Habari za Punde

Taasisi za kizalendo zaiomba ZEC kuwapa kipaumbele wakati wa uangalizi wa Uchaguzi

Na Takdir Ali,    Maelezo                                    06-11-2018 
Viongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC wameombwa kutoa kipao mbele kwa Taasisi za Kizalendo zinazoomba uangalizi wa uchaguzi ili kuondosha migogoro inayoweza kujitokeza kwa Taasisi za nje.
Akizungumza na Waandishi wa Habari huko Mpendae Katibu wa Jumuiya ya Mpendae  Youth  Forum Amani Shaabani Bakari,Jumuiya iliopata kibali cha uangalizi wa ndani katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jangombe amesema wakati umefika kwa Taasisi za Kizalendo kupewa uangalizi huo.
Amesema mara nyengine baadhi ya Taasisi za Kigeni zinaingiza mambo yao binafsi na kusababisha mvutano na Serikali jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma.
“Waangalizi wa nje hawaepukiki hata kidogo lakini lazima wachunguzwe kwa umakini kabla ya kupewa nafasi hizo ili wasije kuleta rapsha katika nchi yetu”asema Katibu huyo.
Amefahamisha kuwa Zanzibar ina Taasisi nyingi zenye sifa ya kupata kibali cha uangalizi wa ndani hivyo iwapo zec watatoa nafasi hizo kwa Wazalendo watafanya kazi kwa uzalendo na kujiamini zaidi.
Aidha amesema haipendezi hata kidogo kuona wanatoka waangalizi kutoka nje ya nchi wakati waangalizi wazalendo na wenye sifa wamekaa mitaani.
“Nafasi hizi tuachiwe sisi Wazalendo kwani mjenga nchi ni Mwanachi mwenyewe”alisema
Hata hivyo ameziomba taasisi za kizalendo kuweka mikakti maalum itakayowawezesha kukabiliana na ushindani wa taasisi za nje ya Zanzibar ili waweze kushiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika 2020.
Mbali na hayo ameiomba Zec kuyafanyia maerkebisho mapungufu madogo mabago yaliojitokeza katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jangombe ikiwemo kuzidi kuweka Makarani wenye vigenzo,kuboresha mazingira kwa Watu wenye ulemavu na kuweka huduma ya kwanza katika vituo vya kupigia kura.
Kwa upande wake Maryam Ali Muhammed Mjumbe wa Kamati Tendaji katika Jumuiya hiyo ameipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Wananchi kwa kuendeshs Uchaguzi huo kwa amani na utulivu,kuanzia kipindi cha Kampeni za vyama vya Siasa,Uchaguzi wenyewe na wakati wa kuhesabu kura na matokeo.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jangombe umefanyika Tarehe 27 mwezi uliopita na Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi kupitia Mgombea wao Ramadhani Hamza Chande aliepata asilimia 90.5 na kuwapita wagombea wa Cuf,Ada Tadea,DP,CCK,TLP,NRA,AAFP na SAU.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.