya kwa
wananchi kuvitunza vifaa hivyo vipya na vya kisasa katika Kitengo hicho cha
Kinywa na Meno katika Hospitali ya Kivunge na kuwataka kuthamini jitihada za (HIPZ)
za kuchangia na kusaidia huduma za afya hapa nchini. ”lazima tushirikiane nao
ili ndugu zetu hawa waendeleee kutusaidia”,alisisitiza Dk. Shein.
Nae Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed alisisistiza haja ya
wananchi kuthamini na kuzijali juhudi zinazochukuliwa na Mradi wa (HIPZ) sambamba na kuiga mifano yao huku
akiwapongeza wasimamizi wa mradi huo hapa nchini.
Aidha, Waziri Hamad alilaani
kitendo kinachofanywa na wale wote wanaosomeshwa na Serikali ndani na nje ya
nchi na hatimae wanaporudi hushindwa kuitumikia nchi yao na wananchi wenzao na badala
yake wanakwenda kufanya kazi sehemu nyengine kwa kisingizo cha mshahara mdogo.
Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Asha Ali Abdalla alieleza kuwa kwa hatua iliyofikia Hospitali ya Kivunge
tayari Hospitali hiyo imeshafikiwa daraja la kuwa Hospitali ya Wilaya na
mwelekeo ni kuendelezwa ili iweze kufikia daraja la Hospitali ya Mkoa.
Alieleza kuwa katika
kufanikisha hilo juhudi zinaendelea za kuimarisha utoaji wa huduma kwenye
Hospitali hiyo ambapo jengo jipya la ghorofa mbili kwa ajili ya wodi ya wazazi
na ya watoto linaendelea kujengwa na linategemewa kumaliza mwezi Julai 2019.
Meneja Mkuu wa Mradi wa (HIPZ)
kutoka Uingereza Ru MacDonald Alieleza juhudi za Mradi huo tokea kuanzishwa
kwake na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya
afya sambamba na kuziimarisha Hospitali ya Kivunge na Makunduchi.
Mapema Meneja wa (HIPZ) Zanzibar
Pamella Allard alisema kuwa (HIPZ) imeanzisha huduma nyingi za msaada katika
Hopsitali ya Kivunge na Makunduchi za kukabiliana na changamoto za kiafya kama
vile utapia mlo, ajali za kuungua, huduma za afya ya watoto njiti ambapo
mtazamo wao ni kutoa elimu kwa jamii hasa kwa maradi ya meno.
Aliongeza kuwa tangu
kuanza mwaka 2007 (HIPZ) imetumia Bilioni 5.5 ambapo kwa kufanya kazi pamoja na
Serikali sasa wana wafanyakazi wengi zaidi kuliko hapo mwanzo katika hospitazli
za Makunduci na Kivunge.
Mapema Dk. Shein
alitembelea jengo jipya lilojengwa la mama wajawazito na watoto na kupata
maelezo juu ya ujenzi huo na kutembelea wodi ya wazazi, maabara, wodi ya watoto
njiti na kuizindua Kitengo cha Kinywa na Meno kilichojengwa chini ya mradi wa
(HIPZ).
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment