Habari za Punde

AWAMU YA KWANZA YA MRADI WA UCHUNGUZI WA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI ZANZIBAR YAMALIZIKA KWA MAFANIKIO

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akizungumza na Madaktari na Wataalamu wa Kichina walioshiriki awamu ya kwanza ya Mradi wa Uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi Hospitali kuu ya Mnazimmoja walipofika Ofisini kwake kumuaga
Mmoja ya Wataalamu walioshiriki Uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi Daktari Lamlat Hassan Nondo akipongezwa na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed baada ya kumkabidhi cheti, anaeshuhudia ni Balozi wa Mradi huo ambae pia ni Naibu Spika Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma.
Baadhi ya Madaktari wa Kichina na Zanzibar walioendesha Mradi wa Uchunguzi wa Saratani ya Kizazi Hospitali ya Mnazimmoja wakifurahia vyeti walivyokabidhiwa na Waziri wa Afya (hayupo pichani) katika hafla iliyofanyika Wizarani kwake Mnazimmoja
Madaktari na Wataalamu walioendesha Mradi wa Uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed na Balozi wa Mradi Mgeni Hassan Juma

Na Ramadhani Ali – Maelezo                                                29.12.2018
Jumla ya Wanawake 11 kati ya 3013 waliopimwa Saratani ya Shingo ya kizazi, awamu ya kwanza, wamegundulika kuwa na maradhi hayo na wengine 48 wameonyesha kuwa na dalili na hatua za kuwapatia matibabu zilianza baada ya kugunduliwa.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed alieleza hayo katika hafla ya kuwaaga na kuwapongeza Madaktari wa kichina, kutoka Jimbo la Jiangsu, baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya Mradi wa uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya kizazi ulioanza tarehe tatu na kumalizika tarehe 25 mwezi huu katika Hospitali ya Mnazimmoja.
Alisema katika awamu ya kwanza ya uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya kizazi, Wizara ya Afya ilipanga kuwafanyia uchunguzi akinamama 3000 lakini kutokana na mwamko wa wananchi kupenda kujua afya zao idadi hiyo iliongezeka na kufikia 3013.
“Hatukufikiria kwamba wanawake wangejitokeza kwa idadi kubwa kama hii kufanyiwa uchunguzi, lakini kila siku idadi ya akinamama ilikuwa ikiongezeka, ni maendeleo mazuri kwa wananchi wetu,”alisema Waziri wa Afya.
Aliwataka akinamama wa Zanzibar kujitayarisha kwa uchunguzi wa awamu ya pili ya Mradi huo mwakani ambapo wamepanga kuwafanyia uchunguzi wanawake 10,000 katika Hospitali mbali mbali za Unguja na Pemba.
Alisema wajibu wa kwanza wa Wizara ya Afya ni kukinga na baadae kutiba, hivyo uamuzi wa kufanya uchunguzi wa afya na kujua tatizo mapema ni rahisi kulipatia ufumbuzi kuliko kuliacha kukua na kuanza kuleta madhara.
Aliupongeza uongozi wa Jimbo la Jiangsu nchini China kwa misaada mbali mbali inayotoa hasa sekta ya afya kwa Zanzibar tokea mwaka 1964 na sasa wameanzisha hatua nyengine ya kufanya uchungzi wa maradhi yanayowasumbua wananchi.
Alitoa ombi maalum kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuongeza Wataalamu na Vifaa tiba katika awamu ya pili ya Mradi huo ambao utawahusu watu wengi zaidi na hospitali mbali mbali kinyume na ule wa awamu ya kwanza ambapo uchunguzi ulifanywa Hospitali ya Mnazimmoja pekee.
Balozi wa Mradi wa Uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi Mgeni Hassan Juma alisema Serikali inataka kuona uchunguzi wa Saratani ya Shigo ya Kizazi ni jambo la kawaida na inajiandaa kuwapa mafunzo Madaktari wazalendo na kuongeza vifaa ili kila Hospitali iweze kufanya uchunguzi baada ya kumalizika Mradi wa sasa wa miaka minne unaondeshwa kwa pamoja na Serikali ya China na Zanzibar.
Mh. Mgeni ambae ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi aliwaomba akinamama wajiandae kwa awawamu ya pili ya uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya kizazi utakaoza mwezi wa sita 2019 ili watakaogundulika kuwa na dalili za maradhi hayo wapatiwe matibabu mapema kwani ni maradhi yanyotibika yanapowahiwa hatua za awali

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.