Habari za Punde

WAZIRI MKUU ATOA SIKU 25 KWA WATUMISHI CHAMWINO *Ni wale washio nje ya kituo, wawe wamehamia ifikapo Desemba 15


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaametoa siku 25 kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Chamwino wanaoishi nje ya kituo chao cha kazi wawe wamehamia.

Pia amemkabidhi Mkuu wa wilaya hiyo Bibi Vumilia Nyamoga orodha ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Chamwino ambao wanaishi nje ya kituo cha kazi kwa hatua zaidi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba 20, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Chamwino.

“Ifikapo Desemba 15 mwaka huu watumishi wote wawe wamehamia katika kituo chao cha kazi. Sheria ya utumishi inamtaka mtumishi aishi katika maeneo ya kituo cha kazi.”

Waziri Mkuu amesema lazima watumishi wote wa umma wafuate sheria, kanuni na taratibu za utumishi na atakayeshindwa kuhamia atakuwa amejiondoa kwenye utumishi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wakuu wa idara na madiwani watambue vyanzo vyote vya mapato.

Amesema baada ya kuvitambua wasimamie utaratibu wa ukusanyaji kwa njia ya kielekroniki ili kuiwezesha halmashauri kupanga miradi na kuitekeleza kupitia fedha za ndani.

Pia Waziri Mkuu amekagua barabara za mitaa katika mji wa Chamwino zenye urefu wa kilomita 3.5 zinazojengwa kwa kiwango cha lami na kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo.

Baada ya kukagua barabara hizo, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa miundombinu ya majengo ya kituo cha Chamwino na kisha kuzungumza na wananchi waliofika  kituoni hapo. 

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
  S. L. P. 980,
  41193 – Dodoma
JUMAMOSI, OKTOBA 20, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.